CAIRO, Misri
GUINEA ya Ikweta ambao mwaka jana walikuwa wenyeji wa fainali za
Mataifa ya Afrika (Afcon), wamekuwa wa kwanza kutupwa nje ya mbio za kufuzu kwa
fainali zile za Gabon 2017.
Timu hiyo imetupwa nje baada ya kupokea kichapo cha bao 1-0 kutoka
kwa Mali.
Mustapha Yatabare ndiye aliyekuwa shujaa wa Mali baada ya
kupachika bao katika dakika ya 89 katika mchezo uliofanyika Malabo na kuifanya
timu yake kushika uongozi wa Kundi C, ikiwa pointi mbili juu ya Benin.
Guinea ya Ikweta, ambayo ilitinga nusu fainali ilipoandaa
masindano hayo mwaka 2015, sasa wanashika mkia katika kundi lake hilo ikiwa na
pointi moja huku zikiwa zimebaki mechi mbili kabla ya kumalizika mbio hizo za
makundi.
Sudan Kusini ni ya tatu, wakiwa na pointi tatu, na wamebaki na
nafasi finyu ya kufuzu kama moja ya timu bora zilizoshika nafasi ya pili.
Kwingineko, Zimbabwe iliisambaratisha Swaziland kwa mabao 4-0 katika
mchezo wa kufuzu kwa fainali hizo kutoka katika Kundi L.
Wenyeji, walioambulia sare ya bao 1-1 na Swaziland katika mchezo
wa Ijumaa, walitawala mchezo huo wa marudiano uliofanyika jijini Harare,
Zimbabwe na kushika uongozi wa kundi wakiwa pointi tatu zaidi ya timu iliyopo
katika nafasi ya pili.
Knowledge Musona ndiye aliyekuwa wa kwanza kufunga bao katika
dakika ya 53 kwa penalti huku Costa Nhamoinesu akiifanya timu hiyo kuwa mbele
kwa mabao 2-0 dakika sita baadae.
Evans Rusike aliongeza ushindi huo wa Zimbabwe huku Khama Billiat akikamilisha
ushindi huo baada ya kufunga bao la nne.
Musona aliiambia BBC Sport: "Najisikia furaha sana. Timu
yangu imekusanya pointi zote tatu nyumbani, sasa tunaongoza kundi letu na sasa
tuna nafasi kubwa ya kufuzu.
“Ni muhimu kuondoka na pointi
zote tatu kutoka katika mchezo wetu uhao nyumbani (dhidi ya Malawi
utakaofanyika Juni 3).
”
Swaziland wanabaki wakiwa na pointi zao tano, tatu juu ya Malawi
na Guinea ambao walitarajia kucheza jana.
Kila mshindi wa kundi na timu mbili zilizoshika nafasi bora za
pili zitafuzu kwa fainali zijazo za Mataifa ya Afrika zitakazopigwa Gabon.
Katika Kundi B Jamhuri ya Afrika ya Kati ikiwa nyuma kwa bao moja,
iliibuka na kuifunga Madagascar kwa mabao 2-1.
Faneva Andriatsima alikuwa wa kwanza kuwafungia wageni bao katika
dakika ya 35 na kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao 1-0.
Lakini mabao mawili yaliyofungwa ndani ya dakika 12, ambayo
yalifungwa na Salif Keita katika dakika ya 53 na baadae Limane Moussa alipachika
la ushindi.
Matokeo hayo yanaiweka Afrika ya Kati kileleni mwa msimamo wa
kundi lao wakiwazidi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa pointi moja.
Libya walipata pointi za kwanza katika Kundi F baada ya kushinda
mabao 4-0 dhidi ya Sao Tome e Principe.
Katika mchezo uliopigwa Misri kutokana na sabbau za kiusalama, Mohamed
Zubya wa Libya alifunga hat-trick katika kipindi cha pili.
No comments:
Post a Comment