Na Mwandishi Wetu
MSHAMBULIAJI mpya wa Free State Stars ya Afrika Kusini, Mrisho Ngassa
ni miongoni mwa wachezaji wanaowania tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara 2014/2015.
Mchezaji mwingine ni mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu
uliomalizika hivi karibuni, Simon Msuva pamoja na mchezaji wa Simba Mohamed
Hussein au ‘Tshabalala’.
Ngassa na Msuva wote walikuwemo kwenye kikosi cha Yanga SC
kilichotwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu uliomalizika Mei mwaka huu.
Ngassa alisaini mkataba wa miaka minne na Free State Stars Mei
mwaka huu kama mchezaji huru, baada ya kumaliza mkataba wake Yanga SC.
Watatu hao, mmoja wao leo atatajwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu
katika taafrija itakayofanyika ukumbi wa JB Belmonte (Kilimanjaro) uliopo
katika jengo la Golden Jubilee Tower (PSPF), mtaa wa Ohio, Dar es Salaam
kuanzia saa 12:00 jioni.
Kipa chipukizi, Mohamed Yusuph wa Tanzania Prisons atachuana na
Said Mohamed wa Mtibwa Sugar na Shaaban Kado wa Coastal Union kuwania tuzo ya
kipa bora.
Aliyekuwa Kocha wa Simba SC, Mserbia Goran Kopunovic atachuana na
Mholanzi Hans Van Der Pluijm wa Yanga SC na Mbwana Makata aliyekuwa Prisons
kuwania tuzo ya kocha bora wa ligi hiyo.
Israel Nkongo atachuana na Jonesia Rukyaa na Samuel Mpenzu kuwania
tuzo ya Refa Bora, wakati Mgambo JKT, Mtibwa Sugar na Simba SC zitagombea tuzo
ya timu yenye Nidhamu.
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kwa kushirikiana na wadhamini wa
Ligi Kuu, Vodacom wanatarajia kutoa zawadi kwa washindi wa ligi hiyo kesho JB
Belmonte.
Mgeni rasmi katika halfa hiyo ya utoaji zawadi kwa wachezaji, makocha,
na timu washindi atakua ni Juma Nkamia, Naibu Waziri wa Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo.
Pamoja na tuzo binafsi, Vodacom ambao ni wadhamini wa Ligi Kuu
tangu mwaka 2002, watatoa zawadi kwa bingwa, mshindi wa pili, mshindi wa tatu
na mshindi wa nne.
WANAOWANIA
TUZO ZA LIGI KUU 2014/2015
Mchezaji
Bora; Mohamed Hussein (Simba SC), Mrisho Ngassa (Yanga SC), Simon Msuva
(Yanga SC).
Kipa Bora; Mohamed
Yusuph (Tanzania Prisons), Said Mohamed (Mtibwa Sugar) na Shaaban Kado (Coastal
union).
Kocha Bora; Goran
Kopunovic (Simba SC), Hans Van Der Pluijm (Yanga SC na Mbwana Makata (Tanzania
Prisons)
Refa Bora; Israel
Nkongo, Jonesia Rukyaa na Samuel Mpenzu.
Timu yenye Nidhamu; Mgambo JKT, Mtibwa Sugar na Simba SC.
No comments:
Post a Comment