Nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mbwana Samatta akiwa mazoezini kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. |
Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Taifa ya Chad ‘Les Sao’ imejiondoa katika michuano ya
kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika (AFCON) itakayofanyika mwaka 2017
nchini Gabon.
Kujitoa ghafla kwa Chad kumeliingizia hasara ya kiasi cha sh. milioni 200 Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa ajili ya maandalizi mbalimbali.
Taarifa ya kujitoa kwa Chad ilitolewa na Shirikisho la Mpira wa
Miguu barani Afrika (CAF) jana baada ya Les Sao kuandika barua ya kujitoka
katika mashindano hayo ikiwa katika kundi G pamoja na timu za Tanzania, Nigeria
na Misri.
Chad ilitarajiwa kucheza leo dhidi ya Taifa Stars katika Uwanja wa
Taifa Dar es Salaam, ikiwa ni mchezo wa marudiano wa kundi G baada ya kucheza
mchezo wa awali jijini N’Djamena
katikati ya wiki iliyopita.
Katika mchezo wa awali uliochezwa Uwanja wa Idriss Mahamat Ouya,
Taifa Stars iliibuka na ushindi wa bao 1- 0 , bao lililofungwa na nahodha,
Mbwana Samatta dakika ya 30 ya mchezo.
Kufuatia kujitoa kwa Chad, matokeo ya michezo yote iliyoihusisha
timu hiyo yanafutwa, na msimamo wa Kundi G kwa sasa unaongozwa na Misri yenye
pointi nne, Nigeria pointi mbili na Tanzania pointi moja.
Awali, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli aliitakia heri timu ya Taifa
yaTanzania (Taifa Stars) ambayo leo ingecheza na Chad.
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu, Gerson Msigwa alisema
katika taarifa yake ya jana kuwa, Rais Magufuli aliwataka wachezaji, benchi la
ufundi na viongozi wa TFF kutambua kuwa Watanzania wana matumaini makubwa kuwa
timu yao itafanya vizuri katika mchezo huo.
Endapo Stars ingecheza na kushinda jana, basi ingefikisha pointi
saba na kuipita Nigeria na kama ingeshinda kwa mabao mengi, ingeweza kushikilia
kwa muda uongozi wa kundi hilo.
Hata hivyo kujitoa kwa Chadi kumekuwa pigo kwa Stars kwa kuwa sasa
inabaki kuwa ya tatu.
Awali, msemaji wa TFF, Baraka Kizuguto alisema hawakuwa na taarifa
zozote za kuwasili kwa Chad na wala hawakuwa na taarifa kama timu hiyo
imeshindwa kuja nchini kutokana na ukata kama baadhi ya watu walivyodai.
“Hadi sasa
hatuna taarifa zao na hatujapata taarifa kama Chad wamejitoa kwa sababu ya
ukata, ebu muulize vizuri aliyekupa taarifa hizo, “alisema Kizuguto jana mchana.
Licha ya Chad, kujitoa lakini kocha wa Stars Boniface Mkwasa,
alisema kikosi chake kilikuwa tayari kwa ajili ya mchezo huo wa leo na lengo
lao kubwa ni kuendeleza ushindi walioupata ugenini Chad Jumatano iliyopita.
Kocha huyo alisema awali walikuwa na majeruhi wawili beki Kelvin
Yondani na kiungo Mwinyi Kazimoto, lakini juzi walianza mazoezi hivyo
angewatumia sambamba na mshambuliaji Abdillah Yusuf, aliyejiunga kwa mara ya
kwanza na timu hiyo akitokea klabu ya daraja la pili ya Mansfield ya England.
Rais wa TFF, Jamal Malinzi alikuwa amemtangaza Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa kuwa mgeni rasmi katika pambano
hilo .
No comments:
Post a Comment