Na Mwandishi Wetu
NDEGE aina ya Bombardier zitaweza kutua katika Kiwanja cha Ndege
cha Arusha baada ya kukamilika mpango wa kuongezwa barabara ya kutua na kuruka
ndege, imeelezwa.
Hayo yalisema bungeni mjini Dodoma juzi na Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Issac Kamwelwe wakati akijibu swali la Mhe Husna
Malima, Mbunge wa Kigoma Kusini aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani
kuboresha Kiwanja cha Ndege cha Arusha ili ndege kubwa ziweze kutua.
Malima alisema kuwa kuongezwa kwa uwanja huo kutawawezesha
wananchi wa mikoa ya Singida, Manyara, Simiyu, Mara na Dodoma kuamasika kutumia
usafiri wa ndege, ambao unatosheleza kwa sasa?
Amesema mafaniko ya uwepo wa ndege nyingi za abiria nchini ni
pamoja na ndege hizo kutumika kwa wananchi kuzipanda.
Kamwelwe amesema kurefushwa huko kutafanikisha ndege aina ya
Bombardier ambayo inabeba abiria kuanzia 70 kutua na kuruka bila tatizo kwenye
kiwanja hicho kilichopo Kisongo mkoani Arusha.
Amesema tayari bajeti imetengwa kwa ajili ya kazi hiyo, ambapo
kiwanja hicho ni cha tatu nchini kwa kutua na kuruka ndege nyingi, ambapo hutua
ndege zaidi ya 125 kwa siku.
“Tumeweka bajeti kuendeleza kiwanja cha ndege cha Arusha na
tayari tenda imetangazwa, kiwanja hiki kinaongoza kwa kutua ndege nyingi zaidi
kwa siku ni biashara kubwa na ndio maana tunataka ndege ya Bombardier itue
hapo,” alisisitiza Mhe. Kamwelwe.
Amesema mikoa jirani na Arusha ya Manyara, Singida, Dodoma,
Simiyu na Mara itafaidika na maboresho ya kiwanja hicho kwa kuwa wataweza
kukitumia ipasavyo.
Naye Meneja wa Kiwanja hicho, Mhandisi Elipid Tesha amesema
barabara ya kutua na kuruka ndege itaongezwa urefu kwa meta 200, ambapo sasa
ina urefu wa meta 1600 na itakuwa 1800, na pia patajengwa eneo la kugeuza
ndege.
Mhandisi Tesha amesema kwa sasa kazi inayoendelea ni ujenzi wa
eneo la maegesho ya ndege (Apron), ambayo yakikamilika yatapunguza msongamano
kwa asilimia 30; pia barabara ya kupita ndege kwenda katika maegesho
(taxiway); ujenzi wa maegesho ya magari
yapatayo 350 kwa kiwango cha lami.
Pia ujenzi wa mfumo wa malipo ya maegesho hayo unaendelea
sambamba na ule wa maegesho ya magari.
Pia amesema ujenzi huo wa maboresho ya kiwanja cha ndege cha
Arusha utahusisha ujenzi wa eneo la kupumzika abiria, ofisi za waegesha ndege
(mashellers), kibanda cha ulinzi na vyoo.
No comments:
Post a Comment