Na Mwandishi Wetu
WANARIADHA wa Tanzania wameng'ara katika mbio za
Nagai Marathon Japan baada ya kutwaa nafasi za juu.
Mtanzania Marco Joseph wa Talent Athletics Club ya
Arusha aliweza kuibuka mshindi kwa upande wa wanaume kilomita 42 akitumia saa
2:21:13 akifuatiwa na Wilbardo Peter wa klabu ya Polisi kwa kutumia saa
2:32:12.
Tanzania pia iling'ara kwa upande wa wanawake km 42
baada ya Angelina John Yumba wa Talent Athletics Club aliyeshinda akitumia saa
2:43:21 muda ambao ni wa kufuzu kushiriki mashindano ya dunia yatakayofanyika
Doha Qatar mwakani.
Moto wa watanzania haukuishia hapo tu kwani kwenye
nusu marathon km 21 wanaume
Fabiano Nelson Sulle wa klabu ya Polisi alishinda kwa
saa 1:02:53.
Kwa upande wa wanawake km 21 moto ulizidi baada ya
nafasi zote nne za mbele kubebwa na watanzania ambapo Amina Mohamed Mgoo
alishinda akitumia saa 1:16:08 akifuatiwa na Rozalia Fabian Duye 1:18:57 (wote
wakitokea klabu ya JKT).
Sylivia Masatu wa Maranatha Athletics Club ya Arusha
alishika nafasi ya tatu kwa muda wa saa 1:32:52 huku Neema Paulo wa Talent
Athletics Club akishika nafasi ya nne kwa muda wa saa 1:41:36.
Timu hiyo ya Tanzania inatarajiwa kurejea nchini
Oktoba 24 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment