Na Mwandishi Wetu
RAIS na Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Gulam
Rashid na Filbert Bayi wamechukua fomu kutetea nafasi zao katika Uchaguzi Mkuu
utakaofanyika Dodoma Desemba 10.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam jana,
zilisema Bayi amechukua na kurudisha fomu.
Viongozi hao wawili ambao jana walitarajia kwenda Qatar kuhudhuria
Mkutano Mkuu wa mwaka wa Kamati za Olimpiki za Taifa (ANOC) utakaofanyika wiki
ijayo Doha, wamelazimika kuchukua kwani watakuwa huko hadi Novemba 17.
Mwisho kwa kuchukua na kurudisha fomu kwa wanaotaka kuwania uongozi
TOC ni Novemba 15 kwani siku hiyo watakuwa hawajarejea nchini.
Akizungumza kwa simu jana, Bayi hakukubali wala kukataa lakini
alisema kuwa jana alikuwa na kazi nyingi ofisini kwake kabla ya kuondoka kwenda
Qatar.
Taarifa zingine zinasema kuwa Mkurugenzi msaidizi wa zamani wa
Kurugenzi ya Michezo katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,
Juliana Yassoda ni miongoni mwa waliochukua fomu za kutaka kuwania ujumbe TOC.
Yassoda ni miongoni mwa wakufunzi wa TOC, ambaye kwa muda mrefu
amekuwa akitoa mafunzo kwa vyama mbalimbali vya michezo nchini.
Wengine ambao tayari wamechukua fomu kutaka kuwania ujumbe ni
pamoja na Muharami Mchume, Irine Mwasanga, Noorelain Sharif, Noel Kihunsi na
Zakia Mrisho anayewania ujumbe wa wale waliowahi kushiriki Michezo ya Olimpiki
(Olympians).
Mkutano huo wa Qatar pamoja na mambo mengine, utasikiliza sera za
majiji yanayotaka kuandaa Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2024 na ile ya walemavu
ya Paralimpiki.
Zaidi ya wajumbe 1,000 kutoka mataifa 206 wanatarajia kuhudhuria mkutano
huo wa mwaka.
No comments:
Post a Comment