Sunday, 22 May 2016

Geita Gold Mine (GGM) yachangisha Sh. Milioni 700 kusaidia mapambano ya Ukimwi


Mkuu wa Kituo cha Watoto Yatima cha Moyo wa Upendo cha Geita, Sista Adalbera Mukure akipokea mfano wa hundi yenye thamani ya sh. milioni 150 kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano, January Makamba. Katikati ni Mkurugenzi Mkuu wa Geita Gold Mine (GGM), Terry Mulpeter katika hafla iliyofanyika katika hoteli ya Kilimanjaro Hyatt Regency Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu
MGODI wa Dhahabu wa Geita (GGM) umechangisha kiasi cha Sh. Milioni 700, huku Kituo cha Watoto Yatima cha Moyo wa Huruma kikipewa kiasi cha sh. Milioni 150,000.

Hayo yalisemwa katika hafla ya 15 ya uzinduzi wa ukusanyaji fedha kwa ajili ya kuzipatia fedha taasisi mbalimbali zinazoshughulika na kupambana na Ukimwi iliyofanyika katika hoteli ya Hyatt Kilimanjaro jijini Dar es Salaam juzi.
aziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano, January Makamba (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa GGM, Terry Mulpeter wakiinua mikono ya Mkuu wa Wilaya ya Geita, Manzie Mangochie baada ya kumkabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya sh. Milioni 150.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano, January Makamba aliyemuwakilisha Makamu wa Rais, Samia Hassan Suluhu.
 
January katika hafla hiyo aliongoza hambee, ambapo jumla ya sh. milioni 23 zilipatikana ukumbini hapo, sh. milioni 8 zikiwa fedha taslimu na zilizobaki ahadi ukumbini hapo, huku zingine zikichangishwa na taasisi na watu mbalimbali.
 
Akisoma hotuba kwa niaba ya Suluhu, January aliwataka watu na taasisi mbalimbali kuchangia mfuko huo, ambao sasa umetimiza miaka 15 tangu kuanzishwa kwake.

Aliitaka GGM kuendelea na moyo huo wa kuchangisha fedha kwa ajili ya vituo, taasisi na vituo mbalimbali vinavyohudumia waathirika wa Ukimwi, hasa watoto yatima.
Makamu wa Rais wa GGM, Simon Shayo akitoa ahadi kununua picha iliyokuwa ikinadiwa wakati wa uchagishaji fedha za mfuko wa Kili Challenge kwenye hoteli ya Kilimanjaro.
 Mkurugenzi Mkuu wa GGM, Terry Mulpeter alisema kuwa wanahitaji kiasi cha sh. Bilioni 1 na sh. Milioni 300 zilizobaki wanatarajia kuzipata katika mfuko wa kupanda Mlima Kilimanjaro wa Kili Challenge.

Alisema fedha zilizotolewa mwaka huu ni kati ya sh. Bilioni 1 walizofanikiwa kukusanya mwaka jana na wanazokusanya mwaka huu watazitoa mwakani katika hafla ya 16.
 
 Baadhi ya taasisi zilizopatiwa fedha na kiasi cha fedha kikiwa katika mabano ni Kituo cha Watoto Yatima cha Moyo wa Huruma (Milioni 150), Wilaya ya Geita (Milioni 150), UVIKI Geita (Milioni 50), Benjamini Mkapa Foundation (Milioni 100) na Tacaids (Milioni 250,000).

Mkuu wa Kituo cha Watoto Yatima cha Huruma, Sista Aldalbera Mukure aliishuhuru GGM kwa msaada huo na kuzitaka taasisi zingine za umma na serikali kusaidia zaidi katika mapambano hayo.
 
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Manzie Mangochie alitoa shukrani kwa wote waliochangia mfuko huo, ambapo alisema kuwa fedha walizopewa zitasaidia mapambano ya Ukimwi wilayani mwake.

Aidha, Balozi wa Kili Challenge Mrisho Mpoto `Mjomba' alitumbuiza na kuzindua kibao chake kipya cha Sauti Nenda, ambacho kinaelezea jinsi watu bado wanavyoendelea kuwanyanyapaa wale walioathirika na ugonjwa wa Ukimwi.
Mtunzi na muimbaji wa kibao cha Sauti Nena, Mjomba Mrisho Mpoto (kushoto) akiwa na Banana Zorro wakati wa hafla hiyo katika hoteli ya Kilimanjaro.
 Mpoto aliimba kibao hicho pamoja na msanii mahiri wa Bongofleva, Banana Zorro katika hafla hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki katika hoteli ya Kilimanjaro Hyatty Regency jijini Dar es Salaam.






 
 
 
 
 
 

No comments:

Post a Comment