Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) leo limefanya mkutano wake mkuu katika hoteli ya Regal Naivera jijini Tanga, huku mkuu wa Mkoa wa Tanga Mwantumu Mahiza akiwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mkutano huo utakaomalizika kesho kwa shughuli ya uwekaji jiwe la msingi katika eneo la kukuzia vipaji mjini humo.
Ifuatayo ni Hotuba ya Rais wa TFF, Jamal Malinzi
Ndugu Mweshimiwa mgeni rasmi, mh Mwantumu Mahiza Mkuu wa Mkoa wa
Tanga,
Ndugu wajumbe wenzangu wa Mkutano Mkuu
Ndugu wageni waalikwa.
Salam aleikum,
Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa ajili ya
aliyotujalia na kutufanikisha kuwepo hapa leo. Ni kwa Rehema zake Mwenyezi
Mungu tumeweza kujumuika hapa leo.
Ninaomba nichukue fursa hii kuwaomba wote tusimame ili kuwarehemu
waliotangulia mbele ya haki.
Ndugu zangu, kama mnavyofahamu tarehe 25/10/2015 nchi yetu
ilifanya Uchaguzi Mkuu. Nichukue fursa hii kumpongeza Rais wetu Mpendwa Dr John
Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wetu pamoja na Makamu wa Rais Mama
Samia Suluhu. Pongezi za pekee ni kwa Mh. Nape Nnauye kwa kuteuliwa kuwa Waziri
wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo na Mh Anastacia Wambura kuwa Naibu
Wake.
Pongezi za kipekee kwa wanafamilia ya mpira wa miguu Tanzania
ambao wamepata nyadhifa kama ifuatazo:
1. Mh. Majaliwa Kassim
Majaliwa, ameshinda nafasi ya ubunge wa jimbo la Ruangwa na pia kuteuliwa kuwa
Waziri Mkuu wa Tanzania.
2. Mstahiki Paschal Kihanga, Mwenyekiti wa Chama cha
Mpira wa Mkoa wa Morogoro, alishinda udiwani na pia amepata wadhifa wa Meya wa
Manispaa ya Morogoro.
3. Mh John Kadutu mjumbe wa
mkutano mkuu toka Mwanza, ameshinda
ubunge jimbo la Ulyankulu.
4. Mh. Maftah Nachuma
Katibu wa Chama cha Mpira wa miguu Lindi vijijini ameshinda nafasi ya ubunge
jimbo la Mtwara Mjini.
5. Mh. Leonard Kiganga Bugimala, Mwenyekiti klabu ya Geita Gold
Sport amechaguliwa kuwa Mwenyekiti Halmashauri ya mji wa Geita na Makamu wake
Mh. Costantian Mdindi pia amechaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa Halmashauri
hiyo.
6. Mh. Khalid Mohammed Abdallah Mjumbe wa Kamati ya Utendaji TFF ameshinda nafasi ya
udiwani.
7. Mh Yusuf Kitumbo Mwenyekiti chama cha mpira mkoa wa
Tabora, ameshinda udiwani.
8. Mh. Golden Sanga, Mwenyekiti chama cha mpira mkoa wa
Ruvuma, ameshinda udiwani.
9. Mh. Bartholmeo Kimario,
Mwenyekiti chama cha mpira mkoa wa Singida, ameshinda udiwani.
10. Mh. Omari Kinyento, mjumbe wa Mkutano Mkuu toka Singida
ameshinda udiwani.
11. Mh. Omar Gindi, Kaimu
Mwenyekiti wa Chama cha Mpira Mkoa Kigoma ameshinda Udiwani.
12. Mstahiki James Bwire,
Mshirika wa TFF, Mkurugenzi Alliance School kwa kuchaguliwa udiwani na umeya
jijini Mwanza.
Tunampongeza pia Makamu wa Rais wa TFF, Ndg Wallace Karia kwa
kupandishwa cheo na kuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba.
Ushindi huu ni heshima kubwa kwa familia ya mpira wa miguu
Tanzania na unaonyesha jinsi gani watanzania wanathamini na kuenzi mpira wa
miguu.
Viongozi wetu hawa tunawaombea mafanikio katika kutimiza majukumu
yao.
Ndugu wajumbe wenzangu wa Mkutano Mkuu, ninawapeni pole sana kwa
usumbufu uliotokana na kuahirishwa Mkutano wetu wa tarehe 19-20 Desemba mwaka
jana, hii ilitokana na sababu ambazo tulizieleza wakati huo. Ufumbuzi wa matatizo
yetu na mamlaka za kodi unaendelea kutafutwa. Ninawashukuru sana kwa kuitikia
wito wa Kamati yetu ya utendaji wa kuhudhuria mkutano mkuu huu muhimu ulioitishwa kwa mujibu wa Katiba
yetu.
Ninaomba nichukue fursa hii kutoa taarifa ya mambo muhimu ambayo
uongozi wetu umeyatekeleza kati ya kipindi tulichokutana mwezi Machi mwaka jana
mjini Morogoro hadi sasa. Kama nilivyotoa
rai kwenye mkutano wetu wa Morogoro, ninaomba tuyapitie, tuyajadili na
kuangalia wapi utekelezaji haukuwa mzuri ili changamoto hizo ziweze kufanyiwa
kazi. Azma yetu ni kuhakikisha mpira wa Tanzania unakua na sisi tunafikia lengo
la kutoa upinzani wa kutosha katika hatua za Kimataifa kuanzia ukanda wetu wa
CECAFA, Afrika na hatimae kung’ara duniani.
1. Timu ya Taifa (Taifa Stars)
Baada ya timu yetu ya Taifa
, Taifa Stars kutofanya vizuri katika michuano ya COSAFA huko Afrika Kusini
mwezi Mei mwaka jana na baadae kufanya vibaya katika mchezo wa kwanza katika mtoano wa mashindano
ya CHAN,Kamati ya Utendaji ya TFF
ilichukua maamuzi ya kusimamisha ajira ya kocha wa kigeni Martin Nooj na badala
yake kuingia mkataba na makocha wazawa Boniface Charles Mkwasa akisaidiana na
Hemed Morocco. Tangu walimu hawa wemechukua timu ya Taifa imeboreka na hadi
sasa tumefungwa mechi mbili tu za mashindano
dhidi ya Algeria na Malawi ugenini, tumetoka sare mbili nyumbani dhidi ya
Nigeria na Algeria na kuifunga Malawi nyumbani.
Aidha timu ya Kilimanjaro Stars chini ya kocha Abdalla Kibadeni na
msaidizi wake Juma Mgunda katika mashindano ya CECAFA Challenge katika mechi
nne ilizocheza Ethiopia haikufungwa hata mechi moja katika “Open Play” ingawa ilitolewa kwa penati tano
tano katika hatua ya nusu fainali. Kipindi chote ambacho tumekuwa na makocha
wazawa kiwango cha Tanzania FIFA kimekuwa kikipanda mara zote.
Tunawapongeza sana makocha wetu hawa na benchi la ufundi.
Kwa sasa tunajiandaa na mechi
za kufuzu kucheza fainali za Afrika AFCON 2017 nchini Gabon. Mechi hizi
ni dhidi ya Tchad tarehe 23/03/2015 ugenini Ndjadema na mechi ya marudiano Dar es Salaam tarehe 28/03/2015. Imani yetu
ni kuwa timu yetu itaendeleza wimbi la ushindi. Katika kujiandaa na mchezo wetu
dhidi ya Nigeria Taifa stars iliweka kambi nchini Uturuki na pia timu iliweka
kambi Afrika kusini kujiandaa na mechi dhidi ya Algeria. Kambi hizi zimesaidia
sana kuimarisha timu yetu kabla ya mechi hizi kubwa mbili.
2. Timu ya Taifa ya Wanawake Twiga Stars.
Timu yetu ya Taifa ya wanawake Twiga Stars chini ya kocha Rogasian
Kaijage ilifanikiwa kuitoa Zambia na
hivyo kufuzu kucheza fainali za michezo ya Afrika nchini Kongo Brazaville.
Katika fainali hizi Tanzania ilifungwa na Ivory Coast na Nigeria na kutoka sare
na Congo, hivyo kutolewa katika hatua za makundi. Uzoefu uliopatikana katika
mashindano hayo umempa fursa kocha mpya wa Timu ya Twiga stars Bi Nasra kuweza
kuunda kikosi kipya kichanga ambacho majuzi kilitoa changamoto kwa timu ya
Zimbabwe, imani yetu ni kwamba hii timu itafanya vizuri mechi ya marudiano
mjini Harare. Aidha timu ya Twiga stars ilipata mechi moja ya majaribio dhidi
ya Malawi.
3. Udhamini na Michuano Mipya.
Ninayo furaha kuwajulisha wajumbe wenzangu wa mkutano mkuu kuwa katika kipindi hiki
tumefanikiwa katika maeneo yafuatayo:
3.1 Kufufuliwa Kombe la Shirikisho.
Kwa kushirikiana na mdhamini Azam Sport Kombe la Shirikisho
limefufuliwa na kuboreshwa. Kwa mwaka
huu tumeanza na timu 64 ambazo ni za ligi Kuu (16), Ligi daraja la kwanza FDL (24) na
Ligi daraja pili SDL (24). Ili kupanua
uwigo wa ushiriki wa Mikoa kwa misimu ya
usoni timu mabingwa wa mikoa (RCL) nazo zitashirikishwa katika mashindano haya
ili kila mkoa wa Tanzania ushiriki katika mashindano haya. Kwa sasa mashindano
haya yako hatua ya robo fainali na yana ushindani mkubwa. Inatia moyo kuwa
mpaka hatua hii bado kuna timu moja ya ligi daraja la kwanza ya Geita Gold
ambayo bado inapambana. Bingwa wa Kombe hili atawakilisha Tanzania katika Kombe
la Shirikisho la Afrika.
3.2 Udhamini Ligi Daraja la Kwanza.
Tumefanikiwa kupata udhamini wawili kwa ligi daraja la kwanza FDL. Tumempata
STARSTIMES ambaye ndiye mdhamini mkuu wa ligi na pia kampuni za Television
ya Sahara Media kupitia STAR TV imepewa
haki za kuonyesha mechi hizi moja kwa moja. Haya ni mafanikio makubwa kwa ligi
ya Daraja la kwanza kwani pia soko la wachezaji hawa litapanuka kwa kuwa
wanaonekana moja kwa moja na pia itakuza
jina la ligi lenyewe. Changamoto ya vilabu kucheleweshewa malipo ya udhamini
tumeliona na tunalifuatilia kwa karibu kupata ufumbuzi ili lisitokee tena.
3.3 Mkataba wa Vodacom na
Ligi Kuu.
Kampuni ya Vodacom baada ya mzungumzo marefu tuliafikiana na
kusaini mkataba mwingine wa miaka mitatu wa udhamini wa Ligi Kuu wenye ongezeko la thamani ya udhamini kwa asilimia
40%. Jitihada zimefanyika kuvutia wadhamini wengine nao waje waongeze udhamini
kwa ligi kuu.
Tunashukuru mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NHIF umeitikia wito. Vilabu vya Ligi Kuu na ligi
Daraja la Kwanza navyo vimeongeza jitihada za kupata wadhamini, tunayashukuru
makampuni ya madini ya ACACIA (Stand
United)) na Geita Gold Mining (Geita Veterans) kwa kujitolea kusapoti mpira.
Tunazidi kutoa wito kwa makampuni mengine yajitokeze kutoa udhamini ikiwa ni
sehemu ya kutangaza biashara zao.
3.4 Udhamini Tarajiwa.
Tunatarajiwa kupata wadhamini kwa ajili ya Ligi Kuu ya vilabu vya
wanawake (Women Premier League) pamoja na ligi ya vilabu vya Ligi Luu ya vijana
chini ya umri miaka 20 (U20).
Jambo hili likifanikiwa matumaini yetu ni kuwa tutaanzisha ligi
mpya mbili, ya vilabu vya wanawake Women Premier League na ya vilabu vya Ligi
Kuu kwa vijana umri chini ya miaka 20. Hii itasaidia sana kuinua kiwango cha
mpira wetu kwa wanawake na wanaume.
4. Soka la Vijana.
4.1 Fainali za Afrika za vijana U17 mwaka 2017.
Kikosi chetu cha Taifa cha vijana chini ya umri wa miaka 17 (U17)
kinachojiandaa na hatua za mtoano mwezi juni, 2016 ilikuwa kifanye ziara ya
kimichezo kwenda Burundi, Rwanda, Uganda na Kenya. Lengo lilikuwa ni kukipatia
kikosi hiki uzoefu wa kimataifa. Wakati tayari kikosi kimejiandaa na
kukabidhiwa bendera, akaunti za TFF zilifungiwa na TRA na hivyo safari
kuvunjika kwa ukosefu wa fedha. Pamoja na changamoto hiyo mpango mkakati
umefanyika na sasa kikosi hiki kitacheza moja ya kirafiki ya kimataifa hapa
Tanzania mwezi April na baadae kwa hisani ya Chama cha Mpira cha India timu
itakwenda India kuweka kambi ya wiki tatu tayari kwa kuikabili Seychelles mwezi
Juni. Tunakishukuru Chama cha Mpira cha India pamoja na serikali ya India kwa
kutupatia sapoti hii.
4.2 Fainali za Afrika U17 mwaka 2019.
Maandalizi ya fainali hizi ambazo Tanzania itakuwa mwenyeji
yanaendelea vizuri na vikao na Wizara tayari vimeanza kwa ajili ya kufanya
maandalizi muhimu ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano hayo. Pia maandalizi
ya timu itakayoshiriki fainali hizi yameanza kwa vijana umri chini ya miaka 13
(U13) kujumuisha pamoja katika shule ya Alliance mjini Mwanza. Mwalimu Kim
Poulsen tumemleta mahsusi ili pamoja na majukumu mengine, atuandalie kikosi cha
ushindi cha vijana umri chini ya miaka 17 mwaka 2019. Imani yetu ni kuwa Tanzania tutafanikiwa
kuandaa mashindano mazuri mwaka 2019 na pia kunyakua kombe hili.
4.3 Mashindano ya Olimpiki Tokyo 2020
Tumedhamiria kushiriki fainali za Olimpiki Tokyo mwaka 2020. Ili
kufanikisha lengo hili zoezi la kuwapata vijana wenye umri stahiki (waliozaliwa
mwaka 1997 na kuendelea) limeanza. Chini ya uangalizi wa Kocha Poulsen
tunaamini tutaweza kujenga kikosi imara cha kufaulu kushiriki fainali hizi.
Kwa kuweza kujenga vikosi imara vya U17 mwaka huu na mwaka 2019 na
pia kuwa na timu nzuri ya Olimpiki Tokyo 2020 imani yetu ni kuwa hiki kizazi
tunachokijenga na kukikuza ifikapo mwaka
2026 kitaweza kutuvusha tucheza fainali za kombe la dunia inshallah.
4.4 Vituo vya mikoa vya
kukuza na kuendeleza vipaji.
Kama nilivyoainisha kwenye mkutano wa mwezi Machi mjini Morogoro,
azma ya TFF ni kuhakikisha kuwa kila
chama cha mpira wa miguu cha mkoa kinakuwa na kituo mama cha kukuza na kuendeleza
vipaji vya mpira. Mkataba wa mfano (template) umekwisha pelekwa mikoani ili
vyama vya mikoa kama havina vituo vyake basi viingie mkataba wa ushirikiano na
kituo kimoja kwa lengo la kukifanya kiwe kituo mama cha Mkoa. Kupita vituo hivi
TFF itaweza kuratibu shughuli za maendeleo ya mpira wa vijana katika mikoa yetu
na kuongeza nguvu kwa kuvipatia vifaa na
walimu.
Mipira 5000, koni 3000, na beeps 2000 tayari vimeagizwa toka nje
ya nchi kwa kutumia vyanzo vya fedha vya TFF yenyewe bila kuomba msaada kwa
ajili ya kuendeleza program hii. Tayari kila mkoa una mwalimu angalau mmoja
aliyefanya kozi ya FIFA ya ukocha
isipokuwa mikoa miwili tu Manyara na Njombe. Hivyo mtaji wa kutosha
tunao wa kuanzisha vituo hivi. Shime viongozi wenzangu wa mikoa tujidhatiti
tuweke nguvu katika uwanzilishaji na uendelezaji wa vituo hivi ambavyo vitakuwa
chachu kuu ya kutoa wachezaji wa Taifa wa kike na wa kiume.
Imani yetu ni kuwa vituo hivi vikiimarika vitakuwa ni chachu ya
kuendeleza vituo vingine ambavyo vitamilikiwa na vyama vya mpira vya wilaya,
vilabu, taasisi binafsi, mashule nk. Kwa utaratibu baadae tutaweza kuwa
tunaratibu mashindano kati ya vituo hivyo ngazi ya wilaya, mikoa, kanda na
hatimae Taifa ili tuweze kutafuta wachezaji bora wa kuimarisha timu zetu na hatimae
kuwa na timu za kuleta mafanikio Kimataifa kwa siku zijazo.
Tunashukuru tumeweza kupata ardhi yetu wenyewe katika mikoa ya
Tanga na Manyara. Ninarudia kutoa wito kwa viongozi wote wa mikoa tuzidi
kukamata ardhi mikoani kwetu ili hatimae tuweze kujenga vituo vya kukuza na
kuendeleza vipaji, centres of excellency.
5. Kozi mbali mbali.
Kwa kushirikiana na CAF na FIFA Shirikisho letu limeandaa kuratibu
na kutoa kozi mbali mbali za waamuzi na makocha katika ngazi mbali mbali.
Jitihada kubwa zimefanyika kuhakikisha mikoa iliyokuwa na hazina ndogo ya
makocha na waamuzi inapewa fursa ya kuratibu kozi hizi. Tunashukuru viongozi
wote wa mikoa na wilaya ambao tumeshirikiana nao kutimiza azma hii. Juhudi
zinaendelea ili tuweze kupata kupata makocha, waamuzi, madaktari wa michezo na
watawala bora na wengi zaidi. Ninatoa rai kwa wakinamama wazidi kujiunga katika
kozi hizi maana wana umuhimu wa kipekee katika maendeleo ya mpira hasa wa
wanawake.
6. Klabu.
Pamoja na jitihada za kutafuta wadhamini wa mashindano mbalimbali
yanayohusisha vilabu, jitihada pia zinaendelea kufanyika kuhakikisha vilabu vyetu
vinaimarisha utawala bora. Kufuatia CAF na FIFA kuanzisha utaratibu wa kutoa
leseni kwa vilabu (Club Licencing) jitihada sasa zinafanyika kuhakikisha vilabu
vinaelimishwa kwa kina juu ya mahitaji ya leseni hizi. Katika utaratibu wa
leseni za vilabu, vilabu vyetu sasa vitalazimika kuwa na ofisi, kuwaajiri watendaji wakiwemo makatibu na
watunza kumbukumbu za mahesabu, kuwa na maeneo ya kufanya mazoezi, kuwa na
program ya maendeleo ya mpira wa vijana, kuajiri walimu wenye sifa nk.
Tunaamini utaratibu wa leseni za vilabu ukitekelezwa ipasavyo uendeshaji wa
vilabu vyetu utaboreshwa na hivyo kuongeza tija kwa vilabu vyetu.
7. Kitega uchumi Karume.
Jitihada za kuendeleza kiwanja chetu uwanja wa Karume, kama
tulivyoahidi, zinaendelea. Tayari tumekwisha malizia kujenga chumba ambacho
kitakuwa ni duka la TFF la kuuzia vifaa vya michezo na pia ujenzi wa chumba
kingine utakapowekwa mgahawa unaendelea. Kwa sasa tunashugulikia kupata mashine
ya TRA ya tozo ya kodi (EFD machine) ili tuweze kufungua duka letu la vifaa vya
michezo.
8. Tiketi za Elektroniki.
Kutokana na matatizo yaliyojitokeza matumzi ya tiketi ya
elektronik yalisimamishwa na mmiliki wa uwanja wa Taifa ambaye ni Serikali.
Baada ya mazungumzo na mwenye mkataba
ambaye ni Benki ya CRDB ilikubaliwa apatikane mshauri mtaalam wa kupitia
mfumo mzima na kupendekeza marekebisho. Baada ya tenda kutangazwa mtaalam
amepatikana na sasa anasubiriwa aanze kazi hiyo. Lengo ni kuhakikisha utaratibu
wa tiketi za elektronik unaanza kutumika msimu ujao wa ligi.
9. Mfuko wa maendeleo ya
mpira (Football Development Fund).
Baada ya mfuko huu kuanzishwa kikatiba katika mkutano mkuu
uliopita, kamati ya utendaji ya TFF iliteua wajumbe wa kamisheni ya uendeshaji
wa mfuko huu chini ya mwenyekiti Ndugu
Tido Mhando. Lengo la mfuko huu kama ilivyoanishwa ni kuwa chanzo kikuu cha
kupata rasilimali kwa ajili ya maendeleo ya mpira wa miguu nchini mwetu. Ninaomba tuwaunge mkono
na kuwapa ushirikiano watendaji wa mfuko huu huku tukitambua kuwa maendeleo ya
mpira wa miguu yanahitaji rasilimali nyingi.
PONGEZI MAALUM
Ninaomba nichukue fursa hii kumpongeza tena Bwana Gianni Infantino
kwa kuchaguliwa kuwa Rais mpya wa FIFA. TFF tulishiriki kikamilifu katika
mchakato mzima wa uchaguzi huu. Tunaamini chini ya uongozi wake mabadiliko makubwa
chanya yatatelezwa katika mpira wetu.
Aidha nirudie tena kumpongeza kijana wetu Mbwana Samatta kwa
kuteuliwa kuwa mwanamichezo bora wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ndani ya
bara letu na pia kwa kufanikiwa kupata fursa ya kucheza katika ligi kuu ya
Ubelgiji. Tunazidi kumuombea na kumtakia mafanikio.
Ndugu wajumbe wa Mkutano Mkuu baada ya kuyasema haya ninaomba
nirudie kuwashukuru wote kwa kuhudhuria kwenu mkutano huu, ninaomba Mola
aubariki Mkutano wetu ili tutakayojadili na kukubaliana yawe ni ya kheri na
yajenge mpira wetu.
Ahsanteni sana.
Jamal Malinzi
Rais wa TFF
Tanga
No comments:
Post a Comment