Monday, 16 April 2018

RC Iringa Kuzindua Michezo ya Mei Mosi Aprili 21

Baadhi ya wachezaji wa timu ya wanaume na wanawake ya kuvuta kamba ya Uchukuzi leo wakifanya mazoezi katika shule ya msingi ya Mlandege wakijiandaa na mashindano ya Mei Mosi yanayoanza kesho kwenye uwanja wa Samora mkoani Iringa.

Na Bahati Mollel-TAA,Iringa
MKUU wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza Aprili 21, 2018 anatarajiwa kuzindua rasmi michezo ya Kombe la Mei Mosi kwenye uwanja wa Samora mjini hapa.

Katibu Mkuu wa Kamati ya Michezo ya Mei Mosi, Award Safari amesema leo kuwa michezo ya ufunguzi itafanyika leo kwenye uwanja wa Samora, lakini uzinduzi rasmi unatarajiwa kufanywa na Mkuu wa mkoa.

Safari amesema michezo hiyo inatarajiwa kushirikisha wanamichezo 1,000 kutoka katika timu 20 za wizara, taasisi na idara za serikali ambazo baadhi ni Ofisi ya Rais Ikulu, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Tumbaku ya Morogoro, Tanesco, Wizara ya Mali Asili na Utalii, Chuo cha Mipango Dodoma, Wakala wa Taifa wa Chakula.

Nahodha msaidizi wa timu ya Kamba ya wanawake, Tabu Cosmas (mwenye ushungi) akiwa na wachezaji wengine wa timu ya wanaume ya kamba ya Uchukuzi wakiwa kwenye mazoezi ya kujiandaa na mashindano ya Kombe la Mei Mosi katika uwanja wa shule ya msingi Mlandege. Mashindano hayo yatafunguliwa rasmi Aprili 21, 2018 na Mkuu wa mkoa wa Irimnga, Mhe. Amina Masenza katika uwanja wa Samora.

Baadhi ya timu nyingine ni Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), Chuo Kikuu cha Mkwawa, timu ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa na Hifadhi ya Ngorongoro.

Safari amesema mashindano hayo ambayo mabingwa wake watakabidhiwa zawadi ya kombe na Mhe. Rais John Pombe Magufuli siku ya sherehe za Wafanyakazi Mei Mosi, yatashirikisha michezo ya netiboli, soka, kuvuta kamba, baiskeli, karata, draft, mbio za marathon na bao.

Daktari wa timu ya Uchukuzi, Hawa Senkoro (wa pili kushoto) akijumuika katika mazoezi ya timu ya kamba katika yaliyofanyika leo kwenye uwanja wa shule ya Msingi Mlandege wakijiandaa na mashindano ya Mei Mosi yanayoanza kesho katika uwanja wa Samora, na yatazinduliwa rasmi April 21, 2018 na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Amina Masenza.

Naye Katibu Mkuu wa timu ya michezo ya Uchukuzi, Mbura Tenga ametamba timu yake kuendeleza wimbi la ushindi kwa kutetea vyema ubingwa wao kwenye michezo ya kuvuta kamba, kuendesha baiskeli, netiboli na karata kwa wanawake na wanaume.

Tenga amesema timu hiyo ambayo tayari imeshafika Iringa ikiwa na wachezaji 78 imejiandaa vyema kwa kufanya mazoezi ya nguvu na kupata mechi za kirafiki katika viwanja vya shule ya sekondari ya Airwing jijini Dar es Salaam.

Kocha Suleiman Kingsley (mwenye trucksuit), akielekeza mazoezi kwa wachezaji wa timu ya soka ya Uchukuzi yaliyofanyika kwenye viwanja vya Chuo Kikuu cha Mkwawa, wakijiandaa na mashindano ya Mei Mosi yatakayoanza leo kwa kushirikisha michezo mbalimbali. Michuano hiyo itazinduliwa rasmi Aprili 21, 2018 na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Amina Masenza.

“Wachezaji wetu wote wapo katika hali nzuri kiafya na hakuna anayeumwa na tayari tupo hapa Iringa kuanza mashindano, kwa kweli tumejiandaa vizuri na tupo tayari kwa mashindano haya, ambayo baadhi ya michezo tulitwaa ubingwa wa kwanza, pili na tatu na tunaahidi tutarejesha vikombe vyetu tumekuja kikazi zaidi,” amesema Tenga.

  Kipa Kennedy Mwamteto (kushoto) wa timu ya Uchukuzi akifanyishwa mazoezi na kocha wake Alter Mollel (kulia) huku kipa mwenzake Willy Barton (mwenye namba 17 mgongoni), wakifanya mazoezi kwenye viwanja vya Chuo Kikuu cha Mkwawa ya kuijiandaa na mashindano ya Mei Mosi yatakayoanza leo kwenye uwanja wa Samora.     


Bayi Apokewa Kifalme Akirejea Kutoka Gold Coast

Filbert Bayi mara baada ya kutua kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) akitokea Gold Coast, Australia, ambako alipewa tuzo ya kutukuka. Kushoto ni mkewe, Anna Bayi.

Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imezitaka kampuni mbalimbali kujitokeza kudhamini riadha badala ya kung’ang’ania soka.

Bayi akiwasili JNIA.
Hayo yameelezwa mjini Kibaha na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Everist Ndikilo  katika hafla ya kumpongeza mwanariadha wazamani wa Tanzania, Filbert Bayi kwa kupata tuzo iliyotukuka iliyotolewa na Shirikisho la Michezo ya Jumuiya ya Madola (CGF).
Bayi alipewa tuzo hiyo wiki iliyopita wakati wa michezo hiyo iliyomalizika juzi Gold Coast, Australia kufuatia mchango wake katika michezo hiyo, ikiwemo kuweka rekodi ya Madola iliyodumu kwa miaka 44 sasa bila kuvunjwa.

Mwanariadha huyo nguli, aliweka rekodi ya dunia sambamba na ile ya Jumuiya ya Madola ya mbio za meta 1500 mwaka 1970 wakati ile ya dunia ilivunjwa baada ya miaka mitano, lakini ya Madola bado anaishikilia hadi leo.

Wanafunzi wa shule yake wakimsubiri kwenye Kiwanja cha Ndege.
Ndikilo alisema kuwa mafanikio ya Bayi yalikuja kutokana na juhudi zake binafsi pamoja na uzalendo kwa nchi yake.

Alisema makampuni yameng’ang’ania kudhamini soka, hivyo aliyaomba kujitokeza kudhamini na riadha ili kuuletea mafanikio mchezo huo, ambao umeiletea sifa kubwa nchi.
Ndikilo alimpongeza Bayi kwa tuzo hiyo na kuwataka wanariadha chipukizi kujituma zaidi katika mchezo huo, kwani juhudi zinalipa kama alivyofanikiwa Bayi na sasa Jumuiya ya Madola imeamua kumuenzi.

Alisema kuwa mkoa wake uko tayari kushirikiana na kusaidia taasisi yoyote, ambayo itakuwa tayari kusaidia kudhamini mchezo wa riadha ili kuhakikisha unakuwa.

Kwenye Kiwanja cha Ndege, Bayi alipigwa na mshituko baada ya kukutana mapokezi makubwa kutoka kwa wadau wa michezo wa mkoa wa Pwani pamoja na wanafunzi na walimu wa shule yake na kupewa shada la maua huku ukiwa na mabango ya kumpongeza.

Bayi aliwasili kutoka Gold Coast na kupokewa katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) na wadau mbalimbali wa michezo kabla ya kuondoka kwa msafara  mzito ulioongozwa na pikipiki ya usalama barabarani na gari la polisi kwenda Mkuza Kibaha, alikoandaliwa sherehe hiyo ya kumpongeza.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Everisy Ndikilo akimpongeza Bayi pamoja na Kamanda wa Polisi (RPC) wa mkoa huo, Jonathan Shana (kulia) 

Awali, Makamu wa Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Henry Tandau alisema kuwa tuzo hiyo imetokana na utendaji bora na jitihada za Bayi katika riadha, hasa kuvunja rekodi hiyo, ambayo sasa itadumu hadi mwaka 2022.

TAA Kukusanya Bilioni 134, Waanzisha Tozo Mpya

Waziri wa Uchukuzi na Mawasiano, Makame Mbarawa akizungumza wakati wa uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) jijini Dar es Salaam leo.

Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) inatarajia kukusanya kiasi cha Sh bilioni 134 kupitia viwanja vyake kwa mwaka wa fedha 2018-19, imeelezwa.

Pia Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Richard Mayongela amesema leo kuwa mamlaka yake iko mbioni kuanzisha tozo mpya ya usalama, ambayo huko nyuma haikuwepo na inatarajia kuwaongezea mapato.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Rochard Mayongela akizungumza baada ya uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi wa TAA.
Mayongela alisema kuwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukizi, Profesa Makame Mbarawa ameridhia kuanzishwa kwa tozo hiyo ya usalama, ambayo watatozwa abiria wanaondoka kupitia viwanja vya ndege hapa nchini.

Hayo yamesemwa leo na Mayongela, ambaye ni mwenyekiti wa baraza hilo la wafanyakazi la TAA, ambalo ni la 21 wakati likizinduliwa leo katika jengo la NSSF Ilala Jijini Dar es Salaam.
Anasema Waziri ameridhia kuanzishwa kwa tozo hiyo ya usalama kutokana na changamoto zilizopo za kiusalama katika viwanja vyetu vya ndege.

Alimshukuru Waziri kwa kufika licha ya majukumu mengi aliyonayo katika kpindi hiki cha Bunge la Bajeti kinachoendelea mjini Dodoma, ambapo alisema kuwa wafanyakazi wanataka kusikia maslahi yao yanaboreshwa.
Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) wakati wa uzinduzi wa baraza hilo leo.
Mbarawa aliwapongeza wafanyaakzi wote waliochaguliwa kuwa wajumbe wa baraza hilo na kuwaambia kuwa kazi ndio kwanza inaanza na wao ndio injini na ndio wanaangalia maslahi ya wafanyakazi, kwani wao ndio kiungo kati ya wafanyakazi na uongozi.

Alisema Serikali inawathamini sana na wako pale kisheria na aliwataka kushirikiana na serikali, ambapo pia aliwakumbusha majukumu yao baada ya kuchaguliwa.
Alitaka wajumbe wa baraza hilo kujiuliza wamewafanyoia nini wadau wa viwanja vya ndege na wamewafanyia nini Watanzania na kupanga bajeti vizuri na kama hawajafikia amewataka kuhoji sababu za kutofikia bajeji ya mwaka 2017-18 na kama wamefikia malengo wajipongeze.

Pia amewataka kujiuliza sababu za viwanja vya ndege Tanzania Bara kutokuwemo katika orodha ya viwanja 10 bora vya ndege barani Afrika, wakati Zanzibar kimo katika viwanja bora.
Alihoji sababu za TAA kushindwa hata kununua gari la zima moto na badala yake kusubiri fedha kutoka Serikali Kuu wakati wana vyanzo vingi vya mapato, ambavyo kama wangevitumia vizuri wangeweza kujinuliwa wenywe magari hayo.

Alisema Watanzania na wasafiri wengi bado wana imani na viwanja vya ndege vya Tanzania, lakini tatizo ni kasoro ndogo ndogo ndizo zinafanya tushindwe kuwa miongoni mwa viwanja bora barani Afrika.

Alisema kama hatuko katika viwanja bora huo ndio mwanzo wa kupoteza watalii kwani wengi watakimbilia Kenya ambako kuna viwanja bora kuliko sisi na wakipungua, basi wafanyakazi wengine watapunguzwa.

Aliwataka kufanyakazi kwa bidii ili kujiongezea mapato na kubuni miradi mingine, ambayo itawawezesha kupata fedha, na alimpngeza Mayongela kwa kuwa nampango wa kununia magari sita kwa mpigo, kitu ambacho huko nyuma hakijawahi kufanywa.

Thursday, 12 April 2018

DRC Wawapaisha Taifa Stars Viwango Fifa


Na Mwandishi Wetu
TANZANIA imepanda kwa nafasi tisa katika Viwango vya ubora wa soka Ulimwenguni vilivyotolewa na Shirikisho la Kimataifa la Soka, FIFA, mapema leo.

Awali, Tanzania ilikuwa inashika nafasi ya 146 na sasa inashika nafasi ya 137 baada ya kukusanya jumla ya pointi 223 kutoka alama 186  ilizopata mwezi uliopita.

Kupanda kwa Tanzania kunatokana na kucheza michezo miwili ya kirafiki ya kimataifa katika kalenda ya FIFA, ambapo ilicheza na Algeria na kufungwa mabao 4-1 na kuifunga DR Congo kwa mabao 2-0.

Katika Ukanda wa Afrika Mashariki, Uganda imeendelea kushika usukani ikiwa katika nafasi ya 74, Kenya nafasi ya 113, Rwanda nafasi ya 123, Sudan ya 126 na Sudan Kusini inashika nafasi ya 155.

Kwa upande wa Afrika, Tunisia inaongoza ikiwa nafasi ya 14 duniani baada ya kupanda kwa nafasi tisa wakifuatiwa na Senegal  iliyopo katika nafasi ya 28 na DR Congo wapo nafasi ya 38.

Ujerumani inaongoza ikifuatiwa na Brazil, Ubelgiji nafasi ya nne ipo Ureno na Argentina inakamilisha tano bora za FIFA.

Simba Yazidi Kuukaribia Ubingwa Ligi Kuu Bara


Na Mwandishi Wetu
VINARA wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara, Simba wanazidu kuukaribia ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bada, baada ya kuifunga Mbeya City kwa mabao 3-1 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.

Kwa ushindi huo, Simba imefikisha pointi 55 ikifunga mabao 55 katika michezo 23, ikifuatiwa na mahasimu wao, Yanga waliopo katika nafasi ya pili wakiwa na pointi 47 katika michezo 22 na nafasi ya tatu Azam yenye pointi 45 katika michezo 23.

Mabao ya Simba yalifungwa na Emmanuel Okwi, John Bocco na Asante Kwasi, huku lile la kufutia machozi la Mbeya City likiwekwa kimiani na Frank Ikobela.

Simba ilianza kwa kasi mchezo huo na kupata bao la uongozi dakika ya 16 lililofungwa na Okwi, likitokana na shuti la  Bocco lililopanguliwa na kipa wa City, Owen Chaima kuzagaa eneo la hatari.
Dakika 29 Bocco alipata nafasi ya wazi na kushindwa kuitumia baada ya kupiga mpira pembeni ya goli lakini dakika 32 baadaye Kwasi akaifungia Simba bao la pili kwa kichwa akipata krosi ya Shiza Kichuya.

Kabla ya wekundu hao kufunga bao la tatu dakika 35 lilifungwa na Bocco kutokana na krosi ya Shomari Kapombe, tayari City walifunga bao dakika 34 lililotokana na kona iliyochongwa na Danny Joram na kmkuta Ikobelo na kuujaza wavuni kwa kichwa.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Simba ilikuwa mbele mabao 3-1 wakiongoza kwa kufanya mashambulizi mengi lakini pia, walitumia faida ya wapinzani waliotumia muda mwingi kujilinda.

Kipindi cha pili Simba ilikuja na mbinu za kujihami na kushambulia kiasi  na wapinzani wao walikuja kwa kasi wakitafuta nafasi ya kufunga lakini walishindwa kutumia nafasi kadhaa walizopata. Dakika ya 65 Victor Hangaya nusura afunge kipa wa Simba Manula aliudaka.

Pia, Simba nusura ifunge dakika ya 53 mpira uligonga mwamba na dakika ya 57 Kichuya alipiga shuti kali golini lilipanguliwa na Chaima.

Hadi dakika 90 zinamalizika hakuna aliyeongeza bao na Simba ikiibuka na pointi tatu muhimu.

Michezo mingine iliyochezwa jana, Mtibwa imeshinda bao 1-0 dhidi ya Ndanda huku mchezo wa Ruvu Shooting dhidi ya Azam ukiahirishwa kutokana na mvua kubwa kunyesha Mlandizi.

Vikosi Simba;Aishi Manula, Nicholaus Gyan/James Kotei dk.87, Asante Kwasi/Mohamed Hussein dk. 73, Juuko Murshid, Yusufu Mlipili, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Shomari Kapombe, Emmanuel Okwi, John Bocco/Laudit Mavugo dk. 79 na Shiza Kichuya.

Mbeya City:Owen Chaima, Rajabu Isihaka, Majaliwa Shabani, Ally Lundenga, Ramadhan Malima, Haruna Shamte, Eliud Ambokile, Danny Joram/Danny Joram dk. 60, Victor Hangaya/Godfrey Milla dk. 76, Babu Ally/Hamidu Mohamed dk.43 na Frank Ikobela.

Wednesday, 11 April 2018

Simba Kibaruani Ikiikaribisha Mbeya City Taifa


Na Mwandishi Wetu
WEKUNDU wa Msimbazi na Vinara wa Ligi Kuu Bara Simba, kesho inashuka dimbani kukipiga na Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa.

Simba, inashuka dimbani ikihitaji pointi tatu muhimu ili kujisogeza zaidi kwenye mbio za kuwania ubingwa wa ligi hiyo, wakati Mbeya City ikihitaji nafasi ya saba.

Kuelekea mchezo huo Wekundu wa Msimbazi watakuwa na faida ya urejeo wa wachezaji wao watatu, Juuko Murushid, James Kotei na Erasto Nyoni, ambao walikua wanatumikia adhabu yao ya kadi tatu za njano kwa kila mmoja.

Tayari wachezaji hao wamemaliza adhabu hiyo na leo watakuwa sehemu ya kikosi cha Simba.

Aidha, Mbeya City inawakosa wachezaji wake muhimu ambao ni,John Kabanda na Hassan Mwasapili, ambao wana matatizo tofauti.

Kocha wa timu hiyo, Ramadhani Nswanzurimo alisema pamoja na kuwakosa nyota hawa bado ana matumaini ya kuondoka na pointi tatu kwenye mchezo huo, kwani tayari ameandaa mbadala wa wachezaji hao.

Alitaja kuwa wachezaji, Haruna Shamte na Rajab Isihaka watachukua nafasi hizo kwa ajili ya kuhakikisha wanaidondosha Simba katika mchezo huo.

Mchezo huo utakuwa wa raundi ya 23 kwa Simba, lakini 24 kwa Mbeya City,  ambaye mpaka sasa imefikisha pointi 26 na wapinzani wao wakiwa kileleni kwa alama 52 kwenye msimamo wa ligi.

Michezo mingine itakayopigwa leo ni Mtibwa Sugar ambao wamekuwa na mwenendo mzuri hivi karibuni itacheza na Ndanda katika dimba la Manungu Mkoani Morogoro, wakati Azam FC itakuwa wageni wa Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mabatini Pwani.

Yanga Yapunguzwa Kasi Mbio za Ubingwa Ligi Kuu


Beki wa Yanga, Hassan Kessy (kushoto) akijaribu kuwatoka wachezaji wa Singida United, Kiggi  Makasi (kulia) na Mudathir Yahya wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana na kumalizika kwa sare ya 1-1.

Na Mwandishi Wetu
MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga jana walipunguzwa kasi katika mbio za kutetea taji hilo baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Singida United, katika mchezo wa ligi hiyo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kwa matokeo hayo, Yanga imefikisha pointi 47 na kuifanya sasa kupitwa na watani zao Simba kwa pointi tano.

Kwa matokeo hayo ni dhahiri kuwa Yanga imeendelea kuwa mnyonge wa Singida kwa kushindwa kuifunga kwa mara ya tatu. Mchezo wa raundi ya kwanza kwenye Uwanja wa Namfua walitoka suluhu, wakati katika Kombe la Shirikisho (FA), walifungana 1-1 kabla ya Yanga kutolewa kwa penalti 4-2.

Sare hiyo inazidi kuisafishia Simba nafasi ya kuwania taji la ligi ikiendelea kubaki kileleni kwa pointi 52 na Yanga ikiendelea kuwa katika nafasi ya pili kwa pointi 47 zikitofautiana pointi tano, huku Singida United ikifikisha pointi 37.

Singida ndio ilikuwa ya kwanza kupata bao la uongozi dakika ya kwanza lililofungwa na Salita Kambale baada ya kupata krosi nzuri ya Kigi Makasi .

Katika mchezo huo, dakika 45 beki Abdallah Shaibu ‘Ninja’ aliisawazishia Yanga kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na Ibrahim Ajibu.

Kipindi cha kwanza kilimalizika Yanga 1-1. Kipindi cha pili Yanga walikuja kwa kushambulia zaidi lakini tayari Singida United walionekana kama wanaitaka sare baada ya kuonekana kuzuia zaidi.

Awali, kipindi cha kwanza Singida ilifanya mabadiliko kwa kuwatoa kipa Mustapha Barthez na kuingia Peter Manyika dakika ya 38. Pia, dakika ya 42 Shafiq Batambuze alitolewa na kuingia Salum Chuku na dakika ya 68 alitoka Nizah Khalifan na kuingia Yusufu Kagoma.

Yanga ilitengeneza nafasi nyingi za kufunga na kushindwa kuzitumia kupitia kwa Yusufu Mhilu, Ajibu na Chirwa kwa vipindi tofauti.

Pia, ilifanya mabadiliko kipindi cha pili kwa kuwatoa Pius Buswita na kuwaingiza Juma Mahadhi dakika ya 73, Ajibu na kuingia Geofrey Mwashiuya dakika 78 lakini haikusaidia chochote kwani hadi mpira unaisha matokeo yaliendelea kubaki sare ya bao 1-1.

Vikosi vilikuwa: Yanga; Youthe Rostand, Hassan Kessy, Haji Mwinyi, Abdallah Shaibu, Kelvin Yondani, Papy Kabamba, Yusufu Mhilu, Pius Buswita, Obrey Chirwa, Raphael Daud na Ibrahim Ajibu.

Singida United; Ally Mustapha, Miraji Adam, Shafik Batambuze, Malik Antir, Kennedy Juma, Mudathir Yahya, Deus Kaseke,Kenny Ally, Kambale Salita, Nizah Khalifan na Kigi Makasi.

Ndege Yaanguka Algeria Leo, Yaua Watu 257


ALGIERS, Algeria
WATU 257 wamekufa baada ya ndege ya jeshi kuanguka Kaskazini ya Algeria, wizara ya ulinzi inasema.

Tukio hilo limetokea muda mfupi baada ya ndege kuondoka kutoka katika kiwanja cha ndege cha jeshi cha Boufarik kilichopo jirani na mji mkuu wa Algiers asubuhi.

Wengi waliokufa ni askari na familia zao, kwa mujibu wa wizara ya ulinzi. Wafanyakazi 10 wa ndege hiyo nao waliuawa katika ajali hiyo.

Hatahivyo, bado haijawekwa wazi kilichosababisha ajali hiyo.
Kiongozi wa jeshi ameamuru kufanyika kwa uchukuzi ili kujua chanzo cha ajali hiyo, na aliahidi kutembelea eneo la tukio.

Ndege nyigine iliyoua watu wengi tangu Julai mwaka 2014,ilitokwa wakati watu  298 waliokuwa ndani ya ndege ya Malaysia Airlines namba MH17 walipokufa wakati ilipotunguliwa mashariki ya Ukraine.

Hiyo ilikuwa ajali ya pili kuuawa watu wengi katika ajali ya ndege tangu mwaka 2003.

Mamlaka zinafanyia kazi kutambua mahiti  ya waliokufa katika ajali hiyo. Picha za video kutoka eneo la tukio linaonesha moshi ukitoka katika mabaki ya ndege hiyo.
Ndege hiyo aina ya Ilyushin Il-76, ilikuwa ikisafiri kutoka Bechar kusini-magharibi ya nchi hiyo.

Nane Bora Ligi ya Wanawake Kuendelea Aprili 21

Na Mwandishi Wetu
VINARA wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara, JKT Queens wanatarajia kushuka dimbani Aprili 21 kucheza na Simba Queens kwenye Uwanja wa Mbweni nje kidogo ya jijini la Dar es Salaam.

Akizungumza jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Cliford Ndimbo alisema hatua ya Nane Bora, inatarajia kuendelea Aprili 21 kwenye viwanja vinne tofauti.

“Ligi ya wanawake hatua ya Nane Bora ilisimama kupisha maandalizi ya timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) iliyokuwa kambini kujiandaa na mchezo wa kufuzu fainali za Africa kwa Wanawake, hivyo sasa itaendelea katika mzunguko wa Tano kuanzia Aprili 21,” alisema Ndimbo.

JKT Queens inaongoza ikiwa na pointi 12 baada ya kucheza michezo minne na kushinda yote, huku Simba Queens ikishika nafasi ya sita ikiwa na pointi tatu baada ya kucheza michezo minne na kufungwa mitatu.

Kigoma Sisters inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi tisa itaikaribisha Baobab ya Dodoma kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Baobab inashika nafasi ya tano ikiwa na pointi tano baada ya kucheza michezo minne, ikishinda mmoja, sare mbili na kufungwa mmoja.

Mabingwa watetezi, Mlandizi Queens watakuwa ugenini kucheza na Panama kwenye Uwanja wa Samora Iringa. Mlandizi ina pointi sita katika michezo minne iliyocheza na Panama,  inashika nafasi ya saba ikiwa na pointi mbili katika michezo minne iliyocheza.

Alliance Girls inayoshika nafasi ya tatu ikiwa na pointi saba, itakuwa ugenini kucheza na Evergreen, ambayo inaburuza mkia ikiwa na pinti moja kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam

Wachezaji wa Cameroon Wajilipua Madola Australia


GOLD COAST, Australia
WACHEZAJI nane wa timu ya Cameroon inayoshiriki Michezo ya 21 ya Jumuya ya Madola inayoendelea hapa, wametoweka katika makazi yao, viongozi wa timu wamesema.

Msemaji wa timu hiyo Simon Molombe viongozi walibaini kutokuwepo kwa wachezaji hao na wameripoti tukio hilo kwa polisi ya Australia.

Wachezaji hao watatu ni wa kunyanyua vitu vizito na mabondia watano, ambao kwa mara ya mwisho walionekana Jumatatu na Jumanne.

Cameroon imesema kuwa kundi la wachezaji hao lilikuwa na viza halali ya Australia hadi Mei 15 mwaka huu.

Viongozi wa timu hiyo waliwataja wachezaji hao waliopotea kuwa ni wanyanyua vitu vizito Olivier Matam Matam, Arcangeline Fouodji Sonkbou na Petit Minkoumba, wakati mabondia ni Christian Ndzie Tsoye, Simplice Fotsala, Arsene Fokou, Ulrich Yombo na Christelle Ndiang.
"Mamlaka imesikitishwa sana na kitendo cha wachezaji hao waliotoweka, wengine wakiwa hata bado hawajaanza kushindana, “alisema Molombe.

"Tunatarajia watarudi kijijini na kurudi nyumbani na wenzao.”
Serikali ya Australia imewaonya wachezaji dhidi ya kukaa ndhini humo baada ya kumalizika kwa viza zao.

Shirikisho la Jumuiya ya Madola limesema kuwa watafuatilia hali hiyo lakini walisema kuwa wachezaji wana “haki ya kusafiri huru” kwa kuwa wana viza zao.

Mwaka 2012, wachezaji saba wa Cameroon walitoweka wakati wakiwa jijini London walipokwenda na timu yao kushiriki Michezo ya Olimpiki.

Klopp Awasifia Liverpool kwa Kuifunga Tena City


MANCHESTER, Liverpool
KOCHA wa Liverpool Jurgen Klopp ameimwagia sifa timu yake baada ya kupenya na kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya baada ya kuifunga tena Manchester City kwa mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Etuhad.

Kwa matokeo hayo, Liverpool imesonga mbele kwa ushindi wa jumlaya mabao 5-1, kufuatia ushindi wa timu hiyo katika mchezo wao wa kwanza wa mabao 3-0.

"Tumefunga mabao matano dhidi ya Man City na tumeruhusu kufungwa bao moja tu. Kwa kweli idadi kama hii ya mabao haiwezekani kirahisi, “alisema kocha huyo Mjerumani.

"Vijana walipata soluhisho katika kipindi cha pili. Tayari katika kipindi cha kwanza ulikuwa na nafasi mbili au tatu hivi, hivyo ilikuwa rahisi kwangu na vijana kuona muendelezo wa mchezo. Tukafanikiwa kupata mabao.”

Bao la mapema la Gabriel Jesus liliwapa matumaini Manchester City kama wanaweza kupindua matokeo ya awali na kuibuka na ushindi mnono, ambao ungewapeleka katika nusu fainali, lakini hilo halikufanikiwa.

Badala yake, bao la Mohamed Salah katika dakika ya 39 liliiweka Liverpool kukontroo mpira kabla Roberto Firmino hajakamilisha na kuiwezesha Liverpool kutinga kwa maraya kwanza nusu fainali katika kipindi cha muongo mmoja.

Liverpool kwa mara ya mwisho ilicheza fainali ya Ligi ya Mabigwa wa Ulaya katika msimu wa mwaka 2007-08 na ni matumainiyake sasa yameongezeka baada ya kutolewa kwaBarcelona.

Vigogo hao wa Hispania walitolewa baada ya kufungwa 3-0 na AS Roma, huku Roma ambayo ni timu ya zamani ya Salah imesonga mbele kwa bao la ugenini kufuatia sare ya jumla ya mabao 4-4.

Klopp alisema kutolewa kwa Barcelona: "Kumeinua ari kwa timu zilizobaki.
"Sio kuidharau AS Roma. Walimpoteza Salah na sasa wako katika nusu fainali. Hicho ni kitu kingine.

"Mashindano haya yametenda haki na nilitarajia fainali ya kawaida kabisa kati ya Manchester City dhidi ya Barcelona, na sasa wote wametolewa.

"Lakini sasa kutakuwa na timu mbili zenye nguvu pamoja na kuongeza AS Roma na sisi. Tutaona nini kitatokea lakini na hicho sio kitu cha mimi kufikiria.”

Kocha wa Man City, Pep Guardiola aliwataka wachezaji wake kurejea kiakili katika hali ya kawaida baada ya kuwa na wiki mbaya ya msimu baadaya kutolewa kwa mara ya tatu mfululizo.

Man City ilipata pigo jingine mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kushuindwa kutangaza ubingwa wa Ligi Kuu baada ya kufungwa na majirani zao wa Manchester United.

City ina pointi 13 kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya England na kilichobaki ni muda tu kabla timu hiyo haijavikwa taji la England.

Guardiola anataka wachezaji wake kufanya kweli katika mchezo ujao wa Ligi Kuu dhidi ya Tottenham utakaofanyika Wembley Jumamosi ili kutangaza ubingwa endapo watashinda.

"Sasa tunatakiwa kwenda Tottenham tukiwa tumebadilika kifikra, “alisema kocha huyo Mhispania.

"Kipindi cha kwanza tulifanya kila kitu, lakini cha pili tulichemsha.”
Guardiola alisema City waliathirika pia na maamuzi mabovu walipocheza dhidi ya Liverpool.

Leroy Sane alifunga na lingefanya matokeo kuwa 2-0 kama sio mwamuzi kulikataa bao hilo, ambapo Guardiola alililalamikia hadi kutolewa uwanjani.

AS Roma Yaifungisha Virago Barcelona Ulaya


ROME, Italia
HAKUNA aliyetarajia Barcelona inaweza kutolewa na AS Roma katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya baada ya vinara hao wa La Liga kuwa mbele kwa mabao 4-1 baada ya kushinda katika mchezo wa kwanza.

Hata hivyo, Barcelona imefungishwa virago baada ya kupokea kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Roma katika mchezo ambao wenyeji ndio walikuwa wenyeji. Roma imesonga mbele kwa faida ya bao la ugenini.

Kiungo wa Barca Andres Iniesta alikuwa hataki kukubali kama timu yake imepokea kichapo hicho, ambacho kimeitoa katika mbio za kuwania taji la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

Wakati Iniesta akishindwa kuamini kilichotokea kwa timu yake, mchezaji mwenzake wa timu hiyo, Sergio Busquets amekiita kipigo hicho kuwa ni kibaya zaidi katika historia yake ya soka.

Awali, safari ya Barca kucheza nusu fainali ilionekana kuiva wakati timu hiyo ilipouanza mchezo huku ikiwa na faida ya mabao 4-1, lakini walionesha kiwango kibovu kabisa msimu huu, katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Olimpiki.

Baracelona imetupwa nje kwa mabao ya AS Roma yaliyofungwa na Edin Dzeko, Daniele De Rossi kwa penalti na na lile la kichwa lililopachikwa na Kostas Manolas header.

"Inauma kwasababu hakuna mtu aliyetarajia kichapo hiki baada ya kuwa na faida ya mabao manne tuliyopata kutoka katika mhezo wa kwanza, lakini hilo ndilo linakufanya kutambua maana ya michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, “alisema.

Kufungwa huko kwa Barcelona kumeshuhudia timu hiyo ikitolewa katika hatua ya robo fainali ya mashindano hayo kwa mara ya tatu mfululizo na kukatisha ndoto zao za kushinda mataji matatu msimu mmoja.

"Ni ngumu kukubali kutolewa huku kwasababu tulikuwa na matumaini kibao msimu huu na kwa mara nyingine tena (Ligi ya Mabingwa) imetuacha solemba, “aliongeza kiungo huyo.

"Inasikitisha sana baada ya kuwa na msimu mzuri. Sasa tumepata pigo.”

Nahodha huyo wa Barca alibainisha kuwa huenda mwishoni mwa msimu huu akaondoka katika klabuhiyo aliyoitumikia kwa muda mrefu na kwenda China kucheza soka, ambako ataufurahisha moyo wake.

"Ni usiku mzito, huzuni na tunatakiwa kuomba radhi kwa mashabiki wetu kwa jisi tulivyoangua, “alisema.

"Hli ni pigo kubwa ambalo nimewahi kulipa katika kipindi chote nilichokuwa Barcelona kwasababu jinsi kilivyotokea.”

Barcelona, ambao ni mabingwa mara tano pia walifungwa 3-0 katika hatua kama hiyo ya robo fainali msimu uliopita walipocheza dhidi ya Juventus.

"Nitakuwa muongo kama nitasema kuwa eti tutatumia kipigo hicho kama somo kwasababu mwaka jana tulitolea kwa njia kama hii hii, “aliongeza Busquets.

"Matokeo yetu Ulaya katika miaka miwili iliyopita yamekuwa mabaya sana, kama tunataka kushinda Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, basi tunatakiwa kubadilika kabisa.”

Yanga Sports Yataka Mashabiki kuwa Watulivu


Na Mwandishi Wetu
KLABU ya Yanga imewataka mashabiki wake kuwa watulivu kufuatia kuondoka kwa Kocha wao George Lwandamina (pichani) baada ya kurudi katika timu yake ya zamani ya Zesco United ya Zambia.

Mwenyekiti wa Kamati ya mashindano Yanga Hussein Nyika alithibitisha jana kuondoka kwa Lwandamina akisema kuwa wataweka wazi taarifa kamili ya sababu ya kutimka kwake baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji kilichotarajiwa kukaa jana jioni.

Kwa mujibu wa gazeti la Lusaka Times, Lwandamina amejiunga na Zesco United baada ya kuondoka katika klabu hiyo mwaka mmoja na nusu uliopita.

 “Ni kweli Kocha ameondoka tunaomba mashabiki wawe watulivu, tunatarajia kukaa kikao cha Kamati ya utendaji jioni baada ya mechi ya Singida United (jana) kisha tutatoa taarifa ya klabu,”alisema.

Mkataba wa kocha huyo Mzambia ulitarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu kwa maana ya mwezi ujao lakini klabu ya Zesco United iliweka taarifa juzi za kumtangaza Kocha huyo kujiunga nao.

Kitendo cha kuondoka kwake ghafla huku timu hiyo ikiwa na mechi muhimu za ligi na kimataifa, kimewaacha mashabiki katika mshangao.

Nyika alisema watazungumza na Lwandamina kujua tatizo lililomkimbiza ghafla akitoa matumaini kwa mashabiki kuwa kocha huyo atarudi.

Lwandamina aliinoa Zesco kati ya mwaka 2014 na 2017  na kujiunga na  Yanga msimu uliopita ambapo aliipa taji la ligi.  Ni mmoja kati ya makocha wenye majina makubwa nchini Zambia kutokana na kujiwekea wasifu mkubwa katika maisha yake ya ukocha nchini humo.

Aliwahi kuwa Kocha wa timu kubwa ya taifa ya Zambia na timu za vijana kwa miaka tofauti.

Monday, 9 April 2018

Ronaldo afunga, Real ikitoka sare na Atletico

MADRID, Hispania
 MSHAMBULIAJI wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo ameifungia timu yake katika sare ya bao 1-1 dhidi ya Atletico Madrid katika mchezo wa Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’ uliochezwa juzi kwenye uwanja wa nyumbani, akifunga katika mchezo wa 10 mfululizo.

Lakini Antoine Griezmann alisawazisha baadaye na kuendelea kubaki katika nafasi ya pili na kuwaacha Madrid inayowafuata kwa tofauti ya pointi nne.

Sare hiyo inaendelea kuwapa nafasi vinara wa La Liga Barcelona ya kushinda taji baada ya kumuacha Atletico kwa tofauti ya pointi 11, huku Madrid ikishuka hadi nafasi ya nne na Valencia ikipanda juu baada ya kushinda 1-0 dhidi ya Espanyola.

Barcelona inaongoza kwa pointi 79 baada ya kuichapa Leganes 3-1 Jumamosi, ikifuatiwa na Atletico yenye pointi 68, Valencia 65 na Real 64 baada ya kila mmoja kucheza michezo 31. Barca inaweza kuchukua taji kama itashinda michezo minne kati ya saba ijayo.

“Siwezi kuwa na furaha kwa sare kwa sababu tulihitaji ushindi,” alisema Kocha wa Atletico, Diego Simeone.

“Walianza kucheza vizuri, tulipambana kucheza kwa umoja lakini kipindi cha pili tulishambulia zaidi na kutengeneza nafasi, walitufunga na tukafanikiwa kurudisha haraka, tunaondoka tukijivunia kwa kidogo tulichopata,” alisema.

Kocha wa Madrid, Zinedine Zidane alisema “Nina furaha na jinsi tulivyocheza ingawa tulistahili zaidi, ni aibu tulishindwa kushinda kwa sababu tulitengeneza nafasi nyingi lakini pia, tungepoteza mchezo.”

Kocha Azam FC Akata Tamaa ya Ubingwa Bara


Na Mwandishi Wetu
SARE ya bila kufungana dhidi ya Mbeya City imemkatisha tamaa kocha msaidizi wa Azam FC,  Idd Nasoro ‘Cheche’ na kusema nivyema wakajipanga upya kwa ajili ya msimu ujao.

Sare hiyo imeifanya Azam kubaki nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu wakiwa na pointi zao 43, katika michezo 23, huku Simba na Yanga zikichuana kwenye mbio za ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu.

Akizungumza na gazeti hili, Cheche, alisema sare ya juzi dhidi ya Mbeya City imevuruga kabisa malengo yao ya ubingwa na kwa mtazamo wake nivyema wakajipanga upya kwa kusajili wachezaji wenye uzoefu ambao wataweza kutimiza malengo ya timu.

“Sisemi kwamba wachezaji waliopo hawana uwezo bali tunahitaji kuongeza baadhi kutoka ndani na nje ili kuimarisha zaidi kikosi chetu kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma,” alisema Cheche.

Kocha huyo alisema kitu kikubwa ambacho kinawakwamisha msimu huu ni baadhi ya wachezaji wao wakutumainiwa kuwa majeruhi huku waliobaki wakiwa hawana zoefu wa kutosha kwa ajili ya mapambano ya ndani ya uwanja.

Azam imebakiwa na michezo saba kabla ya kumaliza msimu huu na matarajio yao hivi sasa ni kuhakikisha wanamaliza kwa heshima ligi hiyo kama ilivyokuwa misimu minne nyuma.