Na Mwandishi Wetu
BARAZA la Michezo la Taifa (BMT), limelitaka Shirikisho
la Riadha Tanzania (RT) kutumia mashindano ya taifa ya riadha ya wanawake
kuchagua timu ya wanariadha watakaoenda kushiriki mashindano ya kufuzu kwa
Michezo ya Olimpiki 2020 itakayofanyika Tokyo, Japan.
Mashindano hayo ya pili ya taifa ya wanawake, ambayo
yanajulikana kama JICA Ladies First, yatafanyika kwenye Uwanja Taifa Jijini Dar
es Salaam kwa siku mbili kuanzia Jumamosi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Katibu
wa BMT Alex Nkenyenge alisema, jumla ya wanariadha 155 wanatarajia kujitokeza
kushiriki katika mashindano hayo.
Nkenyenge alisema kuwa mashindano hayo ni muhimu kwa
sababu yatawasaidia RT kugundua vipaji vya riadha, ambavyo watavitumia katika
mashindano mbalimbali ya kufuzu kwa michezo ya Olimpiki.
"Hii ni nafasi muhimu kwa RT kuchagua wanariadha wenye viwango
kwasababu mwakani kuna mashindano ya kufuzu kushiriki michezo ya
Olimpiki," alisema Nkenyenge.
Alisema kutokana na hilo, Kamati ya RT iwe makini
kwenye mashindano hayo ili kupata wanariadha watakaofanya vizuri na kufikia
viwango, ambavyo vitawasaidia kwenda kushinda katika mashindano mbalimbali ya kufuzu
kwa Olimpiki yanayotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Riadha
(IAA).
Alisema mpaka sasa mikoa yote imethibitisha kushiriki
katika mashindano hayo ambayo mwaka jana ilishirikisha wanariadha wanawake 123
kutoka mikoa 26 ya Bara na Visiwani.
Naye Mwakilishi Mkuu wa JICA, Toshio Nagase alisema
mashindano haya ni muhimu kwa Tanzania hususani wanariadha wakike kwa sababu
yanatoa nafasi ya wao kwenda Japan kushiriki mbio mbalimbali nchini humo.
Mbali na hilo alisema ushiriki wa mashindano hayo, unawasaidia wanariadha kuinua vipaji vyao kutokana na
kwenda nje ya nchi katika.mashindano ya kirafiki ambayo ni moja ya mazoezi ya
kujiandaa na michuano mbalimbali ya kimataifa, yakiwemo yale ya kufuzu Olimpiki
ya 2020.
"Nimefurahia kuona mwitikio wa mikoa ni mkubwa,
tutaendelea kushirikiana ili kuinua vipaji vya wanariadha wa Tanzania,"
alisema Nagase.
Kwa upande wa Katibu msaidizi wa RT, Omben Zavalla
alisema wanakila sababu ya kuwashukuru JICA kwa sababu wamefanya jambo kubwa
kwa RT pamoja na maendeleo ya riadha kwa ujumla.
"Huu ni ushirikiano mzuri sana kwasababu unasaidia
kuibua vipaji vya wanariadha mbalimbali kutoka mikoani," alisema Zavalla.
Alisema wanariadha waliochaguliwa kuwakilisha mikoa
yao washindani kwa bidii ili kuonesha uwezo wao.
Mashindano hayo yanatarajia kuanza kesho huku
wanariadha 155 wanatarajia kushiriki,ambapo kutakuwa na mbio za mita 100,200,
400, 800, 1,500 na meta 10,000 sambamba na kurusha mkuki.
Jica ndio wadhamini wa mashindano hayo, ambayo
yaliadhishwa baada ya mwanariadha wa zamani kwa kushirikiana na RT kuiomba Jica
idhamini ili Tanzania iwe na wanariadha wengi katika Olimpiki ya 2020.
No comments:
Post a Comment