Thursday, 22 September 2016

TAMASHA LA SANAA TANZANIA KUFANYIKA JUMAMOSI SEPTEMBA 24 KIJIJI CHA MAKUMBUSHO DAR ES SALAAM



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAMASHA LA SANAA (24 SEPTEMBA 2016)
UTANGULIZI
Siku ya msanii ni mradi uliobuniwa a Baraza la Sanaa la Taifa ukiwa a lengo la KUTAMBUA, KUHAMASISHA na KUTHAMINI kazi na mchango mkubwa unaotolewa na wasanii mbalimbali hapa nchini. Siku hii imeanza kuadhimishwa rasmi hapa nchini kuanzia mwaka 2014 ambapo baadhi ya wasanii waliweza kupewa tuzo na aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati huo Mh, Dr. Mohamed Gharib Bilal kutokana na umahiri wao kwenye Sanaa walizozifanya na kuliletea taifa sifa ndani na nje ya Mipaka. Mradi huu umeendelea kukua mwaka hadi mwaka na kuwashirikisha wasanii na wadau wengi Zaidi wa Sanaa hapa nchini kama ambavyo itaendelea kushuhudiwa mwaka huu kwenye maadhimisho ya SIKU YA MSANII 2016.

Msanii wa kizazi kipya Juma Nature anatarajia kufanya mavitu yake kesho Jumamosi katika Siku ya Msanii Makumbusho jijini Dar es Salaam.
 SIKU YA MSANII 2016
Siku ya Msanii mwaka 2016 imejumuisha mtiririko wa matukio ambayo yanakwenda kuakisi kauli mbiu yake ya mwaka huu yaani “NGUVU YA SANAA” Tayari maadhimisho haya yalizinduliwa mnamo tarehe 26 mwezi Mei 2016 kwenye ukumbi wa Alliance Francaise ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mh. Nape Moses Nnauye ambaye aliwakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Elisante Ole Gabriel. Uzinduzi huu ulidhihirisha kukua kwa maadhimisho haya kwani yalihusisha mjumuiko wa Sanaa kutoka nchi ya Ufaransa ambapo pia mjumuiko huu utaendelea kwenye matukio mengine yajayo hasa tukio la TAMASHA LA SANAA ambalo linakuja hapo tarehe 24 mwezi Septemba 2016 pale kwenye viwanja vya kijiji cha Makumbusho Kijitonyama Dar es salaam.

Maadhimisho ya mwaka huu kilele chake kitakuwa hapo tarehe 29 Oktoba 2016 ambapo wasanii mbalimbali watapewa tuzo ambapo baadhi ya wasanii watakaokuwa wamepitia mchujo mkali wa kitaaluma na vigezo vilivyowekwa watatunukiwa tuzo mbalimbali kuonyesha mchango wao kwenye sekta ya Sanaa na taifa kwa jumla.
Peter Msechu.
TAMASHA LA SANAA
Kwa mara ya kwanza hapa nchini, SIKU YA MSANII inawakutanisha wasanii wa ainza zote nne za Sanaa kwenye eneo moja yaani Sanaa za muziki, filamu, ufundi na maonyesho ili kuonyesha umahiri wao kwa hadhira. Hili ni tamasha la siku nzima yaani kuanzia saa 3 asubuhi mpaka saa 3 usiku ambapo kutakuwa na maonyesho ya kazi mbalimbali za Sanaa kama ufundi na maonyesho na baadae kuhitimishwa na burudani mbalimbali za muziki kutoka kwa wanamuziki wa mitindo mbalimbali ya muziki ikiwa na lengo la kuonyesha Nguvu waliyonayo wasanii pale wanapoungana pamoja.
 
SHUGHULI ZITAKAZOKUWEPO
1.     Tamasha hili litapambwa na shughuli mbalimbali ili kuifanya kuwa siku maalum ya wakazi wa jiji la Dar es salaam na vitongoji vyake kufika na familia zao na wao pia kujionea umahiri wa wasanii wetu nchini. Shughuli zitakazokuwepo ni pamoja na;
2.     Maonyesho ya kazi za Sanaa za ufundi (uchongaji, ufinyanzi, ushonaji, ufinyanzi na nyingine nyingi) siku hii wale wasusi wote maarufu hapa mjini watahamia kwenye tamasha la Sanaa hili hivyo wale kina mama siku hiyo waje makumbusho kusukwa.

3.     Maonyesho maalum ya filamu za kitanzania ambapo pamoja na kuona wadau wa filamu watapata fursa ya kununua filamu kazi zilizotengenezwa na wasanii wetu maarufu hapa nchini.

4.     Burudani ya muziki wa aina zote utakuwepo huku ukisindikizwa na burudani kutoka kwa ma DJ maarufu wa enzi hizo wakishirikiana na ma DJ wa sasa ili kuhakikisha wadau wanapata burudani isiyochosha kwa siku nzima.

5.     Kutakuwa pia na huduma ya chakula na vinywaji kuanzia asubuhi mpaka jioni ili watu watakaofika kwenye viwanja vya makumbusho waweze kupata huduma zote kusindikizia burudani itakayokuwepo hapo.

Huduma ya utoaji damu itakuwepo.
6.     Kutakuwa na huduma ya uchangiaji damu
7.     Kutakuwa na Jukwaa la Sanaa ambalo litaongozwa na BASATA na Cosota katika kutoa elimu kwa wasanii mbalimbali

8.     Kutakuwa na elimu ya mifuko ya jamii kwa wasanii na jamii ambayo itakuja katika Tamasha

Ifakara Band ni miongoni mwa makundi yatakayotoa burudani ya muziki wa dansi.
BURUDANI
Tamasha hili litashehenezwa na wasanii wa muziki mbalimbali kama ifuatavyo;
Bongo fleva;            Juma Kassim Nature
                                    Peter Msechu
                                    Misoji na wengine wengi ambao watapanda katika jukwaa

Muziki wa Dasi;     CHAMUDATA All Stars (wasanii maarufu wa zamani wataungana na wasanii wa sasa kutoa burudani)
                                    Ifakara Band
                                    John Kitime
Singeli;                      Amsha Group na makundi mbalimbali ya singeli
Ngoma za Asili;      Mandela Group
                                    Safari Group na sarakasi
Taarab;                      Siza Segere
                                    Super Shine

Komedi/Mchekeshaji;     Mluga luga na wachekeshaji mbalimbali
Ma DJ;                       Dj Ibony Moalim
                                    DJ John Pantalikis
                                    Dancer Athuman DigaDiga
Wanamuziki mbalimbali wa nyimbo za injili pia watatoa burudani kuhamasisha Amani ya nchi yetu.

Mtiririko wote huu wa burudani utawahakikishia wadau mbalimbali wa Sanaa watakaofika kuendelea kuwepo mpaka itakapofikia tamati ya tamasha hili kubwa kabisa la Sanaa hapa nchini.

Wanamuziki wa Nyimbo za Injili watakuwepo kuombea taifa amani.
ENI RASMI
Mgeni rasmi kwenye Tamasha hili la Sanaa atakuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mh. Anastazia Wambura (Mb) ambaye pia ataambatana na wageni wengine mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi yetu.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura ndiye mgeni rasmi Jumamosi katika Siku ya Sanaa Tanzania katika Kijiji cha Makumbusho jijini Dar es Salaam.
MWISHO
Tamasha hili ni la wazi yaani halina kiingilio hivyo tunawakaribisha wananchi wote wakazi wa Dar es salaam na vitongoji vyake  wafike bila kukosa kuja kuona mseto wa Sanaa na burudani na pia kuona nguvu ya Sanaa pia kutokosa pale kwenye viwanja vya kijiji cha Makumbusho tarehe 24 Septemba 2016 ,ulinzi utakuwa wa uhakika kwani tumejipanga vizuri sana na pia wapenzi wa nyama choma zitakuwapo  kwani maandalizi yake yamekamika kila kitu tulichopanga kitakuwapo bila kukosa,shughuli hii itaanza kuanzia asubuhi saa tatu hadi saa tatu usiku.

Imeandaliwa
Godfrey Mahendeka
Mkurungezi

No comments:

Post a Comment