Mrisho Mpoto akisaini mkataba wa kuwa Balozi wa Kili Challenge. |
Na Mwandishi Wetu
MGODI wa Dhahabu wa Geita (GGM) kwa Kushirikiana na
Tume ya Kupambana na Ukimwi nchini (Tacaids) imemteua msanii maarufu wa
mashairi Mrisho Mpoto kuwa balozi wa kampeni ya Kili Challenge.
Hafla hiyo ilifanyika katika ofisi za GGM jijini Dar
es Salaam, ambapo Mpoto alisaini mkataba wa mwaka mmoja kuwa balozi wa Kili
Challenge.
Kili Challenge ni kampeni inayolenga kukusanya fedha
kwa ajili ya kutunisha mfuko wa mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi. Kampeni hiyo ilianza miaka
15 iliyopita na hufanyika kila mwaka kwa wadau mbalimbali kupanda mlima Kilimanjaro,
ambapo kwa mwaka jana walipanda watu 39 na kuchangisha takribani bilioni 1.2,
sehemu ya fedha itagaiwa kwa asasi mbalimbali za kiserikali na za kijamii
wakati wa sherehe za uzinduzi rasmi za sherehe ya mwaka huu zitakazofanyika Mei
20 katika hoteli ya Hyatt Kilimanjaro, ambapo mgeni rasmi atakuwa Makamu wa
Rais Mh. Samia Suluhu Hassan.
Mpoto ameteuliwa kuwakilisha na kuitangaza kampeni
hii ili kusaidiana na serikali pamoja na wadau mbalimbali ndani na nje ya
Tanzania, kupambana na janga hili la Taifa. Pia kwa kuwa ni msanii na kupitia
kazi zake za sanaa na ushawishi wake ndani ya jamii ataweza kuihamasisha jamii
ipasavyo kuona umuhimu wa kumaliza tatizo hili hasa katika masuala ya
unyanyapa.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dk.
Fatma Mrisho, “Inakadiriwa kuwa watu milioni 1.6 nchini wanaishi na VVU na
Ukimwi. Ugonjwa wengi umewaathiri zaidi vijana na watoto yatima zaidi ya
milioni 1.3. Tunahitaji kubadilisha hali hii. TACAIDS kwa kushirikiana na mgodi
wa Dhahabu wa Geita (GGM) na wadau wengine kwa kupitia mpango huu wa
Kilimanjaro Challenge tunapenda kutoa mchango na ushirikiano wetu kwa Taifa ili
kutunisha mfuko utakaowezesha kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa huo,”
“Napenda kuupongeza mgoni wa Dhahabu wa Geita kwa
kushirikiana na wadau wengine kwa kuamua kwa dhati kwa kipindi cha miaka 15
kuwekeza katika mradi huu kwa kuuwezesha kuwa mradi wa kitaifa na si wa GGM,
hivyo pamoja na balozi wetu hivi sasa Mpoto tuungane nao ili kuongeza chachu
kwa wadau wengine kujitokeza kuongeza nguvu katika mapambana dhidi ya janga
hili,” alisema Dk. Mrisho.
Mrisho Mpoto 'Mjomba' akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Tacaids nchiniDk. Fatma Mrisho. |
Aliongeza … “Kwa kushirikiana na Mpoto tunamatumaini
ya kujenga timu imara yenye hamasa ya kutuma ujumbe popote Tanzania na duniani
ili kupambana na janga hili. Tunatoa wito kwa makampuni na wadau mbalimbali wa
ndani na nje ya nchi wajitokeze ili kushirikiane kutunisha mfuko wa Kilimanjaro
Challenge na mwishowe kufikia ndoto au malengo ya nchi yetu ya kuhakikisha
tunakuwa na kizazi kisicho na maambukizi ya VVU na Ukimwi,” Bw. Saimon Shayo,
Makamu Rais wa miradi endelevu wa Anglogold Ashanti (GGM).
Shayo alisisitiza kwa kusema “GGM iko tayari
kushirikiana na wadau wengine nia ya dhati, kuungana pamoja kupitia mfumo wa
Kili Challenge katika kuhakikisha maambukizi haya hayaendelei kuleta athari kwa
jamii yetu kwa sababu serikali yenyewe haitaweza kutokomeza tatizo hili,”
Naye Balozi mpya wa Kili Challenge, Mpoto alisema “Nashukuru
sana kwa kupata fursa hii ya kuweza kutoa mchango wangu katika kuisadia jamii
kuepukana na janga hili. Changamoto kubwa inayotokana na janga hili la VVU na
Ukimwi ni ongezeko la maambukizi ya VVU kwa vijana ambao, ndio nguvu kazi ya
Taifa letui pasipo kila mmoja wetu kujitoa kwa dhati hatutalimaliza janga hili.”
Pamoja na hatua kubwa zilizopigwa na serikali
ikishirikiana na wadau, kumekuwepo na ongezeko la maelfu ya watoto yatima
wanaohitaji misaada baada ya wazazi wao kufariki, wajane wasiokuwa na kipato,
pamoja na wazee wanaolazimika kuwalea wajukuu walioachwa na watoto wao, ambao
walifariki kutokana na ugonjwa huo ulisisitiza Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS.
Kilimanjaro Challenge ni mradi unaolenga kutoa elimu
kwa jamii kuhusu ugonjwa wa ukimwi na virusi vya ukimwi (VVU). Pia inalenga
kuchangisha fedha ili kujenga timu itakayoendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa
huo.
Ili kuweza kuwa sehemu yawatakaopanda Mlima
Kilimanjaro, kwa kupitia Kili Challenge mwaka huu, uwe mtu binafsi au kupitia
shirika kulipia wafanyakazi wake kupanda mlima mchango ni $5,000 tu, ambazo
zitalipia gharama za upandaji na kuchangia mfuko wa Kili Challenge.
Kilimanjaro Challenge imebakia kuwa chombo muhimu
kinachoshirikiana na taasisi za nje na ndani ya nchi katika mapambano dhidi ya
VVU na Ukimwi kwa jamii ya Kitanzania na dunia kwa ujumla ili kuwapa matumaini
ya kuhakikisha jamii inabaki bila kuathiriwa na ugonjwa huo katika miaka ijayo.
Mpango huo pia unalenga kusaidia serikali kukabiliana na VVU na Ukimwi sambamba
na kutoa nafasi kwa watalii wa ndani kuupanda mlima Kilimanjaro.
KUHUSU
Kili Challenge:
Kwa maelezo zaidi tembelea tovuti ya www.anglogoldashanti.com na www.geitakilichallenge.com.
Mrisho Mpoto 'Mjomba' akiteta jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Tacaids nchini, Dk. Fatma Mrisho. |
Mrisho Mpoto (katikati) pamoja na Makamu wa Rais GGM, Simon Shayo na Mkurugenzi wa Mtendaji wa Tacaids, Fatma Mrisho wakiwa wameshika mkataba wa kumfanya Mpoto kuwa Balozi wa Kili Challenge. |
Mrisho Mpoto akizungumza na wanahabari wakati wa kusaini mkataba wa kuwa Balozi wa Kili Challenge. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Tacaids, Dk. Fatma Mrisho. |
No comments:
Post a Comment