Monday, 27 November 2017

Uhamiaji yaanza kwa kishindo netiboli Muungano

Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Uhamiaji imeanza vizuri kutetea taji lake la netiboli la Muungano baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 40-39 dhidi ya Mafunzo katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Gymkhana mjini Zanzibar.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta) Judithi Ilunda, mchezo huo ulikuwa wa vuta nikuvute na hadi robo ya kwanza inamalizika, timu hizo zilikuwa sare ya 11-11.

Katika robo ya pili, Uhamiaji walikuwa mbele kwa mabao 21-19 na ile ya tatu washindi waliendelea kuwa mbele kwa mabao 36-28.

Ligi hiyo inachezwa kwa makundi,ambapo Kundi A lina timu za Mafunzo, Uhamiaji, Jeshi Stars, Zima Moto na Duma kuhu Kundi B likiundwa na JKU, JKT Mbweni, Polisi Arusha, KVZ na Afya.

Katibu Mkuu wa Chaneta, Judith Ilunda
Aidha, Ilunda alisema kuwa timu za Polisi Morogoro na Madini ya Arusha zimeshindwa kushiriki na kuifanya Tanzania Bara kuwa na timu nne katika mashindano hayo wakati Zanzibar wana timu sita.

Alisema kuwa pamoja na kutotoa taarifaya kutoshiriki lakinihadi sasa timu hizo zilikuwa hazijawasilisha barua zao za sababu ya kushindwa kuwepo katika ligi hiyo ya Muungano.


Ilunda alisema kuwa wanatarajia mashindano hayo yatakuwa na msisimko wa aina yake na kupatikana kihalali mshindi wake.

Ligi hiyo inaendelea asubuhi hii leo Jumanne kwa Zimamoto kucheza dhidi ya Duma, Polisi Arusha itapepetana na mabingwa wa Tanzania Bara JKT Mbweni huku KVA watapelekana puta na Afya na Jeshi Stars watafunga pazia leo kwa kucheza na mabingwa wa Zanzibar Mafunzo.

No comments:

Post a Comment