Tuesday, 14 November 2017
Italia Yashindwa Kufuzu Kombe la Dunia 2018
ROME, Italia
MABINGWA mara nne
wa dunia Italia wameshindwa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya
kwanza tangu mwaka 1958 baada ya kushindwa katika mchezo wa mchujo dhidi ya
Sweden.
Suluhu dhidi ya
Sweden, haikuisaidia Italia kusonga mbele na badala yake wapinzani wao hao ndio
wamefuzu kucheza fainali hizo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2006 walipofuzu
kwa fainali hizo.
Hiyo ina maana
kuwa timu ya taifa ya Italia inayojulikana kama Azzurri itakosa mashindano hayo
kwa mara ya pili tangu yalipoanzishwa baada ya kushindwa kushiriki wakati wa
ufunguzi wa mashindano hayo mwaka 1930.
Katika mchezo wa
kwanza uliofanyika Sweden wiki iliyopita, Italia walipokea kichapo cha bao 1-0
kabla ya kutoka suluhu katika mchezo huo wa juzi uliofanyika kwenye Uwanja wa
San Siro jijini Milan.
Pamoja na suluhu
hiyo, lakini wenyeji ndio walitawala zaidi mchezo huo kwa asilimia 76, licha ya
kushindwa kuzifumania nyavu.
PIGO KWA KIPA
Mbali na kutolewa,
Italia pia ilipata pigo jingine baada ya kipa wao na baadhi ya wachezaji
wengine kuamua kustaafu baada ya timu yao kushindwa kufuzu kwa fainali za
mwakani zitakazofanyika Urusi.
Nafasi safi ya
Italia kupata bao ilitibuliwa na kipa wa Sweden Robin Olsen alipookoa mpira
uliopigwa na mchezaji aliyetokea benchi Stephan El Shaarawy.
Mshambuliaji Ciro
Immobile alikosa nafasi kibao na juhudi zake katika kipindi cha kwanza
ziliokolewa katika mstari na beki wakati Andreas Granqvist.
Kipa Gianluigi
Buffon alisema alikuwa na majonzi makubwa yeye pamoja na wadau wote wa soka wa
Italia kwa nchi yao kushindwa kufuzu baada ya kufungwa na Sweden.
Buffon, 39,
alisema: "Ni aibu kwa mchezo wangu rasmi wa mwisho kwa kuumaliza kwa
kushindwa kufuzu kwa Kombe la Dunia.
"Lawama
zinagawanywa kwa kila mmoja. Hakuna mtu wa kutupiwa lawama hapa.”
Mchezaji mwenzake
na Buffon wanayecheza pamoja na Juventus Andrea Barzagli na kiungo wa Roma
Daniele de Rossi pia alimaliza kipindi chake cha kuichezea Italia, wakati
Giorgio Chiellini anatarajia kujiunga nao. Wanne hao wamecheza mechi 461
miongoni mwao.
Kipa Buffon
ameichezea timu hiyo mechi 175 katika kipindi cha miaka 20, ambapo alitwaa taji
la Dunia 2006 – na anaamini kuwa bado timu hiyo inaweza kufanya vizuri mbeleni.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment