Mwanasheria wa Baraza la
Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Manchare Heche
(aliyenyanyua mikono) akisisitiza jambo wakati akiongea na wadau wanaotoa
huduma mbalimbali kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere
(JNIA), juu ya katazo la mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku kuendelea
kutumika nchini ifikapo Juni Mosi mwaka huu. Wapili kulia ni Mkurugezi wa JNIA,
Paul Rwegasha na wa kwanza kushoto ni mkuu wa kitengo cha Mazingira cha TAA,
Maxmilian Mahangila.
Na
Mwandishi Wetu
BARAZA
la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), leo limewaondolea hofu wadau
wanaoendesha huduma mbalimbali kwenye Viwanja vya ndege, katika mkutano
ulioitishwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), uliofanyika kwenye
Ukumbi wa Watu Mashuhuri (VIP), kuhususiana na katazo la matumizi ya mifuko ya
plastiki ambalo litaanza rasmi Juni Mosi, 2019.
Mwanasheria
wa NEMC, Manchare Heche amesema kwa upande wa viwanja vya ndege ipo mifuko,
ambayo itaendelea kutumika kwa mujibu wa Kanuni namba tisa (9) ya sheria ya
kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki ya mwaka 2019, lakini baada ya kutumika
inatakiwa ihifadhiwe sehemu maalum na kupekekwa mahali itakapoteketezwa.
“Kweli
katazo linahusu Watanzania wote na wageni na hapa Airport wapo wanaotumia
nikiwa na maana ya wafanyakazi na wateja wakiwemo abiria, lakini katika sheria
ukiangalia kanuni ya tisa 9 ipo mifuko ya vifungashio ambayo haijazuiwa ni kama
ile ya kuhifadhi vyakula, dawa, kilimo na inayohifadhia takataka, mfano korosho
au keki wanazopewa abiria kwenye ndege mfuko wake upo katika kipengele cha
chakula, hivyo itaendelea kutumika lakini baada ya matumizi tu itahuifadhiwa
sehemu iliyoelekezwa tayari kwa kwenda kuteketezwa,” alisisitiza Heche.
Alisema
kwa upande wa plastiki zinazofungia mizigo ya abiria wanaosafiri kutoka ndani
na nje ya nchi kwa usafiri wa ndege itatakiwa kuondolewa abiria anapofika
nchini, na zitakusanywa na kuhifadhiwa maeneo maalum kabla ya kupelekwa eneo
lililotengwa kwa ajili ya kuziteketeza.
Hatahivyo,
kutokana na matumizi makubwa ya mifuko ya plastiki nchini imesababisha
uharibifu mkubwa wa mazingira ikiwemo ya kuziba kwenye mifereji ya maji, kuua
wanyama, na kuharibu ardhi, Heche amesema kufuatia katazo hilo serikali imefuta
leseni za viwanda vinavyotengeneza mifuko ya plastiki na pia haijawapa tena
leseni wale wote leseni zao zilizomaliza muda, ili kuhakikisha sheria na kanuni
ya kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki namba 394 ya mwaka 2019.
Heche
ametoa angalizo kwa wale wote wanaohusika na ukamataji wa watumiaji wa mifuko
hiyo, kutotumia nguvu ili kuepusha mikwaruzano na kutoelewana.
Mrakibu Msaidizi
wa Uhamiaji, Anna Mushi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere
(JNIA), leo akizungumza katika mkutano wa wadau wanaotoa huduma mbalimbali JNIA
katika mkutano ulioitishwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), na
kuwahusisha Wataalam kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa
Mazingira (NEMC) kutokana na katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki ifikapo
Juni Mosi, 2019.
Hatahivyo,
amewataka wadau hao kuhakikisha wanadai vitambulisho kwa wale wote watakaofika
kwenye maeneo yao ya kazi kudai wanakagua endapo wanaendelea kuuza au kutumia
mifuko ya plastiki.
Kwa
upande wa Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere
(JNIA), Paul Rwegasha amesema tayari kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
Tanzania (TAA), wameshatoa taarifa inayokwenda kwenye vituo vyote vya
Kimataifa, ambapo kuna shirika la ndege linaloleta abiria Tanzania, ikitaarifu
juu ya katazo la mifuko ya plastiki.
“Hii
taarifa inajulikana kitaalam kama ‘timatic pre-information’ ambayo inatumwa
kwenye centre zote duniani, ambapo kuna shirika la ndege ambalo linaleta abiria
Tanzania itakuwa rahisi wao kupata taarifa ya katazo hilo na kuwafanya wasibebe
mifuko hiyo,” amesema Rwegasha.
Pia
amewataka wadau wote wanaofanya shughuli mbalimbali kwenye viwanja vya ndege
kutoa ushirikiano mkubwa kuwaeleza abiria juu ya katazo hilo, na kuwaelekeza
watumie mifuko mbadala, ambayo itakuwa ikipatikana kwenye maduka yaliyopo
kwenye majengo ya Kwanza na Pili ya JNIA.
Kwa
mujibu wa NEMC imesema watumiaji wa kawaida endapo watakamatwa na mifuko hiyo
watatozwa faini ya Tshs. 30,000, kifungo cha siku saba, au vyote kwa
pamoja; wakati kwa muuzaji anapigwa
faini ya Tshs 100,000 haizidi Tshs 500,000, kifungo cha miezi mitatu; na
watengenezaji watapigwa faini ya kuanzia Tshs milioni 20 na haitazidi bilioni
moja na kifungo cha miaka miwili.
No comments:
Post a Comment