Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison
Mwakyembe amewataka watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki mbio za 18 za
Kilimanjaro zitakazofanyika Machi mwakani,
Mwakyembe pia aliwataka wanariadha wa Tanzania kufanya
maandalizi ya uhakika ili kuhakikisha wanafanya vizuri katika mbio hizo, ambazo
ni kubwa zaidi hapa nchini na hushirikisha watu wengi kutoka ndani na nje ya
nchi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki wakati wa
uzinduzi wa mbio hizo, ambazo zitafanyika mjini Moshi Machi mosi, 2020, mwakyembe
alisema ni aibu kwa zawadi zote kwenda nje ya nchi, hivyo aliwataka wanariadha
wa Tanzania kujiandaa vizuri ili kuhakiisha zawadi hizo zinabaki nchini.
Mwakyembe aliwapongeza wadhamini wa mbio hizo wakiongozwa na Kilimanjaro
Premium, ambao hudhamini mbio za kilometa 42, Tigo (kilometa 21), Grand Malt
(kilometa 5), ambazo ni mbio za kujifurahisha na hushirikisha watu wengi.
“Inatia moyo sana kuona kuwa Kilimanjaro Marathon sasa ina
washiriki zaidi ya 11,000 kutoka nchi zaidi
ya 56 kote duniani. Hili ni jambo zuri sana kwa taifa, kwani tunapata fedha za
kigeni kutokana na matumizi yanayofanywa na wageni hawa nchini, ikiwemo utalii,
“alisema.
Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Anthony Mtaka,
alitoa wito kwa washiriki wazalendo kuchangamkia zawadi zinazotolewa na
Kilimanjaro Marathon badala ya kukimbilia kushiriki mbio za nje, ambazo zawadi
zake ni ndogo.
“Ni vizuri kwenda kupata
exposure lakini tusiache zawadi nzuri nyumbani na kufuata hela ndogo huko nje
wakati tunaweza kuzipata hapa hapa nchini, “alisema Mtaka.
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Pamela Kikuli,
alisema tangu mashindano yaanze Kilimanjaro Premium Lager imewekeza hela nyingi
sio tu kusukuma mauzo ambayo wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa, lakini pia
kutengeneza ajira na kuchangia uchumi kwa ujumla kupitia gharama za kuyatangaza,
promosheni na masuala mengine ya kimasoko.
Naye Meneja Mawasiliano wa Tigo, Woinde Shisael alisema kampuni yake
inajivunia kudhamini mbio za kilometa 21 kwa mwaka wa tano mfulululizo, ambayo
ni sehemu ya mbio hizo. “Tunajivunia kuwa sehemu ya tukio hili kubwa ambalo
linawaleta pamoja wanariadha wakubwa, “alisema.
Wadhamini wengine katika Kilimanjaro Marathon ni pamoja na
Kilimanjaro Water, Barclays Bank, Simba Cement, TPC Sugar, Precision Air, Kibo
Palace Hotel, Garda World Security, Keys Hotel na CMC Automobiles.
Kwa mujibu ya waandaaji wa Kilimanjaro Marathon-Wild Frontiers
na Executive Solutions, usajili umeshaanza kwa mtandao kupitia
www.kilimanjaromarathon.com.
Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa na mwenyekiti na kaimu katibu mkuu
wa Baraza la Michezo la Taifa, Leodegar Tenga na Neema Msitha, kaimu msaijili
wa michezo nchini, Mwita, Bodi ya Utalii na wadau wengine swa mchezo wa riadha.
No comments:
Post a Comment