Nyota Kibao Kushiriki Tamasha la Karatu 2017
Na Mwandishi Wetu
NYOTA kibao wa
riadha wanatarajia kushiriki mbio za kilometa 10 na zile za kilometa tano za
wanawake na wanaume zitakazofanyika Desemba 23 mjini Karatu.
Mbio hizo pamoja
na michezo mingine kama ya baiskeli, mpira wa wavu, soka, ngoma na kwaya
zitakuwa ni hitimisho la Tamasha la Michezo la Karatu 2017.
Kwa mujibu wa
mratibu wa tamasha hilo Meta Petro, mbio za mwaka huu zinatarajia kushirikisha
wanariadha kibao nyota kutoka sehemu mbalimbali nchini.
Alisema baadhi ya
wanariadha hao watatoka katika taasisi za kijeshi, huku wengine wakitoka katika
klabu za uraiani na sehemu mbalimbali katika mikoa ya Arusha, Manyara, Singida,
Kilimanjaro na Dar es Salaam.
|
Filbert Bayi |
Tamasha hilo
ambalo linaendeshwa na Filbert Bayi Foundation (FBF) lilianza zaidi ya miaka 10
iliyopita na linafanyika Desemba ya kila
mwaka.
Kwa mujibu wa
Petro, tamasha hilo hasa mchezo wa mbio limekuwa na lengo la kuibua na
kuuendeleza vipaji vya chipukizi ili kuwapata nyota wapya watakaochukua nafasi
ya Bayi aliyewahi kuwa bingwa wa dunia wa mbio za meta 1500.
Mbali na meta
1500, Bayi pia aliwahi kutamba na kushikilia rekodi ya dunia ya mbio za maili
moja na kutwaa medali ya fedha katika Michezo ya Olimpiki iliyofanyika Moscow,
Urusi mwaka 1980.
Bayi ni mwenyeji
wa Karatu mkoani Arusha na aliamua kuanzisha mbio hizo ili kupata vipaji vipya
vitakavyomrithi yeye katika mchezo huo.
|
Meta Petro |
Mbali na mbio za
kilometa 10 na zile za tano, pia kutakuwa na mbio za watoto ambazo zitakuwa za
kilometa 2.5.
No comments:
Post a Comment