Thursday, 6 June 2019

Mbwana Samatta Anunuliwa kwa Bilioni 35 England

Mbwana Samatta (wa pili kushoto) akiwa na wachezaji wenzake wa Genk ya Ubelgiji katika moja ya mechi za Ligi  Kuu ya nchi hiyo.

LONDON, England
BRIGHTON inaongoza mbio za klabu za Ligi Kuu kutaka kunsajili mshambuliaji wa mabingwa wa soka wa Ubelgiji Genk na nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mbwana Samatta.

Timu iliyopanda daraja ya Aston Villa, Leicester, Watford pamoja na  Burnley, zote zinataka kumsajili mchezaji huyo kwa kiasi cha pauni milioni 12 (sawa na sh bilioni 35).

Na Samatta, mwenye umri wa miaka 26, anajua kuwa anataka kwenda kucheza soka katika Ligi Kuu ya England baada ya kufanya vizuri katika Ligi Kuu ya Ubelgiji msimu huu.

Mchezaji huyo alifunga mabao 23 na kuisaidia klabu yake ya Genk kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Ubelgiji pamoja na kutwaa tizo ya kiatu cha Ebeny, ambayo hutolewa kwa mchezaji bora wa Ubegiji kutoka Afrika.

Tuzo hiyo huko nyuma imewahi kuchukuliwa na Romelu Lukaku, Vincent Kompany na Michy Batshuayi.

Samatta ataiongoza Taifa Stars katika mashindano ya Mataifa ya Afrika, Afcon 2019, yatakayofanyika Misri mwezi huu, ikiwa ni mara ta kwanza kwa Tanzania kushiriki tangu ilipocheza kwa mara ya mwisho mwaka 1980.

Lakini baada ya kumalizika kwa mashindano hayo, Samatta anatarajia kuondoka Genk, ambayo alijiunga nayo Januari mwaka 2016 akitokea klabu ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo ya TP Mazembe, na kwenda Ligi Kuu ya England.

Brighton imekuwa ikimfuatilia Samatta kwa muda na kocha wazamani Chris Hughton ambaye ni shabiki mkubwa, wakati Graham Potter naye pia amekuwa akimkubali mshambuliaji huyo.

Kocha mpya wa Brighton Graham Potter anataka kuimarisha kikosi chake kipya kwa ajili ya Ligi Kuu.

Samatta endapo atajiunga na Brighton atakuwemo katika ziara ya timu hiyo kabla ya kuanza kwa ligi ambayo itafanyika Austria kuanzia Julai 7 na itacheza mechi kadhaa za kirafiki.

Taifa Stars Yaenda Misri na Matumaini Kedekede


Naibu Waziri, Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Juliana Shonza akikabidhi Bendera ya Taifa kwa Nahodha wa Timu ya Taifa Stars, Mbwana Samatta jijini Dar es Salaam leo Alhamisi. Kulia ni Mkurugenzi wa Michezo, Dk Yussuf Singo. Timu hiyo inatarajia kuondoka kesho Ijumaa kwenda Misri kwa ajili ya michuano ya michuano ya mataifa Africa (Afcon).

Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars,  inatarajiwa kuondoka leo kuelekea nchini Misri ikiwa na kikosi cha wachezaji 32 kwa ajili ya maandalizi ya fainali za Afrika, huku ikibeba matumaini ya kufanya vizuri.

Kabla ya kuanza kwa fainali hizo Juni 21, mwaka huu nchini humo, timu hiyo itaweka kambi ya wiki mbili na kucheza mechi mbili za kirafiki za kujipima nguvu dhidi ya Misri na Zimbabwe au Nigeria.

Akizungumza jana wakati anakabidhiwa bendera na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza,  Nahodha wa kikosi hicho Mbwana Samatta alisema wanaenda kupambana ili kuleta sifa kwa Tanzania.

“Kwa niaba ya wachezaji tunashukuru kwa kuwa nasi hapa na kututakia heri, nafikiri haya ni mashindano makubwa kila mmoja anafahamu, tunaenda kupambana kuleta kitu kitakachoipa sifa serikali hii ya Rais John Magufuli, na tunawaomba muendelee kuwa nasi bega kwa bega kipindi chote cha mashindano,”alisema.

Kocha Mkuu Emmanuel Amunike alisema wanaenda Misri wakiwa na malengo ya kufanya vizuri na kwamba anaamini kujituma kwa wachezaji wake kunaweza kubadilisha historia nyingine, kwani kwenye mpira lolote linaweza kutokea.

“Tangu tumeanza safari hii Agosti mwaka jana hadi hapa tulipofika kumetokana na juhudi za wachezaji, leo tunaenda Misri tukiwa na ahadi na malengo ya kufanya vizuri, lolote linawezekana kama ambavyo baada ya miaka 39 imetokea,”alisema.

Alisema watu wa Tanzania wanastahili kuona mafanikio zaidi kwasababu kuna wachezaji wengi wenye vipaji.

Kocha huyo alimshukuru Waziri Shonza kwa kuwatembelea akisema kuwa wamefurahi ujio wake kwa kuwa umewapa hamasa kama timu.

Awali, Shonza aliwatakia kila la heri wachezaji hao na kusema kuwa ana matumaini watafanya vizuri na kurudi na ushindi.

Alisema macho ya Watanzania yapo kwao hivyo, waende wakapambane, waonyeshe nidhamu na kushikamana ili kuandika historia nyingine nzuri.

“Twende Misri tukashinde na serikali ya awamu ya tano iko pamoja nanyi, tunaomba msituangushe bali mkawe wazalendo mkapigane kufa au kupona kupata matokeo mazuri,”alisema.

Tuesday, 4 June 2019

Arsenal, United Zawania Kumsajili Mchezaji wa PSG


LONDON, England
ARSENAL na Manchester United zinawania kumsajili mchezaji wa Paris Saint-Germain (PSG), Thomas Meunier (pichani) msimu huu, vyanzo vimeiambia ESPN FC.

PSG imeweka wazi mauzo ya mchezaji huyo ambayo itahitaji karibu pauni milioni 30 kwa mchezaji aliyebakiza miezi 12 kwenye mkataba wake.

Vyanzo vilisema, miamba hiyo ya Ligi Kuu tayari imeonyesha nia yao kwa mchezaji huyo.

Kocha wa Arsenal Unai Emery,  aliyemsajili Meunier PSG, yuko nyuma ya the Gunners kumuwania nyota huyo.

Vyanzo viliongeza, United na Arsenal zinajiandaa kupambana kwenye ligi ya Europa msimu ujao badala ya Ligi ya Mabingwa.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 aliliambia Le Parisien kuna klabu kubwa tano zimeonyesha muhitaji tangu Januari.

"PSG haijanambia kama inataka kuniuza,” alisema  Meunier. "Wanajua kwamba wananihitaji.”

"Kama klabu itaniambia 'sikiliza tunataka kukuuza, tunahitaji fedha’ basi sitacheza hapa msimu ujao.”

Wateja Tigo Kujishindia Tiketi Kuishangilia Stars Misri

Mkuu wa Bidhaa na Huduma wa Kampuni ya Simu za Mkononi ya Tigo, David Umoh (kulia) na Meneja wa Huduma za Ziada wa kampuni hiyo, Ikunda Ngowi wakati wa uzinduzi wa Promosheni ya SOKA LA AFRIKA  kwa ajili ya kujishindia tiketi za kwenda Misri kuishangilia Taifa Stars katika mashindano ya Mataifa ya Afrika, Afcon 2019. Hafla hiyo imefanyika Jijini Dar es Salaam leo.

Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Simu za Mkononi ya Tigo itapeleka mashabiki 10 wa soka kuishangilia timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, Afcon 2019, nchini Misri, imeelezwa.

Taifa Stars, itashiriki kwa mara ya kwanza fainali hizo baada ya kushiriki mara ya mwisho miaka 39 iliyopita, wakati mashindano hayo yalipofanyikia Lagos, Nigeria mwaka 1980 na tangu wakati huo imekuwa ikiishia katika hatua ya kufuzu.

Tigo wameanzisha promosheni ya Soka la Afrika ili kupata kupata watu 10, ambao mbali na kujishindia nafasi hizo za kwenda kuishangilia Taifa Stars ikicheza Afcon 2019, pia watapata nafasi ya kuwa mamilionea.
Akizungumza na waandishi wa habari katika uzinduzi wa Soka la Afrika jijini Dar es Salaam leo, Mkuu wa Bidhaa na Huduma wa kampuni hiyo, David Umoh alisema kuwa wateja wa Tigo wanayo nafasi ya kujishindia safari ya kwenda Misri kushuhudia Kombe la Mataifa ya Afrika pamoja na zawadi za fedha taslimu.

Kampuni hiyo imetenga zaidi ya Sh Milioni 50 katika promosheni hiyo ya Soka Letu, ambapo pia kutakuwa na washindi 10, ambao watagharimiwa kila kitu kwenda kuishuhudia Taifa Stars katika michuano hiyo ya Afcon 2019.

“Tunaamini kwa kutumia mashindano haya, tunaweza kupata fursa nzuri kutoa habari, elimu na burudani kwa kutumia jukwaa la mawasiliano na huduma za kampuni hiyo katika kutumia huduma na bidhaa zetu, “alisema Umoh.
Meneja wa Huduma za Ziada wa Tigo, Ikunda Ngowi akizungum\za na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa Promosheni ya SOKA LA AFRIKA uliofanyika jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mkuu wa wa Bidhaa na Huduma wa kampuni hiyo, David Umoh.
Fainali za Afcon ni mashindano makubwa kabisa barani Afrika kwa timu za taifa, ambazo zinawaleta pamoja wachezaji wa Kiafrika wanaoshiriki ligi kubwa na zenye ushindani ndani na nje ya Afrika.

“Tunaamini itakuwa jambo zuri kwa wateja wetu kupata nafasi ya kwenda kushuhudia mashindano haya makubwa ikiwa ni pamoja na kushangilia timu yetu ya Taifa Stars itakayotuwakilisha. Tunawatakia kila la kheri, “aliongeza Umoh.

Alisema zaidi ya wateja 100 watashinda zawasi za fedha taslimu kila siku, wiki na kila mwezi kwa muda wa miezi mitatu katika shindano hilo, ambalo mshiriki atatakiwa kutuma neno SOKA kwenda 15670 ili kuweza kujibu maswali yanayohusu Afcon 2019.

Mashindano ya 32 ya Afcon 2019 yataanza Misri kuanzia Juni 21 hadi Julai 19 na Tanzania imepangwa Kundi C pamoja na Kenya, Senegal na Algeria na itaanza kampeni zake kwa kucheza dhidi ya Senegal.


Saturday, 25 May 2019

Simba Kukabidhiwa Kombe Lao Jumanne Morogoro


Na Mwandishi Wetu
MABINGWA wa Tanzania Bara msimu wa mwaka 2018/19, Simba leo walishindwa kukabidhiwa Kombe lao la Ligi Kuu Tanzania Bara licha ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuahidi kuwakabidhi.

Mchezo huo ambao ulizikutanisha Simba na Biashara ya Musoma, ulichezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na ulianza saa 9:00 Alasiri ili kuikabidhi Simba taji lao. Timu hizo zilifungana bao 1-1.

Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi nchini, Bonface Wambura alisema kuwa wameshindwa kukabidhi kombe jana baada ya kutokuwepo kwa mgemni rasmi, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola.

Wambura alisema kuwa kombe hilo sasa Simba watakabidhiwa Jumanne kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro katika mchezo wa mwisho dhidi ya Mtibwa Sugar.

Hatahivyo, watazamaji waliofika Uwanja wa Taifa licha ya mvua kunyesha karibu kipindi chote cha kwanza na baadhi ya sehemu za uwanja kujaa maji, walionesha kusikitishwa na kutotolewa kwa taji hilo, ambalo ni la 20 kwa Simba kulitwaa.

Katika mchezo huo, Bishara United ndio walikuwa wa kwanza kupata bao baada ya Innocent Edwin kufunga bao la kuongoza katika dakika ya 14, ambalo lilidumu kwa dakika tatu, kwani Simba walisawazisha katika dakika ya 17 mfungaji akiwa ni Clatous Chama.

Nyota wa Simba Meddie Kagere, Emmanuel Okwi na John Bocco walishindwa kufunga licha ya kulifikia mara kwa mara lango la Biashara, lakini maji yaliwazuia wachezaji hao kufunga.

Katika mchezo mwingine leo, Kagera Sugar imekubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa JKT Tanzania katika mchezo uliofanyika jana asubuhi kwenye Uwanja wa JK Park.

NEMC Yawaondoa Hofu Wadau Viwanja vya Ndege


Mwanasheria wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Manchare Heche (aliyenyanyua mikono) akisisitiza jambo wakati akiongea na wadau wanaotoa huduma mbalimbali kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), juu ya katazo la mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku kuendelea kutumika nchini ifikapo Juni Mosi mwaka huu. Wapili kulia ni Mkurugezi wa JNIA, Paul Rwegasha na wa kwanza kushoto ni mkuu wa kitengo cha Mazingira cha TAA, Maxmilian Mahangila.

Na Mwandishi Wetu
BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), leo limewaondolea hofu wadau wanaoendesha huduma mbalimbali kwenye Viwanja vya ndege, katika mkutano ulioitishwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), uliofanyika kwenye Ukumbi wa Watu Mashuhuri (VIP), kuhususiana na katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki ambalo litaanza rasmi Juni Mosi, 2019.

Mwanasheria wa NEMC, Manchare Heche amesema kwa upande wa viwanja vya ndege ipo mifuko, ambayo itaendelea kutumika kwa mujibu wa Kanuni namba tisa (9) ya sheria ya kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki ya mwaka 2019, lakini baada ya kutumika inatakiwa ihifadhiwe sehemu maalum na kupekekwa mahali itakapoteketezwa.
Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Hali ya Hewa kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Joachim Philipo akitoa ushauri kwenye mkutano wa wadau wanaotoa huduma mbalimbali JNIA ulioitishwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), na kuhusisha Wataalam kutoka Baraza ka Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ambao walitoa maelezo mbalimbali juu ya katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki litakaloanza rasmi Juni Mosi, 2019 kwa mujibu wa sheria.
“Kweli katazo linahusu Watanzania wote na wageni na hapa Airport wapo wanaotumia nikiwa na maana ya wafanyakazi na wateja wakiwemo abiria, lakini katika sheria ukiangalia kanuni ya tisa 9 ipo mifuko ya vifungashio ambayo haijazuiwa ni kama ile ya kuhifadhi vyakula, dawa, kilimo na inayohifadhia takataka, mfano korosho au keki wanazopewa abiria kwenye ndege mfuko wake upo katika kipengele cha chakula, hivyo itaendelea kutumika lakini baada ya matumizi tu itahuifadhiwa sehemu iliyoelekezwa tayari kwa kwenda kuteketezwa,” alisisitiza Heche.

Alisema kwa upande wa plastiki zinazofungia mizigo ya abiria wanaosafiri kutoka ndani na nje ya nchi kwa usafiri wa ndege itatakiwa kuondolewa abiria anapofika nchini, na zitakusanywa na kuhifadhiwa maeneo maalum kabla ya kupelekwa eneo lililotengwa kwa ajili ya kuziteketeza.
Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Hali ya Hewa kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Joachim Philipo akitoa ushauri kwenye mkutano wa wadau wanaotoa huduma mbalimbali JNIA ulioitishwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), na kuhusisha Wataalam kutoka Baraza ka Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ambao walitoa maelezo mbalimbali juu ya katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki litakaloanza rasmi Juni Mosi, 2019 kwa mujibu wa sheria.
Hatahivyo, kutokana na matumizi makubwa ya mifuko ya plastiki nchini imesababisha uharibifu mkubwa wa mazingira ikiwemo ya kuziba kwenye mifereji ya maji, kuua wanyama, na kuharibu ardhi, Heche amesema kufuatia katazo hilo serikali imefuta leseni za viwanda vinavyotengeneza mifuko ya plastiki na pia haijawapa tena leseni wale wote leseni zao zilizomaliza muda, ili kuhakikisha sheria na kanuni ya kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki namba 394 ya mwaka 2019.   

Heche ametoa angalizo kwa wale wote wanaohusika na ukamataji wa watumiaji wa mifuko hiyo, kutotumia nguvu ili kuepusha mikwaruzano na kutoelewana.

      Mrakibu Msaidizi wa Uhamiaji, Anna Mushi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), leo akizungumza katika mkutano wa wadau wanaotoa huduma mbalimbali JNIA katika mkutano ulioitishwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), na kuwahusisha Wataalam kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kutokana na katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki ifikapo Juni Mosi, 2019.

Hatahivyo, amewataka wadau hao kuhakikisha wanadai vitambulisho kwa wale wote watakaofika kwenye maeneo yao ya kazi kudai wanakagua endapo wanaendelea kuuza au kutumia mifuko ya plastiki.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Paul Rwegasha amesema tayari kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), wameshatoa taarifa inayokwenda kwenye vituo vyote vya Kimataifa, ambapo kuna shirika la ndege linaloleta abiria Tanzania, ikitaarifu juu ya katazo la mifuko ya plastiki.
Mwanasheria wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Manchare Heche akiwaonesha wadau wanaotoa huduma mbalimbali kwenye Kiwanja cha Ncdege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) moja ya mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku kuendelea kutumika nchini ifikapo Juni Mosi, 2019 katika mkutano uliofanyika leo kwenye ukumbi wa Watu Mashuhuri (VIP).  Kulia ni   Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Paul Rwegasha.
“Hii taarifa inajulikana kitaalam kama ‘timatic pre-information’ ambayo inatumwa kwenye centre zote duniani, ambapo kuna shirika la ndege ambalo linaleta abiria Tanzania itakuwa rahisi wao kupata taarifa ya katazo hilo na kuwafanya wasibebe mifuko hiyo,” amesema Rwegasha.

Pia amewataka wadau wote wanaofanya shughuli mbalimbali kwenye viwanja vya ndege kutoa ushirikiano mkubwa kuwaeleza abiria juu ya katazo hilo, na kuwaelekeza watumie mifuko mbadala, ambayo itakuwa ikipatikana kwenye maduka yaliyopo kwenye majengo ya Kwanza na Pili ya JNIA.

Kwa mujibu wa NEMC imesema watumiaji wa kawaida endapo watakamatwa na mifuko hiyo watatozwa faini ya Tshs. 30,000, kifungo cha siku saba, au vyote kwa pamoja;  wakati kwa muuzaji anapigwa faini ya Tshs 100,000 haizidi Tshs 500,000, kifungo cha miezi mitatu; na watengenezaji watapigwa faini ya kuanzia Tshs milioni 20 na haitazidi bilioni moja na kifungo cha miaka miwili.

Arsenal watangulia Baku kucheza dhidi ya Chelsea

Mchezaji wa Arsenal, Lucas Torreira akiwa mwe ari kubwa akipanda ndege kwenda Baku.

LONDON, England

KLABU ya Arsenal leo imekwea pipa na kwenda Baku tayari kwa nchezo wao wa fainali ya Ligi ya Ulaya utakaopigwa Jumatano, imeelezwa.

The Gunners walipigwa picha wakipanda pipa kutoka Kiwanja cha Ndege cha Luton leo Jumamosi.

Mesut Ozil alionekana akiwa mtulivu kabisa wakati wakianza safari yao hiyo ya saa sita hadi saba kutoka London hadi Baku.

Arsenal wanatakiwa kuifunga Chelsea katika mchezo huo wa wiki ijayo ili kutwaa taji hilo na kupata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa wa Ulaya msimu ujao.

Arsenal imesafiri mapema kwenda Baku, siku tano kabla mchezo huo watakaocheza dhidi ya wapinzani wao wa jiji la London, Chelsea.

Kikosi hicho cha kocha Unai Emery kitakabiliana na Chelsea nchini Azerbaijan kwenye Uwanja wa Olimpiki wa Baku, ambapo wanahitaji ushindi ili kufuzu kwa michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya msimu ujao.

Na leo Jumamosi asubuhi, the Gunners walionekana katika picha wakipanda ndege tayari kwa mchezo huo wa fainali utakaofanyika Jumatano ijayo.
Danny Welbeck akionekana yuko fiti tayari kwa mchezo wa fainali ya Ligi ya Ulaya Jumatano wiki ijayo.
Nahodha wa Arsenal Laurent Koscielny, Mesut Ozil, Lucas Torreira na wachezaji wengine walionekana wakiwa katika ari kubwa wakati wakianza safari hiyo ya saa sita kwenda Baku wakitokea jijini hapa.

Danny Welbeck ameshinda mbio zake za kuwa fiti kwa ajili ya mchezo huo wa fainali ya Ulaya wakati mshambuliaji huyo wa Uingereza naye pia alipigwa picha akisafiri na wachezaji wenzake wa Arsenal akisafiri na timu hiyo ya Arsenal mwishoni mwa wiki.

Mshmabuliaji huyo hajacheza tangu alipoumia kifundo cha mguu Novemba mwaka jana na sasa anatarajiwa kutajwa katika benchi la Emery dhidi ya Chelsea.
Ozil akicheeeka ndami ya ndege kabla ya kupaa kwenda Baku leo.
Huo utakuwa mchezo wa mwisho wa Welbeck katika timu hiyo yenye maskani yake kaskazini ya London, huku mchezaji hyo mwenye umri wa miaka 28 ambaye ni mchezaji wazamani wa Manchester United ataondoka mwishoni mwa msimu wakati mtataba wake utakapomalizika.

Arsenal inaingia katika mchezo huo wa Jumatano usiku ikiwa na presha kubwa zaidi ya Chelsea ili kupata taji hilo la Ulaya kwa ajili ya mashabiki wao.


Chelsea iliipita Arsenal katika mbio za kusaka nne bora katika Ligi Kuu ya England ili kujihakikishia nafasi ya kufuzu kwa hatua ya nne bora na kucheza Ligi ya Mabingwa wa Ulaya msimu ujao.

The Gunners nafasi yake pekee iliyobaki ya kucheza Ligi ya Mabingwa wa Ulaya ni kutwaa taji la Ligi ya Ulaya katika mchezo ho nan i taji la kwanza tangu ili;otwaa taji hilo la Ulaya mwaka 1994.

Monday, 20 May 2019

Guardiola Sasa Ataka Taji Ligi ya Mabingwa Ulaya


LONDON, England
MAFANIKIO ya Manchester City yatakuwa na thamani endapo tu timu hiyo itafanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya licha ya kuweka historia ya kutwaa mataji matatu msimu huu, anasema kocha Pep Guardiola.

Kocha huyo wa Man City, anajua kuwa atakosolewa endapo atashindwa kuiwezesha timu hiyo kufanya vizuri katika mashindano ya Ulaya.

Ushindi wa 6-0 dhidi ya Watford Jumamosi katika fainali ya Kombe la FA likifuatiwa na taji la Ligi Kuu ya England pamoja na lile la Ligi msimu huu.

"Nilisema tangu awali kuwa najua tutahukumiwa mwishoni kama tumeshinda Ligi ya Mabingwa, “alisema Guardiola.

"Bila ya kutwaa taji la Ligi ya Ulaya, basi tutakuwa hatujafanya jambo la kutosha.

"Hilo nililijua mapema, kwani nilipowasili Barcelona, tulikuwa na bahati tulishinda taji hilo la Ulaya mara mbili ndani ya kipindi cha miaka minne na watu walitarajia  kitu maalum kutoka kwangu, ambacho kingetuwezesha kushinda taji la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya hapa City, na hilo litaendelea kuwa sahihi.

"Katika klabu hii, rekodi ya klabu katika mashindano ya nyumbani ni nzuri, lakini Ligi ya Mabingwa wa Ulaya hatujawahi kushinda, hivyo sasa tunajukumu la kushinda taji hilo kwa kuwa tuna wachezaji wazuri sana, “alisema.

Man City imeshinda mara nne taji la Ligi Kuu ya England, mawili ya Kombe la FA na manne ya Ligi, tangu klabu hiyo ilipoanza kumilikiwa na Sheikh Mansour mwaka 2008, lakini pamoja na mafanikio hayo haijawahi kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

Beki Vincent Kompany amekuwa katika timu hiyo kwa wakati wote huo, ikiwemo miaka nane akiwa nahodha wa Man City, lakini alitangaza Jumapili kuwa ataondoka katika klabu hiyo na kwenda kucheza soka Ubelgiji.

Kompany, 33, atajiunga na klabu ya Ubelgiji ya Anderlecht kama kocha mchezaji kwa mkataba wa miaka mitatu.

Mkandarasi Terminal 3 JNIA Kukabidhi Jengo Mapema


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe (Mwenye suti ya bluu) akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Mhandisi Julius Ndyamukama  mara baada ya kuwasili kwa ajili ya ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi katika jengo la tatu la abiria (TB III) katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) jioni ya leo.

Na Mwandishi Wetu
JENGO la Tatu la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA),  Terminal 3, litakabidhiwa mapema kwa wamiliki, imeelezwa.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe amesema kuwa jengo hilo, ambalo litakuwa na uwezo wa kuchukua abiria milioni 6 kwa mwaka, litakabidhiwa Mei 29, ikiwa ni siku moja kabla tarehe ile ya awali iliyoahidiwa na mkandarasi kulikabidhi.

Awali, mkandarasi aliahidi kukabidhi jeingo hilo, Mei 30 kwa wamiliki, ambao ni Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kabla ya kuzinduliwa rasmi na Rais John Pombe Magufuli baadae mwaka huu.

JENGO TAYARI
Tayari ujenzi wa jengo hilo umekamilika kwa asilimia 99.5  na sasa vitu vikubwa vinavyofanyika ni kufunga vifaa mbalimbali, vikiwemo vile vya usalama, milango, vitu na vile vya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TRA).

Alisema kuwa tayari ujenzi umeshakamilika na watu wa TRA, TTCL, Fire na wengine wanaweka mifumo yao ya huduma ili kukamilisha ujenzi huo.


 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe katikati akiwa anaelekea katika jengo la tatu la Abiria (TB III) kuona maendeleo ya mradi wa ujenzi, kulia kwake ni Mhandisi Msimamizi wa Ujenzi wa jengo hilo Barton Komba na kushoto kwake ni Msimamizi wa miradi ya Viwanja vyote vya Ndege Tanzania Mhandisi Godson Ngomuo.

“Mtendaji Mkuu kwa sasa anahangaika na watoa huduma na wanaotakiwa ni wale wenye uwezo mkubsa na ambao hawafanyakazi kwa mazoea na ni bora wakapata vijana wa kitanzania wenye uwezo mkubwa wa kutoa huduma katika jengo hilo bora kabisa na la kisasa, “ alisema Kamwele baada ya kukagua jengo hilo.

MAJARIBIO
Alisema baada ya Mei 29  wataanza kufanya majaribio ya matumizi mbalimbali katika jengo hilo, ambalo halina tofauti kabisa na majengo ya viwanja vya Ulaya nan chi nyingine zilizoendelea.

Aidha, Kamwele alisema baada ya kukamilika kwa Jengo l Terminal 3, ujenzi utahamia katika terminai 2, ambalo lenyewe litatumika kwa ajili ya abiria wa hapa nchini ambao wanatoka na kuwasili kutoka mau kwenda mikoani.

Terminal 3 ina madaraja 12, ambayo yana uwezo wa kuegesha ndege kubwa za idadi hiyo kwa wakati mmoja pia kutakuwa na mageti 16 ya kuingilia na kutokea katika ndege.
Alisema kuwa katika kudhihirisha kuwa ujenzi wa Terminal 3 tayari wafanyakazi wamebaki 1,000 kutoka 2,900 ambao walikuwa wakifanya shuhghuli mbalimbali za ujenzi.

Tayari baadhi ya majengo yaliokuwa ofisi za muda zilizojengwa na mkandarasi katika eneo hilo la Terminal 3 kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali za ujenzi, zimeshavunjwa.
Waziri alisema ameridhishwa kabisa na maendeleo ya ujenzi wa jingo hilo na baada ya Mei 29, TAA itakuwa ikiendesha mafunzo mbalimbali kwa ajili ya watoa huduma uwanjani hapo.

  Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe akisikiliza maelezo kutoka kwa Mhandisi Msimamizi wa Ujenzi Barton Komba kutoka Wakala wa barabara (TANROADS) alienyoosha mkono juu kuhusu eneo la maegesho ya magari katika Jengo la tatu  la Abiria (TB III) wakati wa ziara yake Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) jioni ya leo.

Alisema Mtendaji Mkuu tenda anayohangaika nayo ni watoa huduma kwani wanataka wale wenye uwezo mkubwa, ambao wataendana na ubora wa jingo hilo, hivyo hawataki wale wanaotoa huduma kwa mazoea.

Waziri alipotembelea jengo hilo alishuhudia watu wa TRA, Uhamiaji na wengine wakifunga vifaa vyao, tayari kutoa huduma wakati wowote kiwanja hicho kitapoanza kutumika.

Juni mosi wataanza kutoa huduma kwa majaribio uwanjani hapo, hasa ,ujaribu mifumo mbalimbali kabla ya kutoa taarifa kwa Rais Magufuli kuuzindua jengo hilo la tatu la abiria.

Awali, akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa TB III, Kaimu Mkurugenzi Mkuu TANROADS Mhandisi Crispin Akoo alisema kutokana maendeleo mazuri ya ujenzi Mkandarasi anatarajia kukabidhi jengo mapema.

 “Hadi kufikia terehe 31 Julai 2018 maendeleo yalikua ni asilimia 78.33, lakini hadi kufikia tarehe 18 Mei 2019 ujenzi wote ulikua umefikia asilimia 99.5, ” alisema.

Kuhusu maandalizi ya uendeshaji Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Mhandisi Julius Ndyamukama alimweleza Waziri kwamba majaribio na maandalizi ya uendeshaji yalianza tangu mwezi machi mwaka 2018 na yapo katika hatua za mwisho.

“Majaribio ya kwanza ya kwanza ya mifumo na vifaa vinavyotumia umeme yalianza mwezi Julai 2018 kwa sasa yamefikia asilimia 96 na muda sio mrefu yatakamilika.”

Aidha Mhandisi Ndyamukama aliongeza kwamba majaribio hayo yanatarajiwa kufanyika ndani ya miezi mitatu kuanzia mwezi Mei na ifikapo mwezi Agosti yatakua yamekamilika.

Naye Mhandisi Barton Komba alimwambia mwandishi wetu kuwa, kwa wakati mmoja jingo hilo linaweza kuhudumia hadi abiria 2800 bila tatizo, huku kukiwa na checking counter 42, 37 zikitoa huduma kwa abiria wa madaraja ya kawaida na wale wa business huku tano zikitoa huduma kwa Commecial Important People (CIP).

Saturday, 13 April 2019

Klabu 10 Zawania Ubingwa Taifa wa Kuogelea


Na Mwandishi Wetu
JUMLA ya klabu 10 zimethibitisha kushiriki katika mashindano ya Klabu Bingwa ya taifa ya mchezo wa kuogelea yatakayofanyika kwenye bwawa la kuogelea la Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST), Upanga jijini Dar es Salaam kuanzia leo.

Klabu ambazo zitashiriki katika mashindano hayo ni Bluefins, Champion Rise, Mis Piranhas, klabu ya kuogelea ya Mwanza (MSC), FK Blue na Wahoo ya Zanzibar.

Nyingine zitakazochuana katika mpambano hou ni pamoja na ISM-Moshi, ISM-Arusha, FK Blue Marlins, Talis-IST na mabingwa watetezi, Dar es Salaam Swim Club (DSC).
Mashindano hayo ambayo yatamalizika kesho Jumapili, yamedhaminiwa na IST, Azam, Pepsi, Asas, Samsung, DTB Bank, Kaka’s, Food Lovers na Snow Cream.

Wadhamini wengine ni Kastipharn Ltd, Ruru Logistics, Knight Support, Oppotune Travel ltd, Pyramid Consumers, Print Galore, ITV Media, Clouds FM, Subway, NMB Bank and Umoja Grand Belt na  Road Restaurant.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya mashindano hayo, Hadija Shebe alisema kuwa waogeleaji wa Tanzania wanaoishi nje ya nchi wamewasili tayari kwa mashindano hayo.
Waogeleaji  hao ni Sonia Tumiotto, Maia Tumiotto , Collins Saliboko, Dennis Mhini, Chichi Zengeni, Natalia Sanford, Smriti Gorkarn  na Delvin Barick ambao wote wanasoma Uingereza.

Wengine ni  Christian Shirima anayetokea nchini Ukraine,  Isam Sepetu (Afrika Kusini), Hilal Hemed Hilal na Kangeta wanaotokea klabu ya Hamilton Aquatic ya Dubai.

Alisema kuwa mashindano hayo yamepangwa kuanza saa 2.00 leo na waogeleaji watashindana katika staili tano, ambazo ni Freestyle, Breaststroke, Butterfly, Backstroke na Individual Medley.

Kwa mujibu wa Hadija, waogeleaji hao pia watashindana katika relay katika mashindano ambayo yamepitishwa na Shirikisho la Mchezo wa kuogelea Duniani (Fina) kuwa ya kutafuta alama za kufuzu mashindano ya Dunia yaliyopangwa kufanyika nchini Korea  Julai.

Kwa mujibu wa Hadija, kutakuwa na jumla ya vipengele  vya mashindano 108 na kila klabu imetakiwa kuwakilishwa na waogeleaji wawili katika kila kipengele cha mashindano ambavyo pia vimepangwa kutokana na umri.

Stars Yapangwa na Vigogo Senegal, Algeria Afcon 2019

Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, ikiwa mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

CAIRO, Misri
TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, imepangwa pamoja na majirani zao wa Kenya, Senegal pamoja na Algeria katika Kundi C la fainali za Mataifa ya Afrika, Afcon 2019, zitakazofanyika Misri kuanzia Juni 21 hadi Julai 19 nchini Misri.

Taifa Stars ambayo kwa mara ya kwanza inashiriki hatua ya fainali hiyo baada ya miaka 39, ilijikuta katika kundi hilo baada ya Shirikisho la Soka la Afrika (Caf) kupanga ratiba hiyo jana usiku.

Sasa Stars itakuwa na kibarua kigumu kuhakikisha inatinga hatua ya mtoano kwa kupitia nafasi mbili za moja kwa moja,ambazo hutolewa kwa timu mbili za kwanza au kupitia `best looser’ endapo itafanya vizuri lakini itashindwa kupata nafasi mbili za kwanza.

Aidha, wenyeji Misri, Pharaohs, wamepangwa pamoja na Zimbabwe au Chui,  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR) pamoja na Uganda, ambao walikuwa kundi moja na Tanzania katika hatua ya kufuzu.

Katika Kundi B, timu ya taifa ya Nigeria ya Super Eagles itakabiliana na timu mbili ambazo zimefuzu kwa mara ya kwanza katika Afcon, ambazo ni Burundi na Madagascar pamoja na Guinea.

Mmoja kati ya wachezaji wachezaji kivutio katika mashindano ya mwaka huu, Sadio Mané mwenyewe atakuwepo na timu yake ya Senegal katika Kundi C, ambalo iko Taifa Stars.

Katika Kundi D, Hervé Renard atakutana tena na Ivory Coast. Simba hao wa Milima ya Atlas itawabidi kuwa makini na Afrika Kusini pamoja na nchi ndogo ya Namibia.
Katika Kundi E, Tunisia watakabiliana na Mali pamoja na Mauritania,  ambayo inashiriki kwa bmara ya kwanza fainali hizo, pamoja na Angola.

Mabingwa watetezi Cameroon wenyewe watakabiliana na Black Stars ya Ghana, Benin na Guinea Bissau.

Kufanyika kwa mara ya kwanza kwa fainali hizo katika kipindi cha Juni kutawawezesha wachezaji wote wa Afrika wanaocheza soka Ulaya kuwemo katika timu zao za taifa, kwani wakati huo ligi zote za Ulaya zinakuwa zimemalizika.

Pia hizo zitakuwa fainali kubwa kabisa za Afcon, ambazo zitashirikisha timu 24 kwa mara ya kwanza baada ya huko nyuma kushirikisha timu 16 tu na zilikuwa zikianza Januari hadi Februari.

Kocha wa Morocco Herve Renard atakuwa akiangali kushinda mara ya tatu taji hilo la Afrika, akiwa na timu ya tatu. Simba hao wa Atlas wako katika Kundi D, pamoja na timu ya Ivory Coast aliyowahi kushindwa nayo taji hilo. Zingine ni Afrika Kusini pamoja na majirani zao Namibia.

Mchezo wa kwanza wa mashindano hayo utawakutanisha wenyeji Misri ambao watacheza na Chui wa Zimbabwe, huku Misri wakitarajia kuwa na nyota wa Liverpool Mohamed Salah katika kikosi chao katika mchezo utakaofanyika Juni 21 kwenye Uwanja wa Cairo.

Timu mbili kati ya tatu ambazo zinashiriki kwa mara ya kwanza fainali hizo, Madagascar na Burundi – ziko katika Kundi B pamoja na Nigeria na Guinea.

Ratiba kamili ya Makundi:

Kundi A: Misri, DR Congo, Uganda, Zimbabwe

Kundi B: Nigeria, Guinea, Madagascar, Burundi

Kundi C: Senegal, Algeria, Kenya, Tanzania

Kundi D: Morocco, Ivory Coast, Afrika Kusini, Namibia

Kundi E: Tunisia, Mali, Mauritania, Angola

Kundi F: Cameroon, Ghana, Benin, Guinea-Bissau