Na Mwandishi Wetu
WAWAKILISHI pekee wa Tanzania katika mashindano ya
kimataifa Yanga (pichani), leo wamejiweka katika mazingira mazuri ya kucheza hatua
inayofuata ya Kombe la Shirikisho la Afrika baada ya kuisasambua GD Esperanca
ya Angola katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam
baada ya kushinda mabao 2-0.
Mashujaa wa Yanga katika mchezo huo ni Simon Msuva na
Matheo Antony Simon, baada ya kufunga mabao hayo katika kipindi cha pili cha
mchezo huo, ambao unaiweka Yanga katika nafasi nzuri zaidi ya kutinga hatua ya
makundi.
Kwa ushindi huo, vijanao hao wa Jangwani sasa
wanahitaji sare, au ushindi wa aina yoyote na hata kufungwa 1-0 au kufungwa 2-1
ili kutinga wiki ijayo baada ya mchezo huo wa marudiano utakaofanyika Mei 17
Angola.
Mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe akimtoka beki wa
Sagrada Esperanca, Antonio Kasule
|
Katika mchezo huo uliochezeshwa na waamuzi kutoka
Ghana, Joseph Lamptey aliyeuwa kati akisadiwa na David Laryea na Malik Salifu
walioshika vibendera, Yanga walipoteza nafasi kibao za wazi za kufunga katika
kipindi cha kwanza.
Kinara wa mabao katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara,
Amissi Tambwe ndiye aliyekosa mabao
mengi baada ya kupoteza nafasi nyingi za wazi katika kipute hicho cha leo
jijini Dar es Salaam.
Hatimaye chipukizi wa Yanga, Msuva na Matheo wakapeleka
raha katika mitaa ya Jangwani Twiga baada ya kufunga mabao hayo mawili
yaliyowanyamazisha kabisa Waangola.
Msuva alianza dakika ya 72 akimalizia krosi maridadi
ya winga Godfrey Mwashiuya aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya
Malimi Busungu, kabla ya Metheo kufunga la pili dakika ya 90 kwa shuti la
mbali.
Pamoja na ushindi huo, Yanga ilionekana kabisa
kuathiriwa na kuwakosa nyota wake wawili Wazimbabwe, kiungo Thabani Kamusoko na
mshambuliaji Donald Ngoma ambao walikuwa wanatumikia adhabu za kadi za njano
walizopewa mfululizo kwenye mechi dhidi ya Al Ahly mwezi uliopita.
Kikosi
cha Yanga kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar
Joshua, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Salum Telela/Mbuyu Twite dk46,
Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Malimi Busungu/Godfrey Mwashiuya dk53, Amissi
Tambwe na Deus Kaseke/Matheo Anthony dk77.
No comments:
Post a Comment