Saturday 13 April 2019

Klabu 10 Zawania Ubingwa Taifa wa Kuogelea


Na Mwandishi Wetu
JUMLA ya klabu 10 zimethibitisha kushiriki katika mashindano ya Klabu Bingwa ya taifa ya mchezo wa kuogelea yatakayofanyika kwenye bwawa la kuogelea la Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST), Upanga jijini Dar es Salaam kuanzia leo.

Klabu ambazo zitashiriki katika mashindano hayo ni Bluefins, Champion Rise, Mis Piranhas, klabu ya kuogelea ya Mwanza (MSC), FK Blue na Wahoo ya Zanzibar.

Nyingine zitakazochuana katika mpambano hou ni pamoja na ISM-Moshi, ISM-Arusha, FK Blue Marlins, Talis-IST na mabingwa watetezi, Dar es Salaam Swim Club (DSC).
Mashindano hayo ambayo yatamalizika kesho Jumapili, yamedhaminiwa na IST, Azam, Pepsi, Asas, Samsung, DTB Bank, Kaka’s, Food Lovers na Snow Cream.

Wadhamini wengine ni Kastipharn Ltd, Ruru Logistics, Knight Support, Oppotune Travel ltd, Pyramid Consumers, Print Galore, ITV Media, Clouds FM, Subway, NMB Bank and Umoja Grand Belt na  Road Restaurant.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya mashindano hayo, Hadija Shebe alisema kuwa waogeleaji wa Tanzania wanaoishi nje ya nchi wamewasili tayari kwa mashindano hayo.
Waogeleaji  hao ni Sonia Tumiotto, Maia Tumiotto , Collins Saliboko, Dennis Mhini, Chichi Zengeni, Natalia Sanford, Smriti Gorkarn  na Delvin Barick ambao wote wanasoma Uingereza.

Wengine ni  Christian Shirima anayetokea nchini Ukraine,  Isam Sepetu (Afrika Kusini), Hilal Hemed Hilal na Kangeta wanaotokea klabu ya Hamilton Aquatic ya Dubai.

Alisema kuwa mashindano hayo yamepangwa kuanza saa 2.00 leo na waogeleaji watashindana katika staili tano, ambazo ni Freestyle, Breaststroke, Butterfly, Backstroke na Individual Medley.

Kwa mujibu wa Hadija, waogeleaji hao pia watashindana katika relay katika mashindano ambayo yamepitishwa na Shirikisho la Mchezo wa kuogelea Duniani (Fina) kuwa ya kutafuta alama za kufuzu mashindano ya Dunia yaliyopangwa kufanyika nchini Korea  Julai.

Kwa mujibu wa Hadija, kutakuwa na jumla ya vipengele  vya mashindano 108 na kila klabu imetakiwa kuwakilishwa na waogeleaji wawili katika kila kipengele cha mashindano ambavyo pia vimepangwa kutokana na umri.

No comments:

Post a Comment