Na Mwandishi Wetu
KLABU za mbio za pole pole `jogging’ wilayani Temeke zimemkaribisha rasmi Mkuu mpya wa Mkoa wa
Dar es Salaam Paul Makonda na kumtaka awasaidie kujikwamua kiuchumi.
Makonda akizungumza katika hafla
hiyo alizitaka klabu hizo za jogging wilayani Temeke kuwatimua viongozi
wasioeleweka, ambao wamekuwa wakichelewesha maendeleo yao.
Hafla hiyo ya kumkaribisha
Mkuu mpya wa Mkoa wa Dar es Salaam ilifanyika kwenye Viwanja vya
Buliyaga Temeke.
Alisema kuwa hataki kuona
viongozi wa klabu za jogging kazi yao kubwa
kupita kwa wanasiasa kuomba pesa kutumia
majina ya vijana.
Alisema kuwa kiongozi kama huyo atakuwa
anawachelewesha katika mipango yao ya maendeleo, “hivyo msimvumilie na badala yake mumuondoe haraka.”
Aidha, Makonda alisema kuwa
vijana wengi hawataki kufanya safari ya mapambano na hivyo kushindwa
kufanikiwa kwani hawana nidhamu, hawana bidii na wala hawamuweki Mungu mbele.
Alisema kuwa yuko tayari kuwasaidia vijana wa Temeke ili waweze kuondokana na
umasikini, mradi tu wakubali kufanya kazi kwa bidii, nidhamu na kumuweka Mungu
mbele.
Makonda alisema kuwa Aprili 10 atakutana na vijana wote wa jogging
mkoa wa Dar es Salaam pamoja na
wanamichezo wote na wasanii ili kuzungumzia fursa za kujikwamua kiuchumi.
Pia Makonda alisema kuwa atatoa Sh
milioni 2 kwa kikundi cha jogging ambacho kitakuwa na mipango mizuri ya
kujikwamua kiuchumi.
Naye msanii maarufu wa mashairi nchini, Mrisho Mpoto ambaye ndiye
mratibu wa hafla hiyo alisema kuwa anguko la vijana wa Temeke liko mikononi mwa
Makonda, ambapo alimtaka kuhakikisha vijana hao wanajikwamua katika umasikini.
Alisema kuwa chini ya Makonda wanataka kuiona kesho mpya ya
Temeke, ambayo itatoa fursa kwa vijana kujikwamua kiuchumi tofauti na zamani.
Jumla ya klabu 66 za jogging kutoka wilaya ya Temeke vikiwa na
jumla ya washiriki 2,000 walishiriki katika hafla hiyo, ambapo walianza kwa
kukimbia na Makonda kwa kilomita saba kuanzia Uwanja wa Taifa hadi Viwanja vya
Buliaga Temeke.
Msanii mahiri wa mashairi, Mrisho Mpoto (kulia) akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kabla ya kuanza mbio za pole `Jogging' zilizoanzia Uwanja wa Taifa hadi Temeke. |
No comments:
Post a Comment