Skauti wa shule ya Sekondari ya Ilala
(kushoto) akimvisha skafu mgeni rasmi wa mahafali ya 13 ya shule hiyo, Bi. Harieth
Nyalusi, Kaimu Meneja Biashara na Masoko wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
Tanzania (TAA), aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu Mhandisi Julius Ndyamukama.
Mahafali hayo yamefanyika hivi karibuni.
Na Bahati Mollel,TAA
WANAFUNZI
1560 wa shule ya sekondari ya Ilala ya Jijini Dar es Salaam, watasoma kwa
furaha baada ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kukubali kufanya ukarabati
wa jengo la maktaba, ambalo ni chakavu.
Ahadi
hiyo imetolewa hivi karibuni na Kaimu Meneja Masoko na Biashara wa TAA, Harieth
Nyalusi ambaye alikuwa mgeni rasmi wa mahafali ya 11 ya shule hiyo, akimwakilisha
Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Julius Ndyamukama.
Nyalusi
alisema kuwa Mamlaka inaunga mkono jitihada kubwa zinazofanywa na Mhe. Rais wa
Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli za kutoa elimu bure,
ambapo sasa itaungana naye katika kukarabati chumba hicho cha maktaba, ili
kuwezesha wanafunzi kusoma katika mazingira bora, yatakayochangia kufanya vyema
katika masomo yao na katika mitihani ya kidato cha pili na yake ya kuhitimu kidato cha nne.
Mwanafunzi Diana Seth wa shule ya
sekondari ya Ilala (kulia) akionesha moja ya majaribio katika maabara ya
Biolojia, wakati wageni waalikwa pamoja na mgeni rasmi wa mahafali ya 13 ya
shule hiyo, Bi. Harieth Nyalusi kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
Tanzania (wa pili kushoto),
akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Julius Ndyamukama walipotembelea
maabara hiyo.
“Pamoja na kuunga juhudi za Mhe. Rais pia ni sera ya taasisi yetu kutoa kwa jamii katika kusaidia kutatua changamoto zinazozibabili jamii hizo, hivyo kama Mamlaka tutasaidia kufanya ukarabati wa ndani wa jengo hilo ambalo limekuwa chakavu, linalosababisha ari ya kusoma kushuka,” amesema.
Pia
alisema Mamlaka inatambua jitihada kubwa inayofanywa kwa kushirikiana kwa Walimu,
wazazi na wanafunzi katika kuhakikisha shule inaboresha utoaji wa elimu bora na
ufaulu wa wanafunzi wa mitihani yao ijayo kuongezeka.
Hatahivyo,
ametoa wito kwa wahitimu wa kidato cha Nne 2019 kuhakikisha wanaweka nia
thabiti ya kujiendeleza zaidi kwa wale watakaobahatika kuchaguliwa kwenda kidato cha Tano na vyuo mbalimbali, na
ambao hawatabahatika waangalie nyanja mbalimbali za elimu ili kujitengenezea
wigo mpana wa uwezo wa utambuzi wa kubadilisha changamoto zinazoizunguka jamii
kuwa fursa.
Kaimu Meneja wa Biashara na Masoko wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania
(TAA), Bi. Harieth Nyalusi (aliyesimama), akiwakilisha salamu kutoka kwa
Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Julius Ndyamukama wakati wa mahafali ya 13 ya shule
ya sekondari ya Ilala ya Jijini Dar es Salaam, yaliyofanyika hivi karibuni.
Akiizungumzia
TAA, Nyalusi amesema imepewa jukumu la kusimamia na kuendeleza viwanja vya
ndege 58 vilivyopo Tanzania Bara kati ya hivyo ni viwanja vya Kimataifa vya
Julius Nyerere (JNIA) na Kilimanjaro (KIA), ambavyo ndivyo milango mikuu ya
kuingia nchini kwa kutokea nje ya nchi.
Amesema
katika viwanja vya ndege kuna fursa mbalimbali za kibiashara, ajira rasmi na
zisizo rasmi, ambapo amewataka vijana wanaohitimu kuzichangamkia ajira na fursa
hizo pindi zitakapotangazwa.
Wanafunzi skauti wa shule ya sekondari ya
Ilala wakionesha ukakamavu kwa kupasuliwa tofali kichwani katika sherehe za
mahafali ya 13 ya shule hiyo yaliyofanyika hivi karibu.
Kwa upande wa risala ya wahitimu, imeeleza kuwa shule hiyo iliyoanzishwa miaka 13 iliyopita pamoja na kufanya vyema kwenye mitihani yao ya taifa ya kumaliza kidato cha nne kila mwaka, imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya upungufu wa vyoo vya wanafunzi, ambapo yapo matundu 18 kati ya 72 yanayohitajika; ukosefu wa maabara mbili za masomo ya Biolojia na Fizikia ambazo ujenzi wake haujakamilika.
Changamoto
nyingine ni uchakavu wa majengo ya shule ikiwemo kuvuja kwa paa na ubovu wa
sakafu madarasani; uchakavu wa rangi katika majengo yote ya shule; ukosefu wa
chumba maalum cha watoto wa kike na wagonjwa pindi wapatapo matatizo wanapokuwa
eneo la shule; ukosefu wa vifaa vya teknolojia na mawasiliano zikiwemo komputa,
projeta, mashine za kurudufia na ‘printer’.
Mmoja wa skauti wa shule ya sekondari ya
Ilala ya Jijini Dar es Salaam akizuia pikipiki mbili kwa mikono na kichwa
katika sherehe za mahafali ya 13 ya shule hiyo yaliyofanyika hivi karibuni.
Risala
hiyo imeainisha pia changamoto za ukosefu wa jengo la ofisi za walimu, ambapo
sasa wanatumia madarasa mawili kama ofisi jambo ambalo pia kumesababisha kuwe
na upungufu wa madarasa; uchakavu wa maktaba na ukosefu wa vifaa muhimu ndani
ya maktaba zikiwemo meza, viti, vitabu vya kiada na ziada, makabati; ukosefu wa
kantini bora ya shule na ukosefu wa bwalo.
Pamoja
na changamoto hizo, wahitimu hao wameahidi kufanya vyema katika mitihani yao ya
kuhitimu kidato cha nne, ambapo kila mwaka ufaulu umekuwa ukiongezeka ambapo
sasa umefikia asilimia 70.
Wahitimu wa kidato cha Nne katika shule ya sekondari ya Ilala wakiimba wimbo wa kuwaaga wenzao pamoja na walimu katika mahafali yao yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment