Tuesday, 14 November 2017
Maofisa AAKIA Wafurahishwa Ulinzi JNIA
Na Mwandishi Wetu
MAOFISA kutoka
Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume cha Zanzibar (AAKIA),
wamefurahishwa na namna ulinzi na usalama wa abiria na mali zao unavyofanywa
kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), imeelezwa.
Maofisa hao kutoka
Idara mbalimbali walitoa kauli hiyo jana katika ziara ya siku moja ya mafunzo
JNIA, ambapo walitembelea maeneo mbalimbali na kupata maelezo ya kina kutoka
kwa maofisa husika.
Mkuu wa msafara wa
maofisa hao, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi na Usalama cha AAKIA, Bw.
Shaaban Kombo alisema pamoja na kupata mambo mengi ya msingi ya uendeshaji wa
viwanja vya ndege, pia wamejifunza namna abiria na mizigo anavyokaguliwa kwa
kutumia mitambo ya kisasa kabla ya kupanda ndege.
Bw. Kombo alisema
JNIA imekuwa darasa tosha, ambapo pia katika upande wa utoaji wa vitambulisho
wamejifunza namna utoaji wa vitambulisho unavyofanyika, ambapo AAKIA hutoa
vitambulisho vya kudumu mara utaratibu wa muombaji utakapokamilika, tofauti na
JNIA muombaji anaweza kupewa kitambulisho cha muda na kuendelea kufanyakazi
huku cha kudumu kikiwa katika matengenezo.
“Tumefaidika na
mambo mengi ukiangalia sisi kwetu hii ya vitambulisho ni tofauti kabisa, ila
kwetu kwa kipindi chote mteja anasubiri kitambulisho cha kudumu anakuwa hawezi kuendelea
na kazi zake eneo la kiwanja hadi atakapopata cha kudumu, lakini hapa anakuwa
na cha muda kinachomfanya aendelee na shughuli zake huku cha kudumu kikiwa
katika matengenezo,” alisema Bw. Kombo.
Naye Mkuu wa
kitengpo cha Ulinzi na Usalama cha JNIA, Bw. Lugano Mwansasu alisema ziara ya
maofisa wa AAKIA imewafariji na kuanza ukurasa wa mahusiano katika ushirikiano,
ambapo nao wamejifunza kulingana na maelezo ya uendeshaji wa AAKIA.
Bw. Lugano alitoa
wito kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kuiga mfano huo wa
kupeleka maofisa wake kwenye viwanja mbalimbali vya nje ya nchi kwa ajili ya
kujifunza utendaji kwa lengo la kuboresha huduma za viwanja kwa ujumla. TAA
inasimamia viwanja 58 vilivyopo chini ya serikali.
“Kila siku mambo
ya uendeshaji yanabadilika, basi tunaiomba mamlaka yetu itusaidie na sisi
kwenda kutembelea viwanja vya wenzetu tujifunze huko, zipo changamoto labda
sisi hatujui zinatatuliwaje lakini kwa ziara za mafunzo tunaweza kupata mbinu
kutoka kwa wenzetu,” alisema Bw. Lugano.
Katika hatua
nyingine, Meneja Uendeshaji wa JNIA, Bw. Vedastus Fabian alisema faida ya ziara
ya mafunzo ni kujijengea uwezo na mahusiano mazuri baina ya kiwanja kimoja na
kingine.
Bw.Fabian alisema
ziara hizo zinasaidia katika kutatua matatizo yanayovikumba viwanja vya ndege,
ambapo kwa sasa kumekuwa na masuala ya ugaidi, uvushaji wa dawa za kulevia na
nyara za serikali.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment