*Aondolewa chini ya ulinzi mkali wa polisi akihofia kupigwa
Na Mwandishi Wetu Zanzibar
SAFARI ya Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars
imeiva baada ya leo usiku timu yake kupokea kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa
majirani zao wa Uganda katika mchezo wa kufuzu kwa fainali za Chan 2016.
Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za nyumbani
(Chan), zitafanyika mwakani nchini Rwanda na Tanzania imecheza na Uganda `The
Cranes’ kujaribu
kusaka nafasi hiyo katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Amaan mjini
Zanzibar.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilimpa kocha Mart Nooij
mtihani wa mwisho na endapo atashindwa kuipeleka Taifa Stars, basi atafute njia
ya kuondoka baada ya wapenzi wa soka nchini kuchoshwa na ipigo ya timu hiyo.
Wiki iliyopita, Taifa Stars ilipokea kichapo cha idadi kama hiyo
cha mabao kutoka kwa Misri katika mchezo wa kufuzu kwa fainali za Mataifa ya
Afrika (Afcon) zitakazofanyika mwaka 2017 nchini Gabon.
Hakuna ubishi kuwa baada ya kichapo hicho cha leo kocha huyo
Mholanzi atajiongeza kabla TFF haijamuonesha njia ya kutokea baada ya mchezo wa
pili utakaofanyika Kampala Uganda wiki mbili zijazo.
Mwaka jana Tanzania ilifungwa 1-0 na Uganda katika mchezo kama huo
wa Chan uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa kabla ya kutolewa na kuiacha The
Cranes ikisonga mbele.
Mabao ya The Cranes katika mchezo huo ulioanza saa 2;30 usiku ili
kuwawezesha wapenzi wa soka kufuturu ndio waende uwanjani yalifungwa na
Sekisambo Erisa mabao mawili na Miya Farouk.
Kabla ya kuanza mchezo huo, Taifa Stars ilipata pigo baada ya mchezaji
wake Oscar Joshua kuugua gafla na kuukosa mchezo huo.
Kwa mara ya mwisho Stars ilifuzu kwa fainali hizo za Chan mwaka
2009 zilipofanyika kwa mara ya kwanza nchini Iory Coast na ilitolewa katika
hatua ya makundi ikiwa chini ya Mbrazil Marcio Maximo.
Wakati huohuo kocha wa timu hiyo ilibidi asindikizwe na polisi mara baada ya filimbi ya mwisho ili kumzuia asipate kichapo kutoka kwa mashabiki wenye hasira waliotaka kumpifa.
No comments:
Post a Comment