Meneja Uhusiano wa Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro, Adam Akyoo, (kushoto) akimkabidhi mfano wa hundi Katibu Mkuu wa
TASWA, Amir Mhando. Katikati
ni Katibu Msaidizi wa TASWA, Grace Hoka.
|
MAMLAKA ya
Hifadhi ya Ngorongoro ( NCAA),imetoa Sh. 10, 486,000 kwa ajili ya kudhamini
tuzo za Wanamichezo Bora waliofanya vizuri zaidi katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wa
Rais Jakaya Kikwete.
Tuzo hizo
zinazoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA
zinatarajiwa kufanyika Oktoba 8, mwaka huu ukumbi wa Mlimani City, Dar es
Salaam, ambapo pia TASWA itatoa Tuzo ya Heshima kwa Rais Kikwete ikiwa ni
kuthamini mchango wake kwa sekta ya michezo katika uongozi wake.
Akizungumza
katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Meneja Uhusiano wa
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Adam Akyoo, alisema wameamua kusaidiana na
TASWA kwa sababu Rais Kikwete ni mdau mkubwa wa michezo na pia wa masuala ya
utalii.
"Dk. Kikwete ni mdau mkubwa wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwani kwa
kipindi chote ambacho amekuwa Waziri wa Mambo Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
na hatimaye Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania ametembelea hifadhi hii mara nyingi zaidi kuliko viongozi wengine wote wa Taifa
letu waliomtangulia.
"Pia amekuwa mdau muhimu na wa mstari wa mbele
wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro katika
kutangaza vyema vivutio vya watalii vya hifadhi ya Ngorongoro katika
mataifa mbalimbali duniani alikokwenda kwa ziara za kikazi.
"Jambo hili limeleta watalii wengi nchini
kutoka mataifa mbalimbali dunini. Vile
vile ziara zake za mapumziko hifadhini wakati wa sikukuu mbalimbali
zimewahamasisha sana Watanzania
walio wengi kutembelea hifadhi hii kutoka kote nchini na hata nchi jirani,"
alisema Akyoo.
Pia alisema
waandishi wa habari ni wadau wakubwa na muhimu katika harakati za utalii na
ndiyo sababu wameamua kuisaidia TASWA ifanikishe shughuli yake.
Kwa upande wake,
Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando aliishukuru mamlaka ya hifadhi hiyo na kusema
kuwa msaada huo ni mkubwa na kuomba wadau wengine waungane nao kufanikisha
jambo hilo.
"Kama tulivyosema bajeti yetu ni Sh milioni
130, juzi (Jumatano) tulipata watu wa GSM Foundation waliotupa Sh. Milioni 50,
tunaomba na
wengine tushirikiane nao katika hili,"
alisema Mhando.
Alisema TASWA
imeamua kuandaa hafla ya wanamichezo kumuaga Rais na pia kumpa tuzo kwa vile
wakati wa uongozi wake amefanya mambo makubwa katika sekta ya michezo.
Kwa mujibu wa
Mhando, wanamichezo pia watatumia tuzo hizo zilizoandaliwa na TASWA kumuaga
Rais Kikwete anayemaliza muda wake kikatiba baada ya Uchaguzi Mkuu wa Rais,
Wabunge na Madiwani Oktoba 25, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment