LONDON, England
MAFANIKIO ya Manchester City yatakuwa na
thamani endapo tu timu hiyo itafanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya
licha ya kuweka historia ya kutwaa mataji matatu msimu huu, anasema kocha Pep Guardiola.
Kocha huyo wa Man City, anajua kuwa
atakosolewa endapo atashindwa kuiwezesha timu hiyo kufanya vizuri katika
mashindano ya Ulaya.
Ushindi wa 6-0 dhidi ya Watford Jumamosi
katika fainali ya Kombe la FA likifuatiwa na taji la Ligi Kuu ya England pamoja
na lile la Ligi msimu huu.
"Nilisema tangu awali kuwa najua
tutahukumiwa mwishoni kama tumeshinda Ligi ya Mabingwa, “alisema Guardiola.
"Bila ya kutwaa taji la Ligi ya Ulaya,
basi tutakuwa hatujafanya jambo la kutosha.
"Hilo nililijua mapema, kwani nilipowasili
Barcelona, tulikuwa na bahati tulishinda taji hilo la Ulaya mara mbili ndani ya
kipindi cha miaka minne na watu walitarajia kitu maalum kutoka kwangu, ambacho
kingetuwezesha kushinda taji la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya hapa City, na hilo litaendelea
kuwa sahihi.
"Katika klabu hii, rekodi ya klabu
katika mashindano ya nyumbani ni nzuri, lakini Ligi ya Mabingwa wa Ulaya
hatujawahi kushinda, hivyo sasa tunajukumu la kushinda taji hilo kwa kuwa tuna
wachezaji wazuri sana, “alisema.
Man City imeshinda mara nne taji la Ligi Kuu
ya England, mawili ya Kombe la FA na manne ya Ligi, tangu klabu hiyo ilipoanza
kumilikiwa na Sheikh Mansour mwaka 2008, lakini pamoja na mafanikio hayo
haijawahi kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.
Beki Vincent Kompany amekuwa katika timu hiyo
kwa wakati wote huo, ikiwemo miaka nane akiwa nahodha wa Man City, lakini
alitangaza Jumapili kuwa ataondoka katika klabu hiyo na kwenda kucheza soka
Ubelgiji.
Kompany, 33, atajiunga na klabu ya Ubelgiji
ya Anderlecht kama kocha mchezaji kwa mkataba wa miaka mitatu.
No comments:
Post a Comment