Na Mwandishi Wetu Zanzibar
KAMATI ya Utendaji ya Shirikishi la Soka Tanzania (TFF) imemtimua kocha
wa Taifa Stars, Mholanzi, Mart Nooij na habari zinasema, kocha msaidizi wa
Yanga SC, Charles Boniface Mkwasa atashika timu kwa muda, akisaidiwa na
Suleiman Matola wa Simba SC.
Kamati ya Utendaji ya TFF ililazimika kufanya kikao cha dharula
baada ya Stars kufungwa mabao 3-0 na Uganda usiku wa jana kwenye Uwanja wa
Amaan, Zanzibar katika mchezo wa kwanza raundi ya kwanza kufuzu CHAN 2016.
“Katika kikao cha leo (jana), pamoja na mambo mengine ilipitia mwenendo
wa Timu ya Taifa (Taifa Stars) ikiwa ni pamoja na kuhudhuria mchezo kati ya
Tanzania na Uganda, kama sehemu ya tathmini ya mwenendo wa timu,”imesema
taarifa ya TFF.
“Kamati ya utendaji kwa kauli moja imeamua yafuatayo: 1.Ajira ya
Kocha
Mkuu Maart Nooij inasitishwa mara moja kuanzia
tarehe 21/June/2015.
2. Benchi lote la ufundi la Taifa Stars limevunjwa kuanzia tarehe
21/06/2015.
3.Uongozi wa TFF utatangaza punde benchi jipya la ufundi la timu
ya Taifa,”imemalizia taarifa hiyo fupi iluyitolewa na Mkuu wa Idara ya
Habari na Mawasiliano ya TFF, Baraka Kizuguto.
Lakini mara baada ya mchezo huo, Nooij alisema hawezi kuondoka kwa
matokeo ya uwanjani, kwa sababu ana mkataba hadi mwaka 2016.
TFF italazimika kumlipa Nooij dola za Kimarekani zisizopungua 125,
000 (Sh. Milioni 250,000) kwa kumvunjia mkataba, ambao ni mishahara yake ya
miezi 10, kwa sababu kwa mwezi alikuwa analipwa dola 12,500 (Sh. Milioni 25).
Mabao mawili ya mshambuliaji Erisa Sekisambu na lingine la Farouk
Miya yanahitimisha historia ya kocha huyo Mholanzi Tanzania.
Habari za ndani zinasema Mkwasa na kocha Msaidizi wa Simba SC,
Suleiman Matola watapewa timu kwa muda- mtihani wao wa kwanza ukiwa ni kujaribu
kushinda mabao 4-0 ugenini wiki mbili zijazo ili kusonga mbele CHAN.
Matokeo ya jana yamewakosesha wachezaji wa Taifa Stars donge nono
la Sh. Milioni 1 kila mmoja ahadi iliyotolewa na Rais wa TFF, Jamal Malinzi.
Mchezo wa leo unakuwa wa tano mfululizo, Taifa Stars inafungwa
chini ya Nooij aliyerithi mikoba ya Mdenmark Kim Poulsen Aprili mwaka jana na
kwa ujumla timu hiyo imecheza mechi tisa bila ya ushindi chini ya Mholanzi
huyo.
Kwa ujumla, Nooij ameiongoza Stars katka mechi 18 tangu arithi
mikoba ya Mdenmark, Kim Poulsen Aprili mwaka jana, kati ya hizo ameshinda tatu tu,
sare sita na kufungwa tisa- akifunga mabao 17 na kufungwa 28.
No comments:
Post a Comment