Saturday, 13 April 2019

Stars Yapangwa na Vigogo Senegal, Algeria Afcon 2019

Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, ikiwa mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

CAIRO, Misri
TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, imepangwa pamoja na majirani zao wa Kenya, Senegal pamoja na Algeria katika Kundi C la fainali za Mataifa ya Afrika, Afcon 2019, zitakazofanyika Misri kuanzia Juni 21 hadi Julai 19 nchini Misri.

Taifa Stars ambayo kwa mara ya kwanza inashiriki hatua ya fainali hiyo baada ya miaka 39, ilijikuta katika kundi hilo baada ya Shirikisho la Soka la Afrika (Caf) kupanga ratiba hiyo jana usiku.

Sasa Stars itakuwa na kibarua kigumu kuhakikisha inatinga hatua ya mtoano kwa kupitia nafasi mbili za moja kwa moja,ambazo hutolewa kwa timu mbili za kwanza au kupitia `best looser’ endapo itafanya vizuri lakini itashindwa kupata nafasi mbili za kwanza.

Aidha, wenyeji Misri, Pharaohs, wamepangwa pamoja na Zimbabwe au Chui,  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR) pamoja na Uganda, ambao walikuwa kundi moja na Tanzania katika hatua ya kufuzu.

Katika Kundi B, timu ya taifa ya Nigeria ya Super Eagles itakabiliana na timu mbili ambazo zimefuzu kwa mara ya kwanza katika Afcon, ambazo ni Burundi na Madagascar pamoja na Guinea.

Mmoja kati ya wachezaji wachezaji kivutio katika mashindano ya mwaka huu, Sadio Mané mwenyewe atakuwepo na timu yake ya Senegal katika Kundi C, ambalo iko Taifa Stars.

Katika Kundi D, Hervé Renard atakutana tena na Ivory Coast. Simba hao wa Milima ya Atlas itawabidi kuwa makini na Afrika Kusini pamoja na nchi ndogo ya Namibia.
Katika Kundi E, Tunisia watakabiliana na Mali pamoja na Mauritania,  ambayo inashiriki kwa bmara ya kwanza fainali hizo, pamoja na Angola.

Mabingwa watetezi Cameroon wenyewe watakabiliana na Black Stars ya Ghana, Benin na Guinea Bissau.

Kufanyika kwa mara ya kwanza kwa fainali hizo katika kipindi cha Juni kutawawezesha wachezaji wote wa Afrika wanaocheza soka Ulaya kuwemo katika timu zao za taifa, kwani wakati huo ligi zote za Ulaya zinakuwa zimemalizika.

Pia hizo zitakuwa fainali kubwa kabisa za Afcon, ambazo zitashirikisha timu 24 kwa mara ya kwanza baada ya huko nyuma kushirikisha timu 16 tu na zilikuwa zikianza Januari hadi Februari.

Kocha wa Morocco Herve Renard atakuwa akiangali kushinda mara ya tatu taji hilo la Afrika, akiwa na timu ya tatu. Simba hao wa Atlas wako katika Kundi D, pamoja na timu ya Ivory Coast aliyowahi kushindwa nayo taji hilo. Zingine ni Afrika Kusini pamoja na majirani zao Namibia.

Mchezo wa kwanza wa mashindano hayo utawakutanisha wenyeji Misri ambao watacheza na Chui wa Zimbabwe, huku Misri wakitarajia kuwa na nyota wa Liverpool Mohamed Salah katika kikosi chao katika mchezo utakaofanyika Juni 21 kwenye Uwanja wa Cairo.

Timu mbili kati ya tatu ambazo zinashiriki kwa mara ya kwanza fainali hizo, Madagascar na Burundi – ziko katika Kundi B pamoja na Nigeria na Guinea.

Ratiba kamili ya Makundi:

Kundi A: Misri, DR Congo, Uganda, Zimbabwe

Kundi B: Nigeria, Guinea, Madagascar, Burundi

Kundi C: Senegal, Algeria, Kenya, Tanzania

Kundi D: Morocco, Ivory Coast, Afrika Kusini, Namibia

Kundi E: Tunisia, Mali, Mauritania, Angola

Kundi F: Cameroon, Ghana, Benin, Guinea-Bissau

No comments:

Post a Comment