CAIRO, Misri
MABINGWA wa Afrika wameanza kwa sare ya mabao 2-2 kutetea taji la
Ligi ya Mabingwa ugenini dhidi ya Saint George ya Ethiopia katika mchezo wa
kwanza wa hatua ya 32 bora.
Wakiwa chini ya kocha wao mpya Mfaransa Hubert Velud (pichani), Mazembe jana walijikuta
katika wakati mgumu dhidi ya wapinzani wao hao wa Ethiopia.
Hatahivyo, mabingwa hao watetezi wameondoka Ethiopia wakiwa na
faida ya mabao mawili ya ugenini kabla ya mchezo wa marudiano utakaofanyika
wikiendi ijayo jijini Lubumbashi, Kongo.
Saint George walipata bao la kuongoza katika dakika ya 11 wakati Assefa
Behaile alipowafanya wenyeji kuwa mbele kwa bao 1-0.
Mghana Daniel Nii Adjei aliisawazishia Mazembe, huku bao la
kujifunga la Isaac Isiende yaliwapatia mabingwa hao watetezi uongozi wa mabao
2-1 hadi kipindi cha pili.
Saint George waliongeza presha kwa wapinzani wao na kufanikiwa
kusawazisha kwa bao lililofungwa na Girma Adane na kufanya matokeo kuwa mabao 2-2.
Kwingineko katika mechi zilizofanyika Jumapili, kocha mpya wa Zamalek
Alex McLeish alifurahia ushindi wa timu yake wa bao 1-0 dhidi ya Union Douala nchini
Cameroon katika mchezo wake wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa wa Afrika.
Kocha huyo wazamani wa Scotland, McLeish amekuwa kocha wan ne wa Zamalek
msimu huu baada ya kocha Mreno, Mbrazil na Mmisri kutimuliwa katika timu hiyo.
Baada ya miaka kadhaa ya kupigania kutoshuka daraja England akiwa
na timu ya Birmingham City na majirani zao wa Aston Villa, McLeish yuko mbioni
kutwaa taji akiwa na Zamalek, ambayo imewahi kushinda taji la Afrika katika
vipindi vitano.
Zamalek ilianza vizuri jijini Douala huku beki wa Burkina Faso
Mohamed Koffi akifunga bao la ushindi katika dakika ya 59.
Jumamosi, Al Ahly, ambao ni majirani wa Zamalek walijikuta
wakitoka suluhu dhidi ya Recreativo Libolo nchini Angola. Kwa sasa Ahly inafundishwa
na Mholanzi Martin Jol –kocha
mwingine wa timu ya Ligi Kuu ya Uingereza.
Kwingineko, timu ya Nigeria ya Enyimba ilitawala mchezo wao wa
nyumba dhidi ya Vital'O ya Burundi, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 5-1
katika mchezo uliopigwa Port Harcourt.
No comments:
Post a Comment