Thursday, 22 September 2016

Vigogo wa mpira wa magongo wa dunia na wa afrika watembelea ofisi za Kamati ya Olimpiki Tanzania




Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa magongo Tanzania (THA), Abraham Sykes (katikati) akimtambulisha Rais wa Shirikisho la Kimataifa la mchezo huo, Leandro Negre kwa Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi wakati kiongozi huyo na yule wa Afrika, Seif Ahmed walipotembelea ofisi za TOC mapema leo Alhamisi.

Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Magongo (FIH), Leandro Negre na Rais wa Afrika wa mchezo huo, Seif Ahmed leo walitembelea ofisi za Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC).

Katika ziara hiyo wawili hao waliongozana na viongozi wa mchezo huo wa kitaifa (THA), Abraham Sykes ambaye ni mwenyeki na Kaushik Doshi (Katibu Mkuu) na kufanya mazungumzo mafupi na Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi.
Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi akimkaribisha rais wa Chama cha Hockey cha Afrika, Seif Ahmed leo.
Ujumbe huo ukiongozwa na rais wa FIH, Leandro Negre pamoja na rais wa mchezo huo wa Afrika, Seif Ahmed wa Misri ulijadili mambo mbalimbali ya michezo na jinsi ya kuisaidia Tanzania katika mchezo huo.

Negre aliitaka TOC kuisaidia THA kupata udhamini wa mafunzo kutoka Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) kupitia kitengo chake cha misaada cha Olympic Solidarity ili kupata mafunzo zaidi kwa walimu wa mchezo huo hapa nchini.
 
Mchezo wa hockey kwa mara ya kwanza ulichezwa katika Olimpiki mwaka 1908 iliyofanyika jijini London, ambapo awali ulichezwa katika viwanja vyenye majani.

Katika miaka ya 1970 walibadilisha na mchezo huo kuanza kuchezwa katika kwenye uwanja wa bandia na kuufanya kuwa wa haraka zaidi ya huko nyuma ulipokuwa ukichezwa katika viwanja vya majani.
 
Uongozi huo wa FIH juzi ulikutana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye na kuahidi kuijengea Tanzania uwanja wa kisasa wa mchezo huo.

No comments:

Post a Comment