Na Mwandishi Wetu
MABINGWA watetezi wa Ligi
Kuu Tanzania Bara Yanga, leo wanashuka tena kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar
es Salaam kucheza na JKT Ruvu.
Yanga inashuka dimbani
ikiwa inaongoza katika msimamo wa ligi hiyo baada ya kushinda mechi zake mbili
na kujikusanyia pointi zote sita huku ikifunga mabao matano.
Katika mchezo wa kwanza,
Yanga ilishinda Wagosi wa Kaya Coastal Union kwa mabao 2-0 kabla ya kuibuka na
ushindi mwingine wa mabao 3-0 dhidi ya Prisons ya Mbeya.
Timu hiyo itacheza mechi
nne mfululizo kwenye uwanja wake wa nyumbani kwani baada ya mchezo wa leo,
itashuka tena dimbani kumenyana na watani zao wa jadi Simba Septemba 26 kabla
ya kuanza kutoka wakati itakapocheza na Mtibwa Sugar Septemba 30 kwenye Uwanja
wa Jamhuri Morogoro.
Yanga inahitaji ushindi
katika mchezo huo ili iweze kuzidi kukalia kiti hicho na kufanya biashara
mapema kabla ya kuhesabu mapato jioni.
Yanga imeshafunga mabao
matano katika mechi mbili na haijafungwa bao hata moja, hivyo inaonesha jinsi
safu yake ya ushambuliaji kama akina Donald Ngoma, Hamisi Msuva, Amiss Tambwe
na wengineo ilivyo na uchu wa mabao, hivyo mabeki wa maafande wa JKT Ruvu
watakuwa na kibarua kigumu cha kuwazuia wasifunge.
Hata hivyo, kikosi cha JKT
Ruvu kinachofundishwa na mchezaji na kocha wa zamani wa Yanga, Fred Minziro
hakitakubali kufa kikondoo, kwani kinazihitaji sana pointi hizo tatu ili
kurejesha matumaini ya kufanya vizuri.
JKT Ruvu ndio inaburuza
mkia baada ya kufungwa mechi zote mbili za mwanzo na kuifanya kuwa na kazi
kubwa ya kufanya ili kutoka na pointi zote tatu au moja kwa kutoka sare.
Kocha wa JKT Ruvu, Minziro
alikiri kuanza vibaya kwa ligi hiyo lakini alisema leo hawatakubali kufungwa
licha ya uimara wa Yanga ambayo ina wachezaji wengi wazuri, wakiwemo wa kutoka
nje ya nchi.
Alisema kuwa timu yao
ilianza vibaya mechi mbili za mwanzo baada ya wachezaji wake kutokuwepo katika
maandalizi ya mwisho baada ya kuwa katika mashindano ya majeshi nchini Uganda
kwa takribani siku 11.
Pia alisema timu yake ina
majeruhi wawili, lakini alikuwa na imani siku zinavyokwenda timu hiyo itazidi
kuimarika na kufanya vizuri katika mechi zao zijazo.
Nahodha wa Yanga, Nadir
Haroub alisema kuwa wamejipanga vizuri kuhakikisha wanaondoka na pointi zote
tatu ili kuzidi kung’ara katika ligi hiyo
inayoshirikisha timu 16.
Mechi zingine leo ni Stand
United watachea na African Sports katika mchezo utakaofanyika kwenye uwanja wa
Kambarage mjini Shinyanga, huku Mgambo Shooting itawakaribisha wana Lizombe
Maji Maji ya Songea katika uwanja wa Mkwakwani Tanga.
Mbeya City wenyewe watakuwa
wageni wa ndugu zao wa Tanzania Prisons katika mchezo utakaofanyika kwenye
Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Wakati Mbeya City ni ya
nane baada ya kuwa na pointi tatu kutoka katika mechi mbili walizocheza,
Tanzania Prisons wenyewe ni wa pili kutoka mkiani wakiwa hawana pointi hata
moja baada ya kuchapwa mechi zote mbili za mwanzo.
Mechi hizo zitaendelea tena
kesho Jumapili kwa Mwadui ya Shinyanga kuikaribisha Azam FC huku kocha wa
wenyeji hao Jamhuri Kihwelu kutamba kuibuka na ushindi.
Mtibwa Sugar watacheza na
Ndanda FC katika mchezo utakaofanyika kwenye uwanja wa Manungu, Turiani wakati
Simba baada ya kuanza kwa kucheza mechi mbili ugenini, kesho kwa mara ya kwanza
itakuwa kwenye Uwanja wa Taifa ikicheza na Kagera Sugar.
African Sports wenyewe
watakuwa mwenyeji wa Toto Africans ya Mwanza katika mchezo utakaofanyika kwenye
Uwanja wa Mkwakwani Tanga.
No comments:
Post a Comment