Friday, 15 November 2019

Usipime Usajili Kilimanjaro Marathon 2020


Na Mwandishi Wetu, Moshi
MAANDALIZI ya 18 ya Kilimanjaro Marathon 2020 yameanza kwa kasi huku ikiwa ni juu ya asilimia 30 ikilinganishwa na wakati kama huu mwaka jana, ikiwa ni ongezeko la asilimia 10 ndani ya wiki moja.

Mbali na mbio za kilometa 42, ambzo hudhaminiwa na wadhamini wakuu, Bia ya Kilimanjaro Lager, mbio zingine ni zile za kilometa 21 za Tigo na zile za Grand Malt za kilometa tano.

Kwa mujibu wa taarifa ya waandaaji, mwendendo ni mzuri na wamewataka washiriki kuchangamkia punguzo la bei litakalodumu hadi mwezi Januari mwakani. Washiriki wanajisajili kwa kupitia www.kilimanjaromarathon.com na kwa Tigopesa kwa kubonyeza *149*20#.

Mkurugenzi wa Mbio hizo nchini, John Bayo alisema kwa kupitia taarifa hiyo kuwa kuna idadi maalumu ya washiriki inayotakiwa kwa mbio zote tatu (Kilimanjaro Premium Lager Km 42, Tigo km 21 na Grand Malt Km 5) ili kuhakikisha kuwa mbio hizo zinaendana na viwango vya Shirikisho la Kimataifa la Riadha (IAAF) ili kuhakikisha usalama unazingatiwa.

Kwa mujibu wa Bayo, hii pia itahakikisha washiriki wanafurahia mbio hizo bila ya msongamano na pia kutoa nafasi kwa waandaaji waweze kutoa huduma zinazotakiwa katika njia ya mashindano na sehemu ya kumalizia pia.

Kuhusu punguzo la bei, waandaaji hao pia walitoa wito kwa washiriki wachangamkie utaratibu huo ambao ulianza Oktoba Mosi 2019 hadi Januari 14 , 2020.

Kwa raia wa Tanzania na wale kutoka nchi za Afrika Mashariki watalipa Sh 15,000 kwa mbio za kilometa 42 na 21 na Sh 5,000 kwa kilometa tano lakini kuanzia Januari 15, 2020 hadi Februari 16, 2020 washiriki watakaojisajili watalipa Sh 20,000 kwa kilometa 42 na 21 na Sh 5,000 kwa kilometa tano.

Kwa wageni wakazi au wenye vibali vya kuishi na kufanya kazi na wale wa nchi za SADC watalipa dola za Marekani 35 kwa kilometa 42 na 21 na dola tano kwa kilometa tano kuanzia Oktoba 1, 2019 hadi Januari 14, 2020, lakini kuanzia Januari 15, 2020 hadi Februari 16, 2020 wanaojisajili watalipa dola 45 kwa kilometa 42 na 21 na dola tano kwa kilometa tano.

Washiriki wa kimataifa watalipa dola 70 kwa kilometa 42 na 21 na dola tano kwa kilometa tano kuanzia Oktoba 1, 2019 hadi Januari 14, 2020 na kuanzia Januari 15 hadi Februari 16, 2020 watalipa dola 85 kwa marathon na nusu marathon na dola tano kwa kilometa tano.

Kwa mujibu wa waandaaji hao, usajili utafungwa rasmi saa sita usiku Februari 16, 2020 au pale ambapo idadi inayotakiwa itatimia.

Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa na wawakilishi kutoka Chama Cha Riadha Tanzania, Baraza la Michezo Tanzania, Bodi ya Utalii Tanzania na wadau wengine wa riadha.

Washiriki pia walikumbushwa kuhusu vituo vya kuchukulia namba zao za ushiriki ambapo kwa Dar es Sallaam ni Mlimani City kuanzia Februari 22-23, 2020, Arusha ni Hoteli ya Kibo Palace kuanzia Februari 25-26 na Moshi ni Hoteli ya Keys kuanzia Februari 27-28.

 “Washiriki watatakiwa kujitambulisha na kuthibitisha kuwa wameshalipia kabla ya kukabidhiwa namba zao,” ilisema taarifa hiyo ya waandaaji.

Wadhamini wa mbio za Kilimanjaro Marathon 2020 ni Kilimanjaro Premium lager, Tigo, Grand Malt Kilimanjaro Water, TPC Limited, Simba Cement, Barclays Bank na watoa huduma rasmi ni Kibo Palace Hotel, Keys Hotel, GardaWorld Security, Precision Air na CMC Automobiles.

Mashindano ya Kilimanjaro Marathon yanayoandaliwa na Wild Frontiers na kuratibiwa kitaifa na Kampuni ya Executive Solutions,  yanatarajiwa kufanyika Machi 1, 2020 katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi.

Uzinduzi wa Kilimanjaro Marathon 2020 ulifanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam na kuzinduliwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Mjichezo, Dk Harrison Mwakyembe.


No comments:

Post a Comment