Na Mwandishi Wetu
WATU 717 ambao walikuwa wanashiriki
ibada ya Hijja nchini Saudi Arabia wamefariki kutokana na kukanyagana karibu na
mji mtakatifu wa Makka, maofisa wa Saudi wamesema.
Watu wengine 863 wamejeruhi katika
tukio hilo lililotokea Mina, ambako mahujaji milioni mbili walikuwa wakishiriki
katika shughuli ya mwisho ya ibada hiyo kubwa ya Hijja.
Ni ajali kubwa zaidi kuwahi kutokea
katika miaka 25 ya Hijja.
Maandalizi ya ibada hiyo ambayo ni
nguzo ya tano ya dini ya Kiislamu yaligubikwa na fadhaa baada ya winchi
kuanguka katika Msikiti Mkuu wa Makka mwezi huu na kuua watu 109.
Mahujaji walikuwa wakisafiri kwenda
Mina, bonde kubwa kiasi cha kilometa tano kutoka Makka, wakati wa mahujaji
kurusha mawe katika nguzo saba zinazoitwa Jamarat ambazo zinawakilisha shetani.
Nguzo hizo zimesimama katika maeneo
matatu, ambako Shetani inaaminika alijaribu kumrubuni Nabii Abraham.
Watu walikuwa wakielekea kwenda
kumrushia mawe shetani wakati wengine walikuwa wakirudi upande mwingine. Kisha
ikaanza kuwa vurugu na ghafla watu wakaanza kuanguka.
Kulikuwa na watu kutoka Nigeria,
Niger, Chad na Senegal miongoni mwa mataifa mengine. Watu walikuwa
wakikanyagana ili kwenda sehemu salama na hivyo ndivyo vifo vilivyotokea.
Watu walikuwa wakitaja jina la
Mwenyezi Mungu wakati wengine wakilia wakiwamo watoto wadogo na wachanga.
Wengine walianguka wakiomba msaada, lakini hakukuwapo na yeyote wa kufanya
hivyo. Kila mmoja alionekana kuwa na lake.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Makka,
viongozi wa Tanzania akiwamo Mufti Shekhe Mkuu wa Tanzania, Abubakari Zubery,
walieleza wakati tukienda mitamboni kwamba hakukuwa na taarifa ya kuwapo kwa
mwathirika ambaye ni Mtanzania, na taarifa rasmi zinatarajiwa kutolewa leo.
Katika hatua nyingine, Serikali imesisitiza
amani, upendo na mshikamano katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba 25, huku ikionya kuwa itakabiliana na wote watakaofanya vitendo
vitakavyoashiria kutaka kuvunja amani ya nchi wakati huu wa kampeni, wakati wa
uchaguzi na baada ya uchaguzi.
No comments:
Post a Comment