Aliyekuwa Mbunge wa Ludewa, deo Filikunjombe katika moja ya mikutano yake ya kampeni. |
Na Waandishi Wetu
MGOMBEA ubunge wa CCM katika
Jimbo la Ludewa mkoani
Njombe, Deo Filikunjombe
amekufa katika ajali ya helikopta iliyotokea mkoani Morogoro juzi.
Kwa mujibu wa gazeti la Habari Leo la leo Jumamosi, mbali na Filikunjombe, ajali
hiyo pia imesababisha kifo cha Kapteni wake, William Silaa, ambaye ni baba wa
mgombea ubunge wa Ukonga kupitia CCM, Jerry Silaa na abiria wengine wawili
ambao hawajatambulika.
Uthibitisho wa vifo hivyo
umetolewa jana alasiri na Kamishina wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la
Polisi, Paul Chagonja, ambaye alikwenda katika eneo la tukio ambako
walifanikiwa kutambua mwili wa Filikunjombe na Kapteni Silaa.
*Taarifa za awali
Taarifa kuhusu utata wa ajali
ya helikopta hiyo, zilisikika kuanzia juzi saa tatu usiku na kusambaa kwa kasi
katika mitandao ya simu kuanzia jana asubuhi.
Kwa mujibu wa taarifa za juzi,
helikopta hiyo ilikuwa imepoteza mawasiliano ndani ya Hifadhi ya Taifa ya
Selou, ambayo ndiyo hifadhi ya wanyama iliyo kubwa kuliko zote duniani.
Hata hivyo, taarifa za jana
asubuhi zilieleza kuwa helikopta hiyo, huenda ilipata ajali na kuwaka moto,
lakini hakukuwa na taarifa sahihi kuhusu majaliwa ya abiria.
Miongoni mwa waliothibitisha
ajali hiyo, alikuwa Jerry ambaye pia ni
Meya wa Ilala aliyemaliza muda wake. Yeye kupitia akaunti yake ya mtandao wa
kijamii alithibitisha kutokuwa na mawasiliano na baba yake tangu juzi alasiri
mpaka jana saa tano asubuhi na kushauri wananchi kuwa watulivu, wakati timu ya
uokoaji ikifuatilia chombo hicho.
*Uthibitisho
Muda mfupi baada ya kutaka
wananchi watulie kusubiri kazi ya timu ya uokoaji, Jerry alituma ujumbe katika
akaunti yake ya instagram, akithibitisha kutokea kwa msiba huo.
“Kwa masikitiko makubwa
nimepokea taarifa rasmi kutoka kwa timu ya uokoaji kwamba imefanikiwa kufika
eneo la ajali na kukuta abiria wote na rubani wamepoteza maisha.
“Nimepoteza baba na rubani
mzuri wa nchi yetu, Kapteni William Silaa, nimepoteza rafiki na kiongozi wangu
Mheshimiwa Deo Filikunjombe. Nawapa pole wote waliopoteza ndugu zao nawaombea
marehemu mapumziko ya amani,” alisema Silaa katika taarifa
hiyo.
Pia aliwashukuru wote walioshirikiana na familia
kusaidia uokozi, akiwemo Rais Jakaya Kikwete, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP)
Ernest Mangu, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Adelhem Meru
na Kampuni aliyoitaja kwa jina la
Everest kwa kazi waliyofanya ya kutafuta waathirika wa ajali hiyo.
*Kabwe Zitto
Mwingine aliyezungumzia msiba
huo ni mgombea ubunge wa Kigoma Mjini kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Kabwe
Zitto, aliyekuwa rafiki wa karibu wa Filikunjombe, ambaye asubuhi alitoa
taarifa ya kwenda katika eneo la ajali.
“Nimepoteza rafiki. Nimepoteza
ndugu. Nimepoteza mtu mtiifu kabisa kuwahi kuwa naye. Sina ya kueleza. Mungu
ana mipango yake. Ndugu yetu, rafiki yetu na mzalendo mwenzetu Deo
Filikunjombe, ametutoka katika ajali ya helikopta. Nawasihi tuwe na utulivu
wakati huu mgumu,” alisema Zitto.
*January Makamba
Naye Mjumbe wa Kamati ya
Kampeni ya CCM, January Makamba, alianza kuelezea msiba huo kwa kutaja watu
walioanza kampeni pamoja katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25,
mwaka huu, ambao leo hawapo naye.
Alimtaja Mohamed Mtoi, mgombea
ubunge wa Lushoto kupitia Chadema, ambaye alikufa mwanzoni mwa kampeni za
uchaguzi huu kwa ajali ya gari na kufuatiwa na aliyekuwa mgombea ubunge wa
Ulanga Mashariki kupitia CCM na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma, Celina Kombani, ambaye alifariki hivi karibuni nchini India
alikokuwa akiuguzwa.
Makamba pia amemtaja mgombea
ubunge wa Arusha Mjini, Estomih Mallah (ACT-Wazalendo), aliyefariki Jumamosi
iliyopita baada ya kuugua ghafla na mgombea ubunge wa Handeni Mjini kupitia
CCM, Dk Abdallah Kigoda na Waziri wa Viwanda na Biashara, aliyefariki mwanzoni
mwa wiki hii nchini India na kuzikwa juzi mkoani Tanga.
Taarifa hiyo ya Makamba, pia
ilimtaja Dk Emmanuel Makaidi, Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa na mgombea ubunge wa
Masasi kupitia NLD, ambaye amefariki juzi na anatarajiwa kuzikwa jijini Dar es
Salaam Jumanne katika makaburi ya Sinza.
“Tulianza
nao kampeni, leo hatunao. Mungu waweke na watakatifu mbinguni. Zipe nguvu
familia zao. Siku mbili zilizopita niliongea kwa kirefu na Deo kuhusu mikakati.
Nimepoteza rafiki na ndugu. Mungu amrehemu na pole kwa familia za wafiwa.
“Nimetoka kupokea taarifa
inayothibitisha kwamba chopa aliyokuwa amekodi ndugu yetu Filikunjombe,
imeanguka na watu wote wamefariki,” alisema Makamba katika
taarifa yake kwenye akaunti ya Tweeter.
*Mamlaka ya Anga
Taarifa ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA)
iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana jioni, ilieleza kuwa abiria wengine
waliokufa katika ajali hiyo ni Kasablanka Haule na Egid Mkwela.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, helikopta hiyo iliondoka
katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) juzi saa tisa
alasiri na ilitarajiwa kufika Njombe saa 12 na dakika 20 jioni.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa kituo cha mawasiliano cha
JNIA (ACC) kilipokea taarifa ya ajali hiyo saa 11:54, kutoka kwa mtumishi wa
TCAA, ambaye alipewa taarifa na mtumishi wa Flight Link, ambaye alipigiwa simu
na shuhuda wa ajali hiyo.
Kwa mujibu wa shuhuda huyo aliyekuwa katika vitalu vya
uwindaji vya hifadhi hiyo, helikopta hiyo ilionekana ikianguka huku ikiwaka
moto.
Baada ya taarifa hiyo, imeelezwa kuwa timu ya uokoaji
ilikutana juzi usiku kujiandaa na jana alfajiri iliondoka kwenda eneo la tukio,
kwa kushirikiana na Kampuni ya Ndege ya Everet ya Jijini Dar es Salaam, ambako
walikuta miili ya marehemu hao na kuisafirisha kwenda jijini Dar es Salaam.
*Rambirambi za Magufuli
Mgombea
urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Dk John Magufuli,
ameelezea kupokea kwa mshtuko na huzuni nyingi taarifa za vifo vya
Filikunjombe, Kapteni Silaa na abiria wengine wawili ambao wameaga dunia katika
ajali hiyo.
No comments:
Post a Comment