Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Riadha Tanzania (RT), Meta Petro (kulia) na Katibu Mkuu wa Kamati ya Utendaji ya TOC,, ambaye pia mjumbe wa RT, Filbert Bayi wakipiga kura leo kwenye Uwanja wa Taifa. |
Na Mwandishi Wetu
UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania umefanyika leo kukishuhudia mwanariadha wa zamani, Wilhelm Gidabuday akirithi mikoba ya Katibu
Mkuu wa zamani Suleiman Nyambui aliyeko nchini Brunei.
Nyambui kwa sasa ndiye kocha mkuu wa timu ya taifa ya riadha ya Brunei.
Aidha katika uchaguzi huo Anthony Mtaka aliitetea nafasi yake ya
Urais wa shirikisho hilo kwa mara nyingine tena kwa kura 73 kati ya kura 74.
Gidabuday alipata kura 38 akiwapita Michael Washa (24) na Gidamis
Shahanga (11) huku kura moja ikiharibika katika nafasi hiyo.
Katika nafasi nyingine, William Kalaghe alichukua nafasi ya Makamu
wa Rais Utawala kwa kura 59 dhidi ya 15 zilizokwenda kwa Zainab Mbilo huku Dk.
Ahmed Ndee alichukua nafasi ya Makamu wa Rais Ufundi kwa kura 74 dhidi ya kura
nne za hapana.
Ombeni Zavalla aliyekuwa akikaimu Katibu Mkuu wa RT katika
uchaguzi huo alipita bila kupingwa katika nafasi ya Katibu Mkuu Msaidizi kwa
kura zote 74 na Gabriel Liginyani akipata nafasi ya Mweka Hazina wa shirikisho hilo kwa kura 69 kati ya
74.
Wengine waliopata nafasi ya Ujumbe wa RT ni Lwiza John, Meta
Petro, Robert Kalyahe, Dk. Nassoro Matuzya, Rehema Killo, Zakaria Barie, Mwinga
Mwanjala, Tullo Chambo, Christian Matembo na Yohana Misese.
Katibu Mkuu wa BMT afunguka
Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) Mohamed Kiganja
aliweka bayana “RT ndio chama pekee cha michezo
nchini kinachoongozwa na Mkuu wa Mkoa, kwetu sisi (BMT) ni utajiri, hii
ni dalili nzuri…hivyo ukiboronga unapoteza nafasi zote mbili,” na kuongeza
“Migogoro
kwenye vyama inakimbiza wawekezaji na wafadhili, sio vema pindi mambo ya ndani
yanapokuwa hayaendi sawasawa kukimbilia kwenye vyombo vya habari,” alisema Kiganja.
Gidabuday asutwa, ajitetea
Mjumbe wa BMT na Mwenyekiti wa Kamati ya Rufaa na Usuluhishi ya
baraza hilo Jamal Lwambo alimsuta Gidabuday kwa kauli zake ngumu alizowahi
kuzitoa awali.
“Katibu
Mkuu mpya uliwahi kusema kwa RT wasiporudi na medali ungefanya nini
...sasa kama ulivyokuwa ukiisuta RT ukiwa bado hujaikamata nafasi hiyo watu
wamekurudisha kundini wana matumaini makubwa kwako,” na kuongeza
“Kipindi
mlichopata ni kifupi sana..hatutarajii kuona migogoro bali tunarajia kuona timu
inatengenezwa vizuri ili kuleta heshima ya Tanzania,” alisema Lwambo.
Kwa upande wake Gidabuday alisema, “Challenge zangu kwa RT nilipokuwa nje ya shirikisho ndizo
zilizonifanya nigombee nafasi hii lakini nawashukuru sana RT kwani
hawakunijengea chuki kwa kuwakosoa bali walinitazama kwa upande wa
uzuri.”
Aliongeza, “Kwa umbo mimi ni mwembamba natoa ahadi tena kama ukiniona mwakani
wakati kama huu nina kitambi basi uje uniulize kulikoni,” alisema Gidabuday.
Tullo Chambo atetea nafasi yake
Afisa Habari wa RT na mjumbe wa shirikisho hilo Tullo Chambo
alisema, “
Kwa kweli kinyang’anyiro mwaka huu kilikuwa kigumu ukilinganisha na msimu uliopita
wakati tukiingia, lakini naamini uongozi huu kwa mara nyingine utajitahidi
kufanya makubwa kuinua riadha.”
No comments:
Post a Comment