Wednesday, 14 October 2015

Brazil yaifunga Venezuela katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia kwa Amerika ya Kusini



BRASILIA, Brazil
WINGA mahiri wa Chelsea, William ambaye jina lake halisi ni Willian Borges da Silva, juzi alikuwa shujaa wa Brazil baada ya kuifungia mabao mawili katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Venezuela  katika mchezo wa kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018, Kanda ya Amerika Kusini.

Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Castelao huko Fortaleza na ambao Brazil iliingia uwanjani ikiwa na hasira za kupigwa 2-0 na Chile wiki iliyopita, William alifunga bao la kwanza katika sekunde ya 40 kabla ya kupachika jingine muda mfupi kabla ya mapumziko.

Ilicheza bila ya nyota wake anayeichezea Barcelona ya Hispania, Neymar anayetumikia adhabu ya kufungiwa.

Venezuela ilipata bao lake la kufutia machozi katika dakika ya 64 wakati Christian Santos alipoujaza mpira wavuni kwa mchomo wa kona lakini mshambuliaji Ricardo Oliveira aliifungia Brazil bao la dakika tisa baadae.

Ni muda wa kocha Dunga kuipatia ushindi Brazil kabla ya mchezo wao ujao utakaofanyika Buenos Aires dhidi ya mahasimu wao Argentina, ambao bado hawajafunga katika mechi mbili.

Timu hiyo iliyocheza fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2014 walifungwa 2-0 na Ecuador katika mchezo wao wa kwanza na baadaye Jumanne ilitoka suluhu na Paraguay.

Dunga atakuwa na uwezo wa kumuita Neymar kwa ajili ya mchezo huo baada ya kumaliza kifungo chake alichokipata katika mashindano ya Copa America, wakati Argentina wanatarajia Lionel Messi kupona kutoka katika maumivu yaliyomweka kando katika mechi mbili za kufuzu.

No comments:

Post a Comment