Friday, 22 November 2019

TAA Kujenga Madarasa Sekondari Wilaya Kibaha

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Leonard Mlowe (kushoto) leo akisalimiana na Kaimu Mkurugenzi wa Fedha na Biashara wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Josephine Kolola, ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Julius Ndyamukama kutoa msaada wa mifuko 300 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya shule za sekondari. Kulia ni Mkurugenzi wa Mji Kibaha, Jenifer Omolo na kushoto ni Afisa Habari wa Mji Kibaha, Innocent Byarugaba.

Na Mwandishi Wetu, Kibaha
MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), leo imetoa mifuko 300 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya shule za sekondari za Wilaya ya Kibaha, inayokabiliwa na upungufu wa madarasa 65.

Kaimu Mkurugenzi wa Fedha na Biashara wa TAA, Josephine Kolola aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Julius Ndyamukama amesema Mamlaka hiyo inaunga mkono jitihada za serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli za kutoa elimu bure kuanzia shule za msingi hadi sekondari, ambapo sasa kuongezeka kwa madarasa hayo kutachangia watoto wengi kupata elimu.

   Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Assumpter Mshama leo akizungumzia masuala mbalimbali ya wilaya hiyo, wakati wa hafla ya kuchangia mifuko 300 ya saruji, iliyotolewa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), ambapo kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa  Fedha na Biashara wa TAA,  Josephine Kolola, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Julius Ndyamukama.

“Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, ipo bega kwa bega na jamii katika kuziunga mkono jitihada mbalimbali za maendeleo zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, iliyopo chini ya Mhe. Dkt John Pombe Magufuli, ambapo inahakikisha vijana wengi wanapata elimu ya msingi na sekondari bure katika mazingira bora. Elimu wanayopata vijana wetu itawasaidia kukabiliana na changamoto za maisha kwa ajili ya ustawi wao na Taifa kwa ujumla,” amesema Kolola

Amesema katika kufanikisha jitihada hizo kwa vitendo na pia ni sera ya Mamlaka kurudisha kwa jamii kiasi cha mapato wanayozalisha ili waweze kutatua changamoto zinazowakabili, hivyo wametoa mifuko hiyo wakiwa na imani itasaidia kujenga madarasa hayo.

Amesema TAA ni taasisi ya serikali iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Wakala wa Serikali Na.30 ya mwaka 1997 na kupewa dhamana na Serikali ya kusimamia na kuendesha jumla ya viwanja 58 vilivyopo Tanzania Bara, ambapo Serikali inafanya jitihada kubwa katika kuboresha miundombinu mbalimbali Viwanjani ili viweze kuendana na mahitaji ya soko na ushindani wa kibiashara.

 Kaimu Mkurugenzi wa  Fedha na Biashara wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA),  Josephine Kolola, leo akizungumza na waandishi wa habari na watendaji wa Halmashauri ya Mji Kibaha (hawapo pichani), wakati alipomuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Mhandisi Julius Ndyamukama na kukabidhi mifuko 300 ya saruji kwa ajili ya kujenga madarasa ya shule za sekondari za wilaya hiyo.


“Hivyo kupitia juhudi hizi za serikali zimezalisha fursa mbalimbali viwanjani zikiwemo fursa za kibiashara, ajira rasmi na zisizo rasmi”, amesema.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Assumpter Mshama pamoja na kuishukuru TAA kwa msaada huo mkubwa, amesema katika Kampeni yao ya “Elimisha Kibaha”, wamekusudia kujenga madarasa 65, na kununua viti 3250 na meza 3250 ili kuweka mazingira bora ya kusoma kwa wanafunzi.

“Tunaupungufu mkubwa wa madarasa ambapo wanafunzi 700 wa kidato cha Kwanza mwaka huu (2019) wamekumbwa na kadhia hii, nasi tukaamua waingie darasani kwa awamu mbili asubuhi na mchana, lakini bado ikawa shida kutokana na kuwa na watoto wengi, ndio maana tukaanzisha kampeni hii kwa lengo la kupunguza na ikiwezekana kuondoa kabisa tatizo na watoto wasome katika mazingira bora,” amesema Mkuu huyo.

Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Assumpter Mshama (kushoto) akipokea mifuko 300 ya saruji kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa Fedha na Biashara wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Josephine Kolola (kulia), katika hafla iliyofanyika leo nje ya jengo la Halmashauri ya Mji Kibaha. Kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Jenifer Omolo.
Amesema hadi sasa tayari wamekusanya vifaa vya kutosheleza ujenzi wa madarasa 26, lakini bado hawajaanza ujenzi kutokana na fedha zilizowasilishwa Hazina kushindwa kutolewa hadi sasa kutokana na kuwa na utaratibu mrefu, ambapo amekuwa na hofu huenda hadi kufika Januari mwaka 2020 wakakumbwa na kadhia ya wanafunzi kushindwa kuendelea na kidato cha Kwanza kutokana na kukosekana na madarasa ya kutosha.

“Tunaomba huko tulipopeleka hizi fedha cash basi wazitoe ili ujenzi uanze mlolongo ni mrefu sana hatujui tatizo lipo wapi, na watui ndio kama hivi wanachangia vifaa tunashindwa kuanza ujenzi,” amesisitiza Mhe. Mkuu wa Wilaya.  

 Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kibaha (kulia), ikiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya hiyo, Assumpter Mshama (wapili kushoto), Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Jenifer Omolo (kushoto), Katibu Tawala wa Mji Kibaha, Sosi Ngate (mwenye kilemba) wakiwa pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Fedha na Biashara wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Josephine Kolola aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Julius Ndyamukama.


Hatahivyo, amemshukuru. Rais Dk John Pombe Magufuli kwa jitihada zake za kutoa elimu bure ambayo imesababisha mwamko mkubwa kwa wazazi wengi kuwapeleka watoto wao shule. Hali kadhalika kawashukuru wananchi, walimu na wadau wote waliojitokeza kuchangia kwa kutoa fedha taslimu, vifaa na ahadi, ambapo tayari wameshakusanya Shilingi milioni 950
.

No comments:

Post a Comment