Saturday, 25 May 2019

Simba Kukabidhiwa Kombe Lao Jumanne Morogoro


Na Mwandishi Wetu
MABINGWA wa Tanzania Bara msimu wa mwaka 2018/19, Simba leo walishindwa kukabidhiwa Kombe lao la Ligi Kuu Tanzania Bara licha ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuahidi kuwakabidhi.

Mchezo huo ambao ulizikutanisha Simba na Biashara ya Musoma, ulichezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na ulianza saa 9:00 Alasiri ili kuikabidhi Simba taji lao. Timu hizo zilifungana bao 1-1.

Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi nchini, Bonface Wambura alisema kuwa wameshindwa kukabidhi kombe jana baada ya kutokuwepo kwa mgemni rasmi, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola.

Wambura alisema kuwa kombe hilo sasa Simba watakabidhiwa Jumanne kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro katika mchezo wa mwisho dhidi ya Mtibwa Sugar.

Hatahivyo, watazamaji waliofika Uwanja wa Taifa licha ya mvua kunyesha karibu kipindi chote cha kwanza na baadhi ya sehemu za uwanja kujaa maji, walionesha kusikitishwa na kutotolewa kwa taji hilo, ambalo ni la 20 kwa Simba kulitwaa.

Katika mchezo huo, Bishara United ndio walikuwa wa kwanza kupata bao baada ya Innocent Edwin kufunga bao la kuongoza katika dakika ya 14, ambalo lilidumu kwa dakika tatu, kwani Simba walisawazisha katika dakika ya 17 mfungaji akiwa ni Clatous Chama.

Nyota wa Simba Meddie Kagere, Emmanuel Okwi na John Bocco walishindwa kufunga licha ya kulifikia mara kwa mara lango la Biashara, lakini maji yaliwazuia wachezaji hao kufunga.

Katika mchezo mwingine leo, Kagera Sugar imekubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa JKT Tanzania katika mchezo uliofanyika jana asubuhi kwenye Uwanja wa JK Park.

No comments:

Post a Comment