Kocha Mkuu mpya wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo. Kulia ni msaidizi wake, Hemed Morocco. |
Na Seba Nyanga
KOCHA wa timu ya Soka ya
Taifa, Taifa Stars, Charles
Mkwasa amesema watajitahidi kufanya vizuri katika mchezo wa marudiano
kufuzu kwa fainali ya Afrika kwa
wachezaji wa ndani (Chan) dhidi Uganda,
huku akisisitiza kuwa mashabiki wasitarajie miujiza.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mkwasa alisema kwa muda
mfupi waliokabidhiwa timu, hawataweza kufanya mabadiliko makubwa, lakini
watajitahidi kwa uwezo wao kuleta matumaini mapya.
Aidha, Mkwassa amefanya mabadiliko kwenye timu ya taifa pamoja na
benchi la ufundi, ambapo mbali na kuita wachezaji 26, amemteua kocha wa zamani
wa timu hiyo, Abdallah Kibadeni kuwa mshauri wa timu.
Katika timu yake Mkwasa amewapumzisha wachezaji saba waliotumika
kwa muda mrefu na kuwaita watatu wapya ambao hawakuwahi kuitwa kwenye timu
iliyopita.
Mkwasa aliteuliwa juzi kuwa kocha
mpya wa timu ya taifa ya Tanzania, akirithi mikoba ya Mholanzi Mart Nooij aliyefukuzwa mwishoni mwa wiki
kufuatia kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Uganda katika mchezo wa Chan.
Alisema wachezaji walioteuliwa wanatakiwa kuhakikisha kuwa
wanajitunza na kujiheshimu ndani na nje ya uwanja, huku akisema atashirikiana na benchi jipya la ufundi
kujenga timu imara bila upendeleo.
Wachezaji waliowekwa kando ni pamoja na Amri Kiemba, Deogratias Munishi, Salim Mbonde, Erasto Nyoni, Kevin Friday,
Oscar Joshua na Hassan Dilunga.
Sura mpya ambazo hazikuwahi kuitwa ni Mudathir Khamis (KMKM),
Michael Aidan(Ruvu Shooting) na Ame Ally (Mtibwa Sugar).
Walioitwa kwa jumla ni Mohamed Hussein ‘Tshabalala’(Simba) ,
Deus Kaseke (Mbeya City), Ramadhan Singano (Simba), Mwadini Ally (Azam), Shomari Kapombe (Azam),
Nadir Haroub “Cannavaro” (Yanga), Kelvin Yondani (Yanga), na
Hassan Isihaka (Simba).
Wengine ni Aggrey Morris
(Azam), Jonas Mkude (Simba), Abdi Banda
(Simba), Salum Telela (Yanga), Frank Domayo (Azam), Saimon Msuva (Yanga), Said
Ndemla (Simba), Atupele Green (Kagera Sugar), Rashid Mandawa (Kagera) Ramadhan
Singano “Messi” (Simba). John Bocco (Azam), Sugar)
na Ame Ally (Mtibwa Sugar),
Wachezaji wa akiba ni Juma Abdul (Yanga), Mudathir Yahya (Azam) na
Samwel Kamuntu (JKT Ruvu).
Wachezaji hao wote watazungumza na makocha kesho kwenye hoteli ya
Tansoma na keshokutwa wataanza mazoezi rasmi kwenye uwanja wa Boko Veteran kujiandaa
na mchezo wa marudiano dhidi ya Uganda.
Katika hatua nyingine, Mkwasa
alitangaza benchi la ufundi la Taifa Stars chini ya usaidizi wa Hemed Morocco
wakati kocha wa makipa ni Peter Manyika, mshauri wa timu Abdallah Kibadeni,
mtunza vifaa Hussein Swedi Gaga huku mratibu wa timu akiwa ni Alhaj Ahemd Mgoyi
na meneja wa timu ni Juma Mgunda.
Alisema kamati ya tiba ya TFF
itapendekeza majina ya daktari wa timu na mchua misuli watakaoungana na kambi
ya Taifa Stars.
No comments:
Post a Comment