Naibu Waziri, Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na
Michezo, Juliana Shonza akikabidhi Bendera ya Taifa kwa Nahodha wa Timu ya
Taifa Stars, Mbwana Samatta jijini Dar es Salaam leo Alhamisi. Kulia ni Mkurugenzi wa
Michezo, Dk Yussuf Singo. Timu hiyo inatarajia kuondoka kesho Ijumaa kwenda Misri kwa
ajili ya michuano ya michuano ya mataifa Africa (Afcon).
Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, inatarajiwa kuondoka leo kuelekea nchini Misri
ikiwa na kikosi cha wachezaji 32 kwa ajili ya maandalizi ya fainali za Afrika, huku
ikibeba matumaini ya kufanya vizuri.
Kabla ya kuanza kwa fainali hizo Juni 21, mwaka huu
nchini humo, timu hiyo itaweka kambi ya wiki mbili na kucheza mechi mbili za kirafiki
za kujipima nguvu dhidi ya Misri na Zimbabwe au Nigeria.
Akizungumza jana wakati anakabidhiwa bendera na Naibu
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza, Nahodha wa kikosi hicho Mbwana Samatta alisema
wanaenda kupambana ili kuleta sifa kwa Tanzania.
“Kwa niaba ya wachezaji tunashukuru kwa kuwa nasi
hapa na kututakia heri, nafikiri haya ni mashindano makubwa kila mmoja
anafahamu, tunaenda kupambana kuleta kitu kitakachoipa sifa serikali hii ya
Rais John Magufuli, na tunawaomba muendelee kuwa nasi bega kwa bega kipindi
chote cha mashindano,”alisema.
Kocha Mkuu Emmanuel Amunike alisema wanaenda Misri
wakiwa na malengo ya kufanya vizuri na kwamba anaamini kujituma kwa wachezaji
wake kunaweza kubadilisha historia nyingine, kwani kwenye mpira lolote linaweza
kutokea.
“Tangu tumeanza safari hii Agosti mwaka jana hadi
hapa tulipofika kumetokana na juhudi za wachezaji, leo tunaenda Misri tukiwa na
ahadi na malengo ya kufanya vizuri, lolote linawezekana kama ambavyo baada ya
miaka 39 imetokea,”alisema.
Alisema watu wa Tanzania wanastahili kuona mafanikio
zaidi kwasababu kuna wachezaji wengi wenye vipaji.
Kocha huyo alimshukuru Waziri Shonza kwa kuwatembelea
akisema kuwa wamefurahi ujio wake kwa kuwa umewapa hamasa kama timu.
Awali, Shonza aliwatakia kila la heri wachezaji hao na kusema
kuwa ana matumaini watafanya vizuri na kurudi na ushindi.
Alisema macho ya Watanzania yapo kwao hivyo, waende
wakapambane, waonyeshe nidhamu na kushikamana ili kuandika historia nyingine
nzuri.
“Twende Misri tukashinde na serikali ya awamu ya tano
iko pamoja nanyi, tunaomba msituangushe bali mkawe wazalendo mkapigane kufa au
kupona kupata matokeo mazuri,”alisema.
No comments:
Post a Comment