Friday 23 November 2018

Serikali yakifikiria kupanua Kiwanja cha Ndege Bukoba


1.   Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Isack Kamwelwe akipita eneo la ukaguzi wa abiria na mizigo la Kiwanja cha Ndege cha Bukoba, leo alipofanyua ziara ya kikazi. Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushari (MAB) ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mhandisi Prof. Ninatubu Lema.

 Na Mwandishi Wetu, Bukoba
SERIKALI inafikiria kufanya upanuzi na urefushaji wa barabara ya kutua na kuruka kwa ndege ya Kiwanja cha Ndege cha Bukoba licha ya changamoto zilizopo, ili kiruhusu kutua kwa ndege kubwa zaidi.

Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe katika ziara yake ya kikazi ya kukagua miundombinu ya taasisi zilizopo chini ya Wizara yake, ambapo kiwanja hicho kipo chini ya Mamlala ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).

Mhe. Kamwelwe alisema bado Kiwanja hicho kinakabiliwa na changamoto endapo kitaongezwa lazima baadhi ya nyumba za Ibada, hospitali na nyumba za kuishi watu zitalazimika kuondolewa ili kupisha upanuzi huo.

“Ukiangalia upande mmoja una makazi ya watu na upande mwingine ni Ziwa Viktoria na mwingine kuna Mlima, hivyo bado tunafanyia kazi hizi changamoto na endapo zitatatuliwa, basi miundombinu hii itaboreshwa zaidi kwa kuwa tayari lipo jengo zuri na lenye mfumo mzuri wa maji taka na mifumo mingine mbalimbali,” amesema Mhe. Kamwelwe.


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Isack Kamwelwe (kulia) leo akimsikiliza Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Bukoba, Bi. Doris Uhagile (katikati), akimpa maelezo mbalimbali wakati alipofanya ziara ya kikazi kwenye kiwanja hicho. Mwenye tai nyekundu ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela na kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Mhandisi Richard Ruyangu.

Hata hivyo, alisema Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) litaongeza safari zake mara mbili kwa siku wenye Kiwanja cha ndege cha Bukoba, kutokana na kuwa na abiria wengi kwa sasa.

Mhe. Kamwelwe alisema kwa sasa ndege hiyo aina ya Bombardier Q400 inakuja mara moja kwa siku kwa kila siku kuanzia Jumatatu hadi Jumapili.

“Kwa sasa abiria wameongezeka zaidi nimeelezwa kuwa kwa mwaka ilikuwa kiwanja kinaweza kuhudumia abiria 28,000 pekee, lakini sasa ni zaidi ya 45,000 kwa mwaka, hivyo inaonesha ni kiasi gani wanavyoongezeka na ndio maana ninasema kutakuwa na uwezekano wa kuongeza safari za ATCL na iwe mara mbili kwa siku balada ya sasa mara moja,” alisema Mhe. Kamwelwe.


1.   Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Bukoba, Bi. Doris Uhagile (katikati) leo akiwa eneo la ukaguzi wa tiketi za abiria ambapo alitoa maelezo ya namna mashirika ya ndege yavyohudumia abiria kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Isack Kamwelwe. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Richard Mayongela, akifuatiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri (MAB) ya TAA, Mhandisi Prof. Ninatubu Lema.

Alisema serikali tayari imenunua ndege mbili aina ya Airbus 220 zenye uwezo wa kubeba abiria 132 zitakazowasili nchini Desemba 18 na 23, 2018 tayari kwa safari za maeneo mbalimbali.

Ndege hizi zinaweza kutua kwenye viwanja vya ndege vya daraja la 4C, ambapo kwa sasa ni Songwe na Mwanza, na baada ya ukarabati kukamilika kwenye kiwanja cha Mtwara na kuboreshwa kwa Kigoma, pia itaweza kutua; hali kadhalika pia itatua kwenye viwanja vya Kimataifa vya Julius Nyerere (JNIA) na Kilimanjaro (KIA), ambavyo ni daraja la 4E.

Kiwanja cha Ndege cha Bukoba kinajengo la kisasa la abiria, ambalo lilizinduliwa Desemba 2017 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Mhe. John Pombe Magufuli, ambapo mbali na ATCL ndege nyingine zenye ratiba maalum zinazotua ni pamoja na Precision, wakati nyingine zinakuwa zimekodiwa bila kuwa na ratiba maalum kama Auric.


No comments:

Post a Comment