Na Mwandishi Wetu, Kibaha
MCHEZO mpya ujulikanao kama Teq Ball umetambulishwa
rasmi Tanzania, ikiwa ni nchi ya kwanza katika Kanda ya Tano ya Afrika,
imeelezwa.
Mchezo huo ulitambulishwa rasmi juzi katika Kituo cha
Michezo cha Filbert kilichopo Mkuza Kibaha mkoani Pwani na wawakilishi wa
Shirikisho la Kimataifa la Teq Ball (FITEQ), viongozi wa Kamati ya Olimpiki
Tanzania (TOC), na viongozi wa kituo hicho pamoja na wanafunzi.
FITEQ imetoa meza tatu na mipira 12, ambapo mbili
zitakuwa katika Kituo cha Olimpafrica, ambacho kinatumia vifaa vilivyopo katika
Kituo cha Michezo cha Filbert Bayi mjini hapa.
Kwa Tanzania, meza mbili, moja ya TOC zitakuwa
katika Kituo cha muda cha Olimpafrica kilichoko FBS Mkuza, nyingine Dole
Zanzibar. Meza ya Zanzibar ilitarajia kukabidhiwa jana kisiwani humo.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkuu wa Uhusiano wa
Kimataifa FITEQ, Marius Vizer Jr, alisema shirikisho hilo makao yake makuu yako
Hungary na sasa wako kwenye mikakati ya kuusambaza zaidi Duniani, baada ya kupata
usajili wa kimataifa mwaka 2017.
Mwenyekiti wa Bodi ya Shule za Filbert Bayi, Fibert Bayi akizungumza wakati wa uzinduzi wa mchezo wa Teq Ball uliofanyika Mkuza, Kibaha jana. |
Hadi sasa nchi 14 tayari zimefikiwa na mchezo huo.
Alisema FITEQ itatoa Euro 6,000 (sawa na Sh 15,276,600)
kwa mwaka kwa shirikisho la nchi husika kwa ajili ya uendeshaji, sambamba na
kuendesha mafunzo kwa makocha na waamuzi.
Naye Makamu wa Rais Kamati ya Olimpiki Tanzania
(TOC), Henry Tandau, aliishukuru FITEQ na kusema kuwa historia imeandikwa kwa
kuutambulisha mchezo huo.
Tandau, alisema wataitumia fursa hiyo kuhamasisha
mchezo huo kwa kuundwa chama cha kitaifa, kuusambaza mikoani, kisha mashindano
ya ngazi mbalimbali ili baadae uweze kuwa mchezo mkubwa nchini.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Shule za Filbert Bayi
(FBS), Filbert Bayi, mbali na kushukuru alisema watautendea haki msaada huo kwa
kuhakikisha unachezwa na kuundwa timu mbalimbali.
Mchezo huo ni mchanganyiko wa Mpira wa Meza na Mpira
wa Miguu, ambapo huhesabiwa kwa pointi zifikapo 20 kwa utofauti wa pointi
mbili.
Huchezwa kwa mchezaji moja moja au wawili wawili,
ukitumia meza iliyopinda, mpira kama wa miguu na viungo vya mwili miguu, kifua,
mabega na kichwa, isipoluwa mikono hairuhisiwi.
Mchezaji hatakiwi kutumia kiungo kimoja mara mbili,
pia kuugusa mpira zaidi ya mara tatu.
Na kabla ya uzinduzi wakufunzi wa mchezo huo kutoka
hungary, Gondos Zoltan na Vasas Lea walionesha umahiri mkubwa wa kuucheza
mchezo huo kwa kumiliki mpira na kuupiga kwa kutumia kichwa, mabega, miguu,
magoti na viungo vingine isipokuwa mikono.
Mchezo huu uliasisiwa mwaka 2013 na umewahi kuchezwa
na wanasoka maarufu Duniani kama akina Luis Figo na Ronaldihno Gaucho ambaye
pia ndiye Balozi wa mchezo huo.
No comments:
Post a Comment