Friday, 29 December 2017

TAA Waomboleza Kifo cha Mwanasheria Delfine

Bi. Delfine Mulogo wakati wa uhai wake.
Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), inamlilia kwa masikitiko makubwa Mwanasheria wake Bi. Delfine Mulogo (32) aliyekuwa Kituo cha kazi cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) aliyefariki dunia Desemba 25.

Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi na Ugavi, Bw. Mtengela Hanga akisoma wasifu wa marehemu katika kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Augustine Mbezi Temboni, alisema, atakumbukwa kwa uchapakazi, uhodari na uadilifu wake kazini.

Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Augustine, Padri Fidelis Mfaranyembo lililopo Mbezi Temboni jijini Dar es Salaam, akinyunyizia maji ya baraka kwenye mwili wa aliyekuwa Mwanasheria wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Kituo cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bi. Delfine Mulogo kabla ya kusafirishwa kwenda Kijiji cha Uru Kishumundu Mkoani Kilimanjaro kwa maziko.

“Tunasikitika kumpoteza mwanasheria huyu kijana, kwa niaba ya Bodi ya Ushauri ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, tunatoa pole kwa wafiwa kwa kuondokewa na mpendwa wao, lakini sisi kama mamlaka na taifa kwa ujumla tumempoteza mtu muhimu sana aliyekuwa mchapakazi, tutamkumbuka sana marehemu,” alisema Bw. Hanga.

Marehemu ambaye ameacha mume Bw. Alex Temba na watoto wawili, Faith (9) na Harieth (4) alihamishiwa TAA tarehe 01/04/2016 akitokea Halmashauri ya Manispaa ya mji wa Songea alipokuwa akifanya kazi kama mwanasheria kuanzia mwaka 2012.
Bw. Alex Temba (wa pili kushoto), mume wa marehemu aliyekuwa Mwanasheria wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kituo cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bi. Delfine Mulogo akiwa na binti yake Faith Temba (mwenye gauni jeupe) wakitoa heshima za mwisho katika kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Augustine lililopo Mbezi Temboni kabla ya kusafirishwa kwa mazishi katika Kijiji cha Uru Kishumundu mkoani Kilimanjaro. 
Naye Mwakilishi wa Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS), Bw. Stephen Msechu alisema marehemu alikuwa mwanachama tangu alipoapishwa kuwa Wakili mwaka 2012 na kupewa namba ya uanachama 3361 na amekuwa akishirikiana nao katika shughuli mbalimbali kwa uadilifu mkubwa.

Hata hivyo, Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Augustine lililopo Mbezi Temboni, Padri Fidelis Mfaranyembo aliwataka waombolezaji waliofika kuuaga mwili wa marehemu  Delfine kujiandaa wakati wote kwa kuwa hawajui siku wala saa watakayotwaliwa.

Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Lawrence Thobias akitoa heshima zake kwa mwili wa aliyekuwa Mwanasheria Kituo cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bi. Delfine Mulogo aliyefariki Desemba 25. Marehemu atazikwa Kijiji cha Uru Kishumundu mkoani Kilimanjaro.
Padri Mfaranyembo alisema pia waombolezaji wahakikishe wanakuwa watu wa sala wakati wote ili kumuombea marehemu aweze kupokelewa na aingie katika ufalme wa mbinguni, kwani ufalme huo upo kwa kuwa kunamaisha baada ya kifo.

“Kuna mwanafalsafa mmoja wa zamani, Plato alitafakari  sana kuwa mwanadamu akifa anakwenda wapi? na akaona kila mwanadamu anabeba roho ya muumbaji  na hivyo unapokufa roho inarudi kwa yule aliyeiumba, "alisema na kuongeza:

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Bi. Agnes Kijazi akimpa pole Bw. Alex Temba kufuatia kifo cha Mkewe Bi. Delfine Mulogo aliyekuwa Mwanasheria kwenye Kituo cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) aliyefariki Desemba 25 na atazikwa Kijiji cha Uru Kishumundu mkoani Kilimanjaro.
" Plato anatufundisha ya kwamba mwisho wa maisha yake hapa duniani Mwanadamu anarudi kwa Mungu wake kulingana na namna alivyokuwa akiishi na wengine hapa duniani,” alisema Padri Mfaranyembo.

Pia amemtaka mume wa marehemu Bw. Temba asifadhaike kwa kuondokewa na mkewe, bali ajikabidhi kwa Mungu kwa kumuomba hakika atamsaidia kwa kumtia nguvu na kumpa uwezo wa kuendelea kuwahudumia watoto wake kwa kadri ya uweza wake Mungu.

Wafanyakazi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) wakijumuika na waombolezaji wengine katika misa ya kumwombea marehemu Bi. Delfine Mulogo aliyekuwa Mwanasheria kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).
Marehemu alipata elimu ya msingi katika shule ya Oysterbay (1991), baadaye sekondari ya St. Mathew (1998), na baadaye elimu ya Kidato cha Tano na Sita katika shule ya Wasichana ya Kibosho (2004), na mwaka 2008 alihitimu Shahada ya Kwanza ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Tumaini.     
Mweka Hazina wa Klabu ya Uchukuzi, Bw. Benjamin Bikulamchi (kulia), akimkabidhi rambirambi aliyewahi kuwa Katibu wa Klabu hiyo, Bw. Alex Temba aliyefiwa na mkewe Bi. Delfine Mulogo aliyekuwa Mwanasheria Kituo cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).
Viongozi wa Shirikisho la Michezo la Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI), Bi. Itika Mwankenja na Bi. Joyce Benjamin wakitoa rambirambi zao kwa Katibu Msaidizi wa shirikisho hilo Bw. Alex Temba (kushoto) aliyefiwa na Mkewe Bi. Delfine Mulogo wakati wa misa ya kumwombea marehemu iliyofanyika jana katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Augustine lililopo Mbezi Temboni.
Bwana Ametoa na Bwana Ametwaa Jina Lake Lihimidiwe.  Amina.

Monday, 25 December 2017

Bodi ya Ushauri ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania yakutana JNIA katika kikao cha kawaida


 Bodi ya Ushauri (MAB) ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, wakiwa kwenye ukumbi wa mikutano wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) katika kikao cha kawaida cha 33 cha kujadili masuala mbalimbali ya utendaji ya mamlaka kwa kipindi cha robo ya kwanza na pili ya mwaka wa fedha 2017/2018.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (kulia) akimweleza jambo Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri (MAB) ya mamlaka hiyo, Prof. Mhandisi Ninatubu Lema (katikati),  katika kikao cha 33 cha Kawaida cha kujadili robo ya kwanza na pili ya mwaka wa fedha 2017/2018 kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).

Wajumbe wa Bodi ya Ushauri (MAB) ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, wakiwa katika kikao cha kawaida cha 33 cha kujadili masuala mbalimbali ya utendaji kwa kipindi cha robo ya kwanza na pili ya mwaka wa fedha 2017/2018 kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).

Mjumbe wa Bodi ya Ushauri (MAB) ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Dr. Frederick Mwakibinga (kushoto) akizungumza jambo kwenye kikao cha 33 cha bodi hiyo cha kujadili robo ya kwanza na pili ya mwaka wa fedha 2017/2018, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA). 

Mkombozi arudi SHIMIWI kwa kishindo

Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed Kiganja (kulia) akimpongeza Alex Temba mara baada ya uchaguzi wa Shirikisho la Michezo la Idara na Wizara za Serikali (SHIMIWI), uliofanyika hivi karibuni kwenye hoteli ya Mount Uluguru mkoani Morogoro.
 Na Mwandishi Wetu

MWEKA Hazina, William Mkombozi ‘Mgosi’ amerudi kwa kishindo katika nafasi hiyo baada ya kushinda kwenye uchaguzi wa Shirikisho la Michezo kwa Idara na Wizara za Serikali (SHIMIWI), uliofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa hoteli ya Mount Uluguru mkoani Morogoro.

Mkombozi aliyewahi kuongoza katika miaka ya mwanzoni ya 2000 akiwa na aliyewahi kuwa mjumbe na baadaye Katibu Mkuu, Bw. Ramadhani Sululu, lakini baadaye alikaa pembeni sasa amechaguliwa tena kwa kura 23.

Naye Alex Temba aliyeongoza kwa muda mrefu katika Klabu yenye wachezaji mahiri ya Uchukuzi, alichaguliwa kuwa Katibu Msaidizi baada ya kushinda kwa kura 28 na kumbwaga Margreth Mtaki aliyepata kura 15.

Hatahivyo, nafasi ya Mwenyekiti ilirudi tena kwa Daniel Mwalusamba aliyekuwa hana mpinzani kwa kupata kura 42;  huku Ally Katembo akichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti kwa kura 41; wakati Moshi Makuka ametetea nafasi yake ya Ukatibu kwa kura 38 dhidi ya Andrew Sekimweri aliyeondoka na kura sita.

Katika nafasi ya Mweka Hazina Msaidizi, ameshinda Frank Kibona kwa kura 21; wakati walioshinda kwenye ujumbe wa kamati ya utendaji na kura zao zikiwa kwenye mabano ni Apolo Kayungi (44), Assumpta Mwilanga (42), Aloyce Ngonyani (40), Damiani Manembe (39)  na Seleman Kifyoga (31).

Kwa upande wa nafasi ya viti maalum wanawake walioshinda ni Mwajuma Kisengo (20) na Mariam Kihange (18) na waliwashindwa ni Costance Momadi (16) na Buya Masunga (12).


Michezo ya SHIMIWI inayoshirikisha wafanyakazi wa mashirika ya umma imepoteza mvuto kwa kutofanyika takribani miaka miwili mfululizo kutokana na sababu mbalimbali zilizokuwa zikielezwa na uongozi wa juu.

Hatahivyo, kutofanyika kwa michezo hiyo kumewanyima haki watumishi wa umma kushindwa kujenga afya zao na kudumisha umoja na urafiki ikiwa ni pamoja na kukutana na watumishi wengine mbalimbali wa Idara na Wizara nyingine wakati wa michezo hiyo.

Mbali na kutofanyika kwa michezo hiyo pia kumekuwa hakuna mabonanza ya kushirikisha idara za serikali na wizara kwa muda mrefu, ambapo tayari Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameagiza kufanyika kwa mazoezi ya viungo angalau mara moja kila mwezi ili kujenga afya kwa watumishi wa umma.


 

Kifimbo cha Malkia chatua Brisbane, Australia

Mbio za Kifimbo cha Malkia wa Uingereza zilianza Machi 13 mwaka huu.

BRISBANE, Australia

BAADA ya kuanza safari yake kutoka Buckingham Palace Machi 13 mwaka huu jijini London, Kifimbo cha Malkia hatimaye kimewasili kwa waandaaji wa Michezo ya Jumuiya ya Madola nchini Australia leo na sasa kinaelekea katika mji wa Gold Coast.

Kifimbo hicho kiliwasili jijini hapa asubuhi ya leo baada ya kusafiri kwa takribani siku 288 na kutembelea mataifa yote ya Jumuiya ya Madola.

Leo ambayo ni siku ya Krismas inabakisha siku 100 kamili kabla ya kuanza kwa michezo hiyo ya 21 tangu kuanza kufanyika kwake.

Balozi wa Gold Coast 2018 na muogeleaji Mcameroon McEvoy alipokea kifimbo hicho kutoka kwa Hugh Graham, ambaye ni makamu wa rais wa Shirikisho la Michezo ya Jumuiya ya Madola kwa Kanda ya Oceania, kufuatia kuwasili kutoka New Zealand.


Umati mkubwa wa watu akiwemo Borobi, walikusanyika kumuona McEvoy akibeba Kifimbo katika ukumbi wa Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Brisbane, asubuhi ya pilika pilika nyingi katika mwaka.

Serikari yawakoromea Maofisa Michezo, Utamaduni

Na Mwandishi Wetu, Karatu


SERIKALI imesema kuwa maofisa michezo na wale wa utamaduni hawafanyi kazi zao vizuri na ndio maana kumeshindwa kuvumbuliwa vipaji vipya na kusababisha wachezaji wale wale kushiriki katika mashindano mara kwa mara.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akifunga tamasha la 16 la Michezo na Utamaduni la Karatu kwenye viwanja vya Mazingira Bora hapa.

Shonza alisema kuwa maofisa michezo na utamaduni wengi wao wamekuwa wakipokea mishahara bure, kwani wameshindwa kufanya kazi zao za kusaidia kuibua vipaji kama wanavyofanya wenzao wa Karatu kupitia tamasha hilo.

Alisema maofisa hao wanatakiwa kwenda chini hatua ya vijiji ili kuibua vipaji na kuviendeleza tofauti na wengi wao, ambao wanapokea mishahara bure bila ya kufanya kazi yoyote.

Aliongeza kusema kuwa ndio maana vijana wengi wamekuwa wakijihusisha na shughuli zisizofaha kama uvutaji wa bangi, matumizi ya dawa za kulevya na wizi kutokana na kutoshirikishwa katika michezo, hivyo aliwataka maofisa hao kufanya kazi zao vizuri.

Pia aliwataka viongozi wa wilaya ya Karatu kuhakikisha wilayani kwao kuna kiwanja kikubwa cha michezo ili kuwawezesha vijana kutumia kiwanja hicho kuendeleza vipaji vyao.

Alisema ni aibu kubwa kuona wilaya ya Karatu pamoja na vipaji vya michezo vilivypo hakuna uwanja wa maana wa michezo, hivyo aliwataka kukijenga au kuwapokonya wale waliovamia maeneo ya wazi.


Tuesday, 19 December 2017

Kocha, Wakala wa Gatlin katika Kashfa ya doping

NEW YORK, Marekani
BINGWA wa dunia wa mbio fupi Justin Gatlin (pichani) anasema kuwa `ameshtushwa na kushangazwa’ na madai ya dawa za kuongeza nguvu zilizotolewa dhidi ya kocha na wakala wake.

Viongozi wa riadha na Taasisi ya Kupambana na Dawa za Kuongeza Nguvu Michezoni wameanza uchunguzi kile ambacho Rais wa mchezo huo duniani ameyaita  ‘madai mazito’ kuhusu Dennis Mitchell na Robert Wagner.

Gazeti la The Daily Telegraph liliandika Wagner – wakala anayehusiana na Gatlin – alitoa dawa hizo zilizopigwa marufuku kwa waandishi wa habari ambao hawakujulikana.

Mkanda wa video uliotolewa na Telegraph unamuonesha mtu ambaye gazeti hilo limesema ni Wagner alimshauri Gatlin kutumia dawa hizo zilizopigwa marufuku, kama vile wanariadha wengine wa mbio fupi wa Marekani.

Gazeti hilo limesema kuwa kocha wa Gatlin, ambaye ni bingwa wa medali ya dhahabu wa Olimpiki Mitchell, aliwaambia waandishi wa habari kuwa wanariadha wanaweza kukwepa kubainika kutumia dawa hizo kwa sababu vipimo vinashindwa kubaini dawa hizo walizotumia.

WOTE WAKANA TUHUMA
Akiandika katika Instagram jana, Gatlin alisema kuwa “atamtimua mara moja” Mitchell "mara nitakapobaini ukweli kuhusu tuhuma hizi ".

Mwanariadha huyo Mmarekani mwenye umri wa miaka 35 alisema “hatumii na hajawahi kutumia” dawa hizo za kusisimua misuli.

Aliongeza: "Suala hilo tayari ameanza kulishughulikia kisheria ili kuhakikisha hakuna watu wengine wanatoa taarifa za uongo kama hizi kuhusu mimi.”

The Telegraph limesema waandishi wa habari ndio walimpeleka wawakilishi wa kampuni ya filamu, ambaye alijifanya kama kocha amabaye anamfundisha kocha mwanariadha wake kuwa nyota.

Taasisi mbalimbali ikiwemo Shirikisho la Kimataifa la Riadha (IAAF) pamoja na Chama cha Maadili, na Taasisi ya Kuzuia Matumizi ya Dawa za Kuongeza Nguvu ya Marekani (Usada) zilisema zimeanzisha uchunguzi kuhusu madai hayo.

Rais wa IAAF Lord Coe alisema: "Tuhuma hizi ni kubwa sana na ninajua Kamati Huru ya Maadili ya Riadha itachunguza kwa kina kuhusu tuhuma hizo…”


Gatlin, ambaye alitumikia mara mbili vifungo baada ya kubainika kutuia dawa hizo, alishinda medali ya dhahabu katika mbio za meta 100 katika mashindano ya riadha ya Dunia mwezi Agosti jijini London, akimshinda Usain Bolt katika mchezo wa mwisho wa meta 100 kwa Mjamaica huyo kabla hajastaafu kucheza mbio.

Real Ikifungwa na Barcelona ndio basi tena La Liga


MADRID, Hispania
KLABU ya Real Madrid endapo itafungwa katika mchzo wao wa El Classico dhidi ya Barcelona, basi itakuwa imetupwa nje ya mbio za kusaka ubingwa wa Ligi Kuu ya Hispania ya La Liga kagika mchezo utakaofanyika wikiendi hii.
Endapo itashinda, na ikifuatiwa na ushindi mwingine  kutaiwezesha timu hiyo kupunguza tofauti ya pointi dhidi ya Barcelona na kuwa  pointi tano kabla ya mapumziko ya kipindi cha baridi na kukipa kikosi cha  Zinedine Zidane nafasi ya kupambana.
Mpambano huo wa El Clasico kwa timu hizo kupambana katika mpmbano wa La Liga ni wa kwanza tangu Aprili.
Tangu walipofugwa na Real Madrid katika mchezo wa Supercopa de Espana katika kipindi cha majira ya joto. Barca wametamba zaidi dhidi ya wapinzani wao.

TAARIFA ZA TIMU
Rais wa Real Madrid, Florentino Perez anatazamia Gareth Bale atacheza kufuatia kufanya vvizuri katika Kombe la Klabu Duniani.

Na Cristiano Ronaldo anataka Bale kucheza katika nafasi ya Isco kutokana na kutoelewana na Muhispania huyo wa Kimataifa.

Majeruhi Paco Alcacer hatakueemo katika kikosi cha Barcelona licha ya kufanya kazi nzuri msimu huu katika klabu hiyo, baada ya kufunga mabao yote katika ushindi wa timu hiyo wa mabao 2-1 nyumbani dhidi ya Sevilla.

HISTORIA YA MECHI ZAO

Mchezo huo wa Jumapili utakuwa ni wa 236 wa kiushindani kukutana timu hizo zenye upinzani wa hali ya juu katika soka.

Zawadi Zaongezwa Tamasha la Karatu 2017

Na Mwandishi Wetu
WAANDAAJI wa tamasha la kila mwaka la michezo na Utamaduni la Karatu wameongeza zawadi kwa washindi watatu wa kwanza wa michezo yote itakayoshindaniwa mwaka huu.

Kwa mujibu wa mratibu wa tamasha hilo Meta Petro, bingwa wa mwaka huu wa mbio za kilometa 10 kwa wanaume ataondoka na kitita cha sh 500,000 huku mshindi wa pili akipata sh 300,000 wakati watatu ataondoka na sh 250,000.

Zawadi kama hizo pia zitatolewa kwa washindi wa kwanza hadi watatu wa mbio za wanawake za kilometa tano, huku watoto wadogo, ambao watashiriki mbio za kilometa 2.5, wenyewe mwaka huu mshindi wa kwanza, ataondoka na sh 100,000 badala ya 50,000.

Mbali na riadha, pia zawadi kwa washindi wa mbio za baiskeli ambazo zitawashindanisha wanaume katika umbali wa kilometa 60 na wanawake 30, nao mwaka huu wameongezewa zawadi.

Mbali na mbio na baiskeli, pia tamasha hilo linashirikisha mchezo wa soka, mpira wa wavu, kwaya pamoja na ngoma za utamaduni na sarakasi.

Alisema kuwa tamasha la mwaka huu linatarajia kuvuta washiriki wengi baada ya klabu kibao na wanariadha binafsi na wapanda baiskeli kujisajili kwa wingi kwa ajili ya kushiriki michezo hiyo.

Baadhi ya klabu za riadha ambazo zimethibitisha kushiriki tamasha hilo ni pamoja na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT),ambayo itakuwa na zaidi ya wanariadha 25, Magereza Arusha yenye anariadha 20, Jambo Athletics Club, Ketra zote za Arusha, Lingwa ya Singida na Lyan ya Mbulu.

Mbali na riadha, Petro alizitaja klabu za baiskeli zilizothibitisha kushiriki kuwa ni pamoja na Lake Manyara Cycling Club ya Manyara, Hakika ya Arusha , Klabu ya Baiskeli ya Magugu na Arusha Cycling Club kutoka mkoani humo.

Mbali na riadha na baiskeli, tamasha hilo pia litakuwa na mpira wa wavu pamoja na soka, ambazo fainali zake zitafanyika Desemba 22 ikiwa ni siku moja kabla ya kilele cha tamasha hilo, ambalo linatarajia kufungwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe.


Tamasha hilo ambalo huandaliwa na Filbert Bayi Foundation (FBF) kwa kushirikiana na TOC, Chama cha Riadha Karatu na kudhaminiwa na Olympic Solidarity,limekuwa chachu ya kuibua vipaji hasa katika mchezo wa riadha.

Friday, 15 December 2017

TFF Yarekebisha Ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara

Na Mwandishi Wetu
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limefanya marekebisho ya Ligi Kuu Tanzania Bara na sasa itaendelea mwishoni mwa mweiz huu baada ya kusimama ili kupisha michuano ya Chalenji ambayo inafikia kikomo kesho Jumapili nchini Kenya.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka TFF, mechi za Ligi Kuu raundi ya 12 zitapigwa Desemba 2 na 31 na zingine zitafanyika Januari mosi mwakani.

Vilevile mechi 16 kati ya 152 zilizobaki za Ligi hiyo zitachezwa kuanzia saa 8:00 mchana. Kwa mujibu wa Kanuni ya 14 (45) ya Ligi Kuu, mchezo wowote wa Ligi Kuu unatakiwa kuchezwa kati ya saa 8:00 mchana, na saa 4:00 usiku.

Uamuzi huo umefanywa ili kuongeza mechi ambazo zinataoneshwa moja kwa moja (live) na mdhamini wa matangazo, hatua ambayo itaisaidia Bodi ya Ligi kufuatilia kwa karibu uchezeshaji wa waamuzi na pia kutoa nafasi kwa wadhamini wa Ligi pamoja na wa klabu kuonekana zaidi (mileage).

Hivyo, mechi 102 kati ya 152 zitaoneshwa moja kwa moja ikiwemo zile zinazofanyika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam ambazo kwa kawaida zinachezwa kuanzia saa 1:00 usiku.

Mechi za raundi ya 12 ni Desemba 29; Azam vs Stand United (saa 1 usiku), Desemba 30; Lipuli vs Tanzania Prisons (saa 8 mchana), Mtibwa Sugar vs Majimaji (saa 10 jioni), 

Ndanda vs Simba (saa 10 jioni), Desemba 31; Njombe Mji vs Singida United (saa 8 mchana), Mbao vs Yanga (saa 10 jioni), Januari 1; Mbeya City vs Kagera Sugar (saa 10 jioni), na Mwadui vs Ruvu Shooting (saa 10 jioni).

Baada ya raundi ya 12, Ligi Kuu ya Vodacom itapisha mechi za Kombe la Mapinduzi na raundi ya tatu ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports itakayochezwa kati ya Januari 5 na 7 mwakani kabla ya kuingia raundi ya 13 itakayofanyika kati ya Januari 13 na 17, 2018.

Kwa upande wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL), itaingia raundi ya 10 Desemba 30 kwa mechi za Kundi A na C, wakati mechi za Kundi B zitafanyika Desemba 31.

Fainali ya Michuano ya Kombe la Chalenji inafanyika leo nchini Kenya wakati wenyeji Harambee Stars watakapotoana jasho na timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes.

Zanzibar Heroes Yaivua Ubingwa Uganda Cranes


Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes, imeivua ubingwa wa Kombe la Chalenji Uganda Cranes baada ya kuifunga mabao 2-1 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Moi mjini Kisumu leo.

Zanzibar ambayo awali ilikuwa haipewi nafasi ya kufanya vizuri, iliwavua ubingwa Uganda katika mchezo huo wa nusu fainali ya pili na sasa itakutana na wenyeji Kenya katika mchezo huo wa fainali.

Hii ni mara ya pili kwa Zanzibar kucheza nusu fainali baada ya mara ya kwanza kufikia hatua hiyo mwaka 1995, ambapo ilitwaa taji hilo kwa mara ya kwanza.

Mchezaji wa Zanzibar, Abdul-Azziz Makame ndiye aliyeifungia timu hiyo bao la kwanza katika dakika ya 22 kabla mfungaji anayeogoza kwa kupachika mabao katika mashindano hayo, Derrick Nsibambi kuisawazishia Uganda na kufikisha mabao manne dakika saba kabla ya mapumziko.

Mohammed Issa Juma ndiye aliyeihakikishia Zanzibar Heroes kucheza fainali na kunusa ubingwa baada ya kufunga bao la ushindi  kwa penalty baada ya dakika 57 na kuiwezesha timu hiyo ya kisiwani kuweka historia ya ushindi mjini Kisumu.

Sasa sasa watacheza na wenyeji Harambee Stars – ambao waliifunga Burundi kwa bao baada ya muda wa nyongeza katika nusu fainali ya kwanza baada ya timu hiyo kutoka suluhu katika dakika 90 za kawaida na kuongezewa dakika zingine 30 kwenye Uwanja wa Kenyatta mjini Machakos.
Fainali hiyo itapigwa Jumapili, ambapo mshindi atapatikana.

The Cranes walimaliza wakiwa 10 uwanjani baada ya mchezaji aliyeingia akitokea benchi, Joseph Nsubuga alipotolewa nje baada ya kuonyeshwa kadi yekundu ya moja kwa moja katika dakika ya 55 baada ya kumchezea vibaya Ahmada Ibrahim katika eneo la hatari.

“Huu ulikuwa mchezo mgumu dhidi ya mabingwa watetezi, Namshukuru Mungu na wachezaji wangu kwa ushindi huu uliotupeleka katika fainali ya Cecafa Challenge Cup. Tulistahili kushinda leo kutokana na jinsi tulivyocheza.”


“Tunaiheshimu Kenya ambao ni wapinzani wetu wajao katika fainali. Na hiyo haina maana kuwa tunawaogopa bkwa sababu tumekuja hapa kushinda kikombe.” Alisema kocha wa Zanzibar Hemed Morocco.

Mabondia Timu ya Taifa Walilia Kambi, Vifaa

Na Mwandishi Wetu
MABONDIA wa timu ya taifa ya Tanzania wamesema kuwa wanataka kupatiwa kambi ya kudumu pamoja na vifaa ili waweze kujiandaa vizuri kwa ajili ya Michezo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika Aprili mwakani Gold Coast, Australia.

Kocha Mkuu wa timu hiyo inayoendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa, Said Omary au maarufu kama Gogopoa alisema juzi kuwa timu inaendelea na mazoezi lakini ina changamoto kibao.

Amezitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na mabondia kukosa vifaa vya mazoezi zikiwemo padi, glovu na vifaa vingine pamoja na kutokuwa katika kambi ya kudumu na hivyo kushindwa kufuatilia mazoezi vizuri.

Amesema anaiomba Serikali kuingia kati suala hilo ili timu hiyo ipate mahitaji yake na iweze kujiandaa vizuri kwa ajili ya michezo hiyo ya mwakani.

Naye nahodha wa timu hiyo, Seleman Kidunda alisema kuwa mabondia wanahitaji kambi ya kudumu ili kuwapunguzia gharama za kwenda na kurudi kutoka mazoezini.

Alisema mbali na nauli, mabondia hawana fedha za kupata mlo baada ya mazoezi na timu hiyo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa vifaa vya mazoezi,

Pia Kidunda amesema kuwa pia mabondia wanahitaji mechi za majaribio ili kuwaweka fiti na kuwapatia uzoefu kwa ajili ya mashindano ya kimataifa.


Juhudi za kuwapata viongozi wa Shirikisho la Ndondi Tanzania (BFT) zinaendelea baada ya simu ya katibu mkuu wake, Makore Mashaga kuitwa bila kupokelewa leo.

Taifa Cup Netiboli Kuanza Rasmi Jumapili Arusha

Na Mwandishi Wetu
KINYANGANYIRO cha kumsaka bingwa wa taifa wa netiboli Tanzania kinaanza rasmi Jumapili kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha na Katibu Tawala wa Mkoa huo, Richard Kwitega ndiye anatarajia kuwa geni rasmi katika ufunguzi huo.

Katibu Mkuu wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta), Judith Ilunda amesema kuwa, ufunguzi rasmi utafanyika Jumapili na timu za mikoa ya Morogoro na wenyeji Arusha ndio itafungua mashindano hayo.

Ilunda amesema kuwa mechi ya pili Jumapili ni ile itakayozikutanisha timu za mikoa ya Dodoma na Kilimanjaro, ambay ndio italayofunda dimba siku hiyo.

Amesema kuwa mechi za mashindano hayo zinatazamiwa kuanza Jumamosi kabla ya ufungizi rasmi Jumapili, ambapo kutakuwa ne mpambano kati ya Kigoma watakaocheza dhidi ya Arusha kuanzia saa 8:00 mchana, huku mkoa wa Songwe ukitoana jasho na Kigamboni kabla ya Morogoro haijapepetana na Kagera.

Ilunda anasema kuwa hadi sasa jumla ya mikoa 12 ilikuwa imethibiisha kushiriki mashindano hayo yanayotarajia kumalizika Desemba 23 mwaka huu, ambapo washindi watakabidhiwa zawadi zao vikiwemo vikombe na vyeti vya ushiriki.

Anasema kuwa uongozi wake ambao uliingia madarakani Septemba 30 mjini Dodoma, unaendesha mashindano kwa shinda kutokana na ukosefu wa fedha nan i matumaini yao kuwa wadau wa netiboli ikiwemo Serikali itawasaidia kufanikisha majukumu yao.

Awali, mashindano hayo yalipangwa kuanza Desemba 10, lakini yaliahirishwa kutokana na Chaneta kushindwa kupata zaidi y ash milioni 20 kwa ajili ya kuendeshea mashindano hayo ya Taifa Cup.


Hivi karibui Chaneta iliendesha kwa mafanikio makubwa mashindano ya Ligi Daraja la Pili Taifa yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Jakaya Kikwete Jijini Dar es Salaam, ambapo timu saba zilipanda daraja.

Thursday, 14 December 2017

Wanariadha kibao wajitokeza mbio za Karatu 2017

 
Na Mwandishi Wetu

WANARIADHA na klabu mbalimbali za riadha zimejitokeza kwa wingi kuthibitisha kushiriki tamasha la 16 la Michezo na Utamadani la Karatu litakalofanyika Desemba 23, imeelezwa.

Mratibu wa tamasha hilo linalofanyika kila mwaka mjini humo, Meta Petro alisema leo kwa njia ya simu kuwa, wanariadha binafsi au klabu zimethibitisha kushiriki tamasha hilo, ambalo litamalizikia katika viwanja vya Mazingira Bora mjini Karatu.

Petro alitaja baadhi ya klabu za riadha zilizothibitisha kushiriki kuwa ni pamoja na Magereza Arusha, ambayo itakuwa na wanariadha 20, Jeshi la Kujenga Taifa, Jambo Athletics Club, Ketra zote za Arusha, Lingwa ya Singida na Lyan ya Mbulu.

Mbali na riadha, Petro alizitaja klabu za baiskeli zilizothibitisha kushiriki kuwa ni pamoja na Lake Manyara Cycling Club ya Manyara, Hakika ya Arusha , Klabu ya Baiskeli ya Magugu na Arusha Cycling Club kutoka mkoani humo.

Mbali na riadha na baiskeli, tamasha hilo pia litakuwa na mpira wa wavu pamoja na soka, ambazo fainali zake zitafanyika Desemba 22 ikiwa ni siku moja kabla ya kilele cha tamasha hilo, ambalo litafungwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe.

Petro alisema kuwa pia kutakuwa na burudani za ngoma za utamaduni, kwaya pamoja na maigizo na sarakasi vitakavyofanyika wakati wa ufungaji wa tamasha hilo la kila mwaka.

Wanariadha watachuana katika mbio za kilometa 10 na tano kwa wanaume na wanawake huku watoto wadogo wakichuana katika mbio za kilometa 2.5 wakati mbio za baiskeli zitakuwa za kilometa 60 kwa wanaume wakati wanawake watapiga pedari umbali wa kilometa 30.


Tamasha hilo ambalo huandaliwa na Filbert Bayi Foundation (FBF) kwa kushirikiana na TOC, Chama cha Riadha Karatu na kudhaminiwa na Olympic Solidarity,limekuwa chachu ya kuibua vipaji hasa vya mchezo wa riadha.

Wednesday, 13 December 2017

Moody Sheli ndiye Mr Tanzania Fitness 2017

Moody Sheli (mbele) akiwaongoza wenzake katika moja ya mazoezi kwenye viwanja vya Leaders Club Kinondoni jana.
Na Mwandishi Wetu
MOODY Sheli ametwaa ubingwa wa Mr Tanzania Fitness baada ya kuwashinda washiriki wengine 29 katika mpambano uliofanyika kwenye viwanja vya Leaders Club jijini Dar es Salaam.

Katika shindano hilo washiriki walichuana katika michuano mbalimbali ikiwa kubeba vyma, kupiga pushapu, kukimbia na mazoezi mengine mbalimbali, ambapo Sheli alinekana kungara zaidi.

Nafasi ya pili ilichukuliwa na watu wawili, ambao walifungana kwa pointi ambao ni Eric Majura pamoja na Obadia Andabwile huku nafasi ya tatu ikienda kwa Martine Njessa.


Mwenyekiti wa Shirikisho la Mchezo wa Kujenga Mwili Tanzania, TBBF, Nemes Chiwalala akitete jambo wakati wa shindano la kumsaka Mr Tanzania Fitness kwenye viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam.
Kilele cha shindano la kumsaka Mr Tanzania 2017 kitafanyika kesho Ijumaa katika ukumbi wa hoteli ya May Fair Plaza Mikocheni Jijini Dar es Salaam, ambapo mshindi atapatikana, ambapo washindi wataondoka na zawadi nono likiwemo gari aina ya Noah na sh milioni 10 kwa mshindi wa kwanza.

Leo Alhamisi litafanyika shindano la kumsaka mshiriki maarufu zaidi katika mitandao ya kijamii.