Na Mwandishi Wetu
BARAZA la Michezo la
Taifa (BMT) limetoa wiki tatu kwa klabu ya Yanga kuhakikisha wanachama wake
wanajisajili upya katika matawi yote nchini kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu, huku
ikilipa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) mwezi mmoja kutangaza tarehe ya Uchaguzi Mkuu wa klabu
hiyo.
Hivi karibuni Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dr Harrison Mwakyembe alikutana na viongozi
wa Yanga pamoja na wazee wa klabu hiyo kusikiliza kero zao.
Kaimu Katibu Mkuu wa wa
BMT, Alex Mkeyenge alisema jana kuwa wamefanya hivyo baada ya wanachama wa
Yanga kuwasilisha malalamiko yao kwa
Waziri, na baada ya kuwahoji wakafikia muafaka na ndipo suala hilo likarejeshwa
kwa BMT.
Mkyenge alisema Yanga ni
timu ya wananchi na inahitaji kutoa burudani kwa wanachana na wapenzi wake
pamoja na kutoa ajira kwa wachezaji iliowasajili, hivyo migogoro haina nafasi
kwa sababu inaua soka nchini.
Na ndio maana BMT
imeamua kutoa agizo kwa viongozi wa Yanga pamoja na TFF ili litekelezwe kwa wakati
huo.
"Tunaomba wale
kwenye kadi za Benki ya Posta na CRDB wote watumie muda waliopewa kwenda kwenye
matawi yao kwa ajili ya kujisajili," alisema kiongozi huyo wa BMT.
Kikosi cha Yanga. |
Akizungumzia tarehe ya uchaguzi alisema wameiagiza TFF
kupitia kamati yake ndani ya mwezi mmoja watangaze tarehe ya kufanyika kwa Uchaguzi
Mkuu wa Yanga.
Alisema anaamini TFF
itafanya kazi kwa weledi ili kuhakikisha wananusuru migogoro midogo, ambayo
inarudisha nyuma hadhi ya klabu hiyo, ikiwemo kushusha ari za wachezaji wake.
"Tunataka kuona
Yanga kama ilivyokuwa mwanzo,sio malumbano tena wanachama wameshatoa.madukuduku
yao wakitaka uchaguzi ufanyike, “alisema Mkeyenge.
Kwa upande wa Makamu wa
Rais wa TFF Athuman Nyamlani alisema Kamati ya TFF iko kamili kwa ajili ya
kusimamia uchaguzi huo, huku ikisisitiza ndani ya muda huo tarehe ya uchaguzi
itatangazwa.
"Kila kitu safari
hii kitakwenda sawa kwa sababu kila mtu Yanga anataka uchaguzi na hili sio
suala la mtu mmoja, “alisema Nyamlani.
Alisema muda waliopewa
inatosha sana kufanya walichoagizwa kwa sababu uchaguzi huo umeahirishwa mara
nyingi kutokana na wanachama mwenyewe kutoelewana.
Alifafanua zaidi ya
kuwa, Yanga inahitaji kuwaburudisha wanachama na mashabiki wake, hivyo anapoendekeza
migogoro,wanashindwa hata kusajili nakuwatunza vizuri wachezaji.
No comments:
Post a Comment