Na Mwandishi Wetu
KING’AMUZI cha DStv kitaonesha mpambano mkali wa
kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kati ya timu ya
Tanzania, Taifa Stars itakayocheza leo dhidi ya Cape Verde.
Mchezo huo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa wa
Capo Verde au Praia, utaanza kuanzia saa 2:00 Usiku na DStv watakuwa mubashara
kuonesha kipute hicho muhimu.
Watanzania wataweza kufuatilia mpambano huo kupitia
DStv na kushuhudia nyota wao kama akina Mbwana Samatta anayeichezea timu ya
Ubelgiji ya KRC Genk, Farid Mussa, Shaaban Idd Chilunda na Simon Msuva.
Tayari kikosi cha Stars kimeshawasili visiwani humo
tangu juzi Jumatano kikiwa na ari kubwa ya kupambana na kupata ushindi katika
mchezo huo, ambao ni muhimu ili kuweka matumaini ya kufuzu fainali hizo, ambazo
Tanzania ilifuzu kwa mara ya mwisho mwaka 1980 zilipofanyika Lagos, Nigeria.
Msimamo wa kundi lao la unaonesha Uganda ndio vinara
wakiwa na pointi nne, Lesotho ya pili wakiwa na pointi mbili sawa na Stars, lakini
wanatofautiana kwa mabao ya kufunga, wanaoburuza mkia ni Cape Verde wanye
pointi moja.
Stars itaingia kwenye mchezo huo huku ikijua wazi
kuwa na deni kubwa kwa Watanzania baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupewa
sapoti kubwa na Serikali katika maandalizi ya mchezo huo ikiwemo kuandaliwa
ndege maalum ya kwenda na kurudi.
Rekodi zinaonesha kuwa timu hizi zimekutana mara
mbili mwaka 2008 katika harakati za kufuzu Kombe la Dunia, ambapo Oktoba 11
Stars wakiwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam waliiibuka na ushindi wa 3-1
kwa mabao ya Athuman Iddy, Jerson Tegete na Mrisho Ngassa, waliporudiana Cape
Verde walishinda 1-0.
Kocha wa kikosi cha Stars kinachoongozwa na nahodha
Mbwana Samatta, Emmanuel Amunike amesema kuwa kikosi chake kipo kwenye hali
nzuri na kimejipanga kuwapa furaha Watanzania.
Amesema benchi la ufundi, wachezaji na kila kitu kiko
tayari kwa ajili ya mchezo huo, ambao utawawezesha Watanzania kufurahi kutokana
na matokeo mazuri watakayopata.
Timu mbili za kwanza kutoka katika kila kundi ndizo
zitafuzu kwa fainali hizo, ambazo zitafanyika mwakani nchini Cameroon.
No comments:
Post a Comment