UBORA
wa majengo ya shule mpya ya Msingi ya Tumaini Bukoba yenye miundombinu ya
kisasa pamoja na maji na umeme, yataongeza ufaulu wa wanafunzi wa darasa la
Saba, imeelezwa.
Kauli
hiyo, imetolewa jana na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe Isack
Kamwelwe alipokuwa akiikabidhi shule hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia
Jenerali Marco Gaguti kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe, John Pombe Magufuli.
Mhe.
Kamwelwe amesema majengo hayo ya kisasa yaliyojengwa na Mamlaka ya Viwanja vya
Ndege Tanzania (TAA), ni kielelezo cha kuwafanya wanafunzi wasome kwa bidii kutokana
na kuwa na miundombinu rafiki.
1.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhe. Isack Kamwelwe akinyanyua juu funguo za moja ya madarasa 24
ya Shule ya Msingi Tumaini ya Bukoba, kabla ya kuikabidhi kwa Mkuu wa Mkoa wa
Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli.
“Hii
shule inamajengo mazuri sana natamani nirudi katika umri wa mtoto ili nisome
hapa, maana madarasa mazuri, nasikia pia kuna umeme na maji ya kutosha, basi
ninaimani kubwa ubora huu utakuwa chachu ya kuongeza juhudi katika masomo na
mtafaulu zaidi,” amesema.
Pia
amewapongeza TAA kwa kuhakikisha wanawajali wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa
kujenga madarasa matatu kwa ajili ya kufundishiwa na chumba kimoja
kinachotumika na walemavu hao kupumzika nyakati za mchana.
Naye
Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Richard Mayongela amesema Mamlaka ilijenga shule
hii mpya kwa sababu shule ya zamani ilikuwa imejengwa eneo hatarishi ikiwa na
mita chache kutoka kwenye barabara ya kutua na kuruka kwa ndege na pia kelele
na mingurumo ya ndege sio salama kwa wanafunzi na walimu wao.
Bw.
Mayongela amesema ujenzi wa shule hiyo imejumuisha jumla ya madarasa 24 kati ya
hayo matatu ni ya watoto wenye uhitaji maalum, jengo la utawala, chumba cha
kupumzikia watoto wenye uhitaji maalumu, uzio na vyoo.
“Kiusalama
ilikuwa lazima shule ya Tumaini iondoke pale kiwanjani na kutafutiwa sehemu
nyingine, kwani wakati ndege inatua inakuwa na makelele na kutua kwake inakuwa
karibu na paa la shule inaleta shida,” amesema Bw. Mayongela.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Ushauri (MAB) ya TAA, Mhandisi Prof. Ninatubu Lema amewataka watoto
wasome kwa bidii ili waweze kufika Chuo Kikuu kusomea uhandisi ambao
wanahitajika kwa wingi.
“Mimi
ni mwalimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, natamani sana baada ya miaka 15
nije kuwafundisha uhandisi kule Chuo Kikuu, taifa linauhitaji sana wa
Wahandisi, hivyo msome kwa bidii maana hata shule hii mliyokabidhiwa ni nzuri
na inawavutia kusoma, nawapongeza na wazazi waliowaleta shule kusoma,” amesema
Prof. Lema.
Mkuu
wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti ameishukuru serikali kwa
kuwezesha ujenzi wa shule hii, ambayo imejengwa kwa kuhudumia wanafunzi wazima
na wenye mahitaji maalum, ambapo kwa mkoa mzima hii ndio ya kipekee.
“Tunakuomba
ufikishe salaam zetu za shukrani kwa Mhe. Rais John Pombe Magufuli kwa shule
hii, ambayo itainua kiwango cha elimu cha mkoa wetu, mwaka huu darasa la Saba
tumeshika nafasi ya Tano Kitaifa, ninaimani mwakani (2019) tutakuwa juu zaidi,”
amesema.
Kwa
upande wake Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bi.Augustina Daniel amesema ufaulu
umeongezeka mara dufu na wazazi wamekuwa na mwamko wa kuandikisha wanafunzi
wengi wa darasa la kwanza.
“Tumekuwa
tukipata idadi kubwa ya wanafunzi wanaokuja kujiunga na darasa la kwanza,
ambapo mwaka 2018 tumeandikisha 246 wa darasa la kwanza, na hata
ufaulu wa darasa la saba umeongezeka tumefaulisha kwa asilimia 97.7,” amesema
Bi. Daniel.
Shule
hiyo yenye wanafunzi 1232 kati ya hao 45 ni wenye uhitaji maalum, na imejengwa na Kampuni ya Ujenzi ya CMG Construction Co Ltd.
No comments:
Post a Comment