Friday, 10 November 2017

Chaneta Yaishusha Daraja Timu ya Simiyu

Na Mwandishi Wetu

WAKATI kinyang’anyiro cha netiboli za Ligi Daraja la Pili Taifa kikiendelea kutimua vumbi, timu ya Simiyu kutoka mkoani humo, imeshushwa daraja baada ya kushindwa kushiriki mashidano hayo.

Mashindano hayo ya kuwania kupanda daraja kucheza Ligi Daraja la Kwanza Taifa, yanaendelea kwenye viwanja vya Jakaya Kikwete Youth Park, ambapo timu saba zitapanda na kucheza Ligi Daraja la Kwanza Taifa.

Katibu Mkuu wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta) Judith Ilunda amesema kuwa, timu ya Simiyu itashushwa daraja na kutakiwa kulipa sh 500,000 baada ya kuthibitisha kushiriki, lakini imeshindwa kutokea.

“Jana (juzi) tuliongea na kiongozi mmoja wa Simiyu alisema wako njiani wanakuja katika mashindano, lakini leo (jana) akathibitisha kuwa hawaji tena, watashushwa daraja na kutakiwa kulipa sh 500,000, “anasema Ilunda.

Anasema kuwa mashindano hayo yanaendelea vizuri na timu 11 kutoka mikoa sita Tanzania bara zinachuana kuwania nafasi saba za kupanda daraja.

Katika mechi za jana; timu ya Pamoja Youth iliichakaza Zimamoto kwa kuichapa mabao 55-27 wakati Magereza ya Morogoro iliibuka na ushindi wa magoli 53-28.

Katika mechi za juzi kwenye uwanja huo, Magereza Moro ilitamba kwa kuifunga Chem Chem kwa mabao 49-11, wakati Bandari Dar ikiichapa Sedico kwa mabao 49-30, Coca Cola waliilowesha Zima Moto kwa 43-31.


Hayo ni mashindano ya kwanza kufanyika chini ya uongozi mpya wa Chaneta ulioingia madarakani Septemba 30 mwaka huu mjini Dodoma.


No comments:

Post a Comment