Wednesday, 13 December 2017

TAA Yataka Magari ya Zimamoto kutunzwa

  Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (aliyesimama mbele), akiongea na askari wa zimamoto na uokoaji wa kituo cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA). Mbele kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa JNIA, Bw. Johannes Munanka na (kulia) ni Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji wa Viwanja vya Ndege nchini, Kamishna Msaidizi, Christom Manyologa.

Na Mwandishi Wetu
KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela  amewataka madereva wanaoendesha magari ya zimamoto na uokoaji kwenye viwanja vyote vya ndege Tanzania kuyathamini na kuyatunza magari hayo kwa kuwa wameaminiwa kufanya kazi hiyo.

Kamanda wa Vikosi vya Zimamoto na Uokoaji wa Viwanja vya Ndege, Kamishna Msaidizi, Christom Manyologa (wa pili kushoto) akiwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (wapili kulia) na Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Johannes Munanka (kushoto), wakiwa na msimamizi wa chumba cha Habari na Mawasiliano cha kituo hicho, afande Joines Matucha.

Bw. Mayongela alitoa kauli hiyo kwenye Kituo cha Zimamoto na Uokoaji cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), alipokwenda kujitambulisha na kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili, ambapo alisema magari hayo yamenunuliwa kwa gharama kubwa, hivyo yanapaswa kutunzwa.

Alisema uthamini wao kwa magari hayo kutayafanya kudumu na kuyafanya kazi kwa muda mrefu bila kuharibika, jambo ambalo litachangia ufanisi wa kazi, ya uokoaji na usalama kwenye viwanja vya ndege, ambapo mbali na miundombinu pia lazima miundombinu ipewe kipaumbele.


“Najua wapo wenzenu wachache sio waaminifu wamekuwa wakitengeneza manunuzi hewa ya vifaa na hata mafuta kwa manufaa yao binafsi, lakini ninawaomba mujione nyie ndio wenye thamani kwa kuaminiwa kuendesha magari haya ya mamilioni ya fedha, kwani ni nyie tu mnayoweza kuyaendesha kutokana na kuwa na mitambo ya kisasa tofauti kidogo na mengine, hivyo basi tuyatunze ili tuisaidie serikali yetu isiingie gharama za mara kwa mara za kununua vifaa au magari mengine mapya,” alisisitiza Bw. Mayongela.

Hatahivyo, alisema zimamoto ni moja ya mambo ya msingi hivyo amewahakikishia kuwapeleka kozi za mara kwa mara za ndani na nje ya nchi, kutokana na mambo mbalimbali yanayobadilika duniani, na kwa kuanzia ataanza na askari wawili hadi wanne, kulingana na mafunzo wanayostahili kushiriki, na atahakikisha washiriki ndio wanaokwenda kufanyia kazi kwa vitendo katika utendaji wao na sio kupeleka mabosi ambao hawahusiki.

“Nia yangu ni nyie kufanya kazi kwa weledi na kufanyakazi kwa bidii, nisije kusikia hakuna fedha, lakini wakati huo huo mnamuona Mkurugenzi Mkuu anapanda ndege kwenda Ulaya na kurudi hizo fedha zinatoka wapi, nasema kama kweli kuna mambo ya msingi basi Zimamoto ni jambo la msingi, hivyo basi sisi wafanya maamuzi tunatakiwa kuangalia wanaostahili kupata mafunzo na waende, hivyo nitahakikikisha kwa kadri ya bajeti nitatenga mafungu ya kupeleka watu wangu hawa kwenye mafunzo, ili nao waende na wakati katika endeshaji kulingana na mabadiliko ya teknolojia na mashirika ya usafiri wa anga duniani yanavyoagiza,” alisema Bw. Mayongela.

Hatahivyo, ameahidi kwa mwaka wa fedha 2017/2018 TAA itanunua magari sita ya zimamoto na uokoaji pamoja na redio zitakazotumika kwa mawasiliano katika chumba cha habari na mawasiliano, kinachowasiliana na mnara wa kuongoza ndege.

Kutokana  na kuharibika kwa mara kwa mara kwa magari ya Zimamoto kwenye viwanja vya ndege,  Tanzania ameahidi kufufua karakana ya kutengeneza magari hayo iliyopo JNIA, ambapo tayari amewaita mafundi waliopo hapo kukutana naye ili kuwasilisha changamoto na vifaa vinavyohusiana na magari hayo, ili waanze kutengeneza kwa haraka baada ya kununuliwa vifaa hivyo.

Pia aliwataka kuwa na ushirikiano wa dhati na wafanyakazi wa TAA katika utendaji wao wa kazi na kuwa walinzi wa mali za serikali kutokana na wao wamekula kiapo.

Naye Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji wa Viwanja vya Ndege Tanzania, Kamishna Msaidizi Christom Manyologa alisema amefarijika kwa ujio wa Kaimu Mkurugenzi wa TAA, Bw. Mayongela,  ambaye ameonesha nia thabiti ya kushirikiana katika kazi.

Kamishna Manyologa alisema askari wa Zimamoto na Uokoaji , astahili kuheshimika zaidi kwani yeye ndio anayeweza kuingia ndani na kufika karibu ya ndege na pia anayewasiliana na waongoza ndege.


“Huyu askari anastahili kuheshimiwa kwanza anamamlaka makubwa ya kuwa karibu kabisa ya ndege, kupita ndani ya barabara ya kutua na kuruka kwa ndege, hivyo anaweza kufanya lolote baya akiamua, hivyo watendewe vizuri,” alisema Kamishna Manyologa.
Kamanda wa Vikosi vya Zimamoto na Uokoaji wa Viwanja vya Ndege, Kamishna Msaidizi, Christom Manyologa (wa pili kushoto) akiwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (wapili kulia) na Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Johannes Munanka (kushoto), wakiwa na msimamizi wa chumba cha Habari na Mawasiliano cha kituo hicho, afande Joines Matucha.


Monday, 11 December 2017

Chelsea, Real mtihani mgumu 16 bora Ulaya

Real Madrid
ZURICH, Uswisi
KLABU ya Chelsea itakuwa na mtihani mgumu kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya baada ya kupangwa kucheza dhidi ya Barcelona katika mchezo wa hatua ya 16 bora,  wakati Tottenham itakabiliana na mabingwa wa Italia Juventus katika mchezo mwingine wa hatua hiyo.

Vinara wa Ligi Kuu ya England Manchester City wenyewe watakabiliana na wawakilishi wa Uswisi Basel, Manchester United wenyewe watacheza dhidi ya timu inayoshiriki Ligi Kuu ya Hispania, La Liga ya Sevilla na Liverpool watatoana jasho dhidi ya timu ya Ureno ya Porto.

Mabingwa watetezi wa Kombe la Ligi ya Mabingwa wa Afrika Real Madrid wenyewe watakabiliana na vinara wa Ufaransa Paris St-Germain.

England imeweka rekodi kwa kuingiza timu tano kutoka hatua ya makundi na kucheza hatua ya 16 bora msimu huu.

Celtic v Zenit, Arsenal watacheza dhidi ya Ostersunds katika hatua ya timu 32 bora ya Ligi ya Ulaya au Uefa ndogo kama inavyojulikana na wengi.

Chelsea ndio timu eee ya Uingereza kufuzu hatua ya 16 bora kama mshindi wa pili swa kundi lake, huku timu zingine nne zikiongoza katika makundi yao.

The Blues (Chelsea) ndio inaonekana kuwa na kibarua kigumu zaidi kwa timu za Uingereza katika hatua hiyo ya 16 bora na kuiweka katika wakati mgumu wa kuvuka hatua hiyo kutokana na ukali pamoja na uzoefu wa Barcelona inayoongozwa na Lione Messi.

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya kocha wa Chelsea Antonio Conte kusema kuwa nafasi ya timu yake kutetea taji la Ligi Kuu imetoweka baada ya timu hiyo kupokea kivhapo cha kutoka kwa West Ham, ambacho kimewaacha wakiwa nyuma hya Manchester City kwa pointi 14.

Hatahivyo, Chelsea iliifunga Barcelona katika nusu fainali kabla ya kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya mwaka 2012.

Real Madrid, ambayo iko mbioni kutwaa taji la 13 na la tatu mfululizo, nayo imepewa timu ngumu ya PSG, ambayo imetumia fedha kwa ajili ya usajili  na imemaliza nyuma ya Tottenham katika Kundi H.

Washindi wa makundi watakuwa ugenini katika mchezo wa kwanza wa hatua hiyo ya 16 bora Februari 13 au 14 na Februari 20/21, na nyumbani katika mchezo wa marufdiano utakaofanyika kati ya Machi 6/7 na Machi 13/14.

Fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya itafanyika Mei 26 Kiev,

RATIBA KAMILI YA HATUA YA 16 BORA YA LIGI YA MABINGWA WA ULAYA:-

Juventus v Tottenham (Februari 13 na Machi 7, 2018)

Basel v Manchester City (Februaria 13 na Machi 7, 2018)

Porto v Liverpool (Februari 14 na Machi 6, 2018)

Sevilla v Manchester United (Februari 21 na Machi 13, 2018)

Real Madrid v PSG (Februari 14 na Februaria 6, 2018)

Shakhtar Donetsk v Roma (Februari 21 na Machi 13, 2018)

Chelsea v Barcelona (Februari 20 na Machi 14, 2018)


Bayern Munich v Besiktas (Februari 20 na Machi 14, 2018)

Sunday, 10 December 2017

Mr Tanzania 2017 kupatikana Desemba 15 MayFair

Mwenyekiti wa Kamati ya Shindano la Mr Tanzania 2017, Nilesh Bett akizungumza na wanahabari kuhusu shindano hilo. Kushoto ni Katibu wa Shirikisho la Mchezo wa Kutunisha Misuli Tanzania (TBBF), Francis Mapugilo.
Na Mwandishi Wetu
SHINDANO la kumsaka MR Tanzania 2017 litafanyika jijini Dar es Salaam Desemba 15 katika hoteli ya MayFair, imeelezwa.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Kujenga Mwili Tanzania (TBBF), Francis Mapugilo alisema jijini Dar es Salaam kuwa, maandalizi ya shindano hilo yanaendelea vizuri na hadi sasa kuna washiriki 60, ambao watachujwa na kubaki 30 watakaoingia kambini.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Kunyanyua Vitu Vizito Tanzania, TBBF, Francis Mapugilo (katikati) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu shindano la Mr Tanzania 2017 litakalofanyika Desemba 13, 2017. Kulia ni msemaji wa Pilipili Entertainment, Mzee Chilo na kushoto ni mwenyekiti cha TBBF,, Nemes Chiwalala.
Akifafanua kuhusu kumpata Mr Tanzania 2017, Mapugilo alisema kuwa Desemba 12 kutakuwa na shindano la kumsaka Fashion Icon, ambalo litafanyika kwa Hussein Pamba Kali, ambalo washiriki watavaa nguo mbalimbali na yule mwenye mwonekano mzuri atashinda.

Alisema siku inayofuata, kutakuwa na shindano la kumsaka Mr Fit, ambapo washiriki watachuana katika mazoezi mbalimbali yakiwemo kuchomoka kwa kasi, kupiga pushapu na mazoezi mengine.
Mapugilo alisema kuwa shindano jingine dogo litafanyika Desemba 14, ambalo litakuwa kumsaka Mr Photojenic, ambalo litafanyikia katika eneo la kuogelea la hoteli ya MayFair.

Alisema katika shindano hilo atatafutwa mshiriki mwenye m uonekano mzuri katika picha, ambapo pia washiriki watatembea na kupozi ili kupata picha nzuri,ambazo zitashindanishwa na kumpata mshindi.

Alisema yote hayo yatakamilishwa Desemba 15 kwa shindano kubwa na mshiriki atakayekuwa maarufu zaidi ndiye atayeibuka Mr Tanzania 2017 na kupata nafasi ya kushiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa.

Naye Mwenyekiti wa Shindano hilo, Nilesh Batt alisema kuwa shindano hilo limeandaliwa vizuri  ili kuhakikisha mshindi wa ukweli anapatikana ambaye atawakilisha vizuri Tanzania katika mashindano ya kimataifa ya Mr Afrika pamoja na yale ya dunia yatakayofanyika mwakani Nigeria na Uingereza.

TOC yavitaka vyama kuweka wazi mahesabu yao


Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Gulam Rashid akizungumza wakati wa ufungiuzi wa Mkutano Mkuu wa TOC leo mjini Zanzibar. Kushoto ni Makamu wa Rais, Henry Tandau na kulia ni Katibu Mkuu wa Kamati hiyo, Filbert Bayi.
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
KAMATI ya Olimpiki Tanzania (TOC) imevitaka vyama au mashirikisho ya michezo kuwa na utawala bora.

Hayo yameelezwa leo na Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa kawaida wa kamati hiyo uliofanyika jana katika Kituo cha Amani Welezo mjini Zanzibar.
Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi akisoma taarifa yake katika Mkutano Mkuu wa kamati hiyo leo.
Bayi alisema kuwa ujumbe wa mwaka huu ni Utawala Bora’ikiwa ni pamoja na uwazi ma uwajibikaji, ambapo alivitaka vyama na mashirikisho ya michezo kuwa wa wazi katika mapato na matumizi yao.

Alisema kila mwaka wakati wa mkutano mkuu wa TOC wamekuwa wakivitaka vyama kuwdeka wazi fedha wazipatazo pamoja na matumizi, lakini hilo limekuwa halitekelezwi na viongozi wengi.
Mmoja wa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TOC, Juliana Yassoda akifuatilia mkutano huo leo.
Alisema wao (TOC) wamekuwa wazi kwani kila mwaka wakati wa mkutano wao mkuu, huweka wazi kwa vyama mapato na matumizi yao bila kificho kama ilivyoagizwa na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki,IOC.

Naye Rais wa TOC, Gulam Rashid alisema kuwa TOC inapinga kabisa matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu kwani ni hatari kwa wachezaji wetu.

Wajumbe wakifuatilia Mkutano Mkuu wa TOC leo mjini Zanzibar.
Alisema anaipongeza Serikali kupitisha sharia ya kupinga matumizi ya dawa hizo na kuifanya Tanzania kuwa mwanachama rasmi katika upingaji wa matumizi ya dawa hizo.
Makamu wa Rais wa TOC, Henry Tandau akizungumza wakati wa mkutano huo.
Rashid aliyasema hayo wakati akisoma taarifa yake katika mkutano huo mkuu wa kawaida wa mwaka.

Aidha, alivitaka vyama kuthibitisha kushiriki katika mikutano mikuu pamoja na ile ya Kamati ya Wachezaji (Kawata) ili kuondoa usumbufu kwa TOC katika kupanga taratibu.

Mwenyekiti mpya wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta), Dk Devota Marwa akihudhuria kwa mara ya kwanza Mkutano Mkuu wa TOC tangu alipochaguliwa Septemba 30 mjini Dodoma.
Mkutano huo pia ulijadili mambo mbalimbali yakiwemo maandalizi ya Tanzania katika mashindano mbalimbali ya kimataifa kwa mawaka 2018 yakiwemo yale ya Jumuiya ya Madola itkayofanyika Gold Coast, Australia.

Huo ni mkutano mkuu wa kwanza tangu kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa TOC Desemba mwaka jana mjini Dodoma.



Saturday, 9 December 2017

Ukata wakwamisha kufanyika Taifa Cup ya netiboli

Na Mandishi Wetu, Zanzibar
MASHINDANO ya Kombe la Taifa ya netiboli yaliyopangwa kuanza kesho mjini Arusha, yameahirishwa kwa sababu ya ukata, imeelezwa.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta) Judith Ilunda, amesema leo kwa njia ya simu kutoka jijini Dar es Salaam kuwa, mashindano hayo sasa yatafanyika kuanzia Desemba 16 hadi 23 mjini Arusha.

Alisma awali mashindano hayo yangeanza Desemba 10 hadi Desemba 19 na sasa baada ya kuahirishwa yatamalizika Desemba 23 kenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Ilunda alisema kuwa chama chake kinahitaji kiasi cha sh milioni 29 kwa ajili ya kuendeshea mashindano hayo, ambayo hushirikisha timu za mikoa.

Alisema tayari wamepiga hodo kwa wadau mbalimbali wakiomba wawasaidie kupatikana kwa fedha hizo ili waweze kufanikisha mashindano hayo muhimu.

Alisema kuwa Chaneta inakabiliwa na ukata licha ya uongozi huo mpya kukutana majukumu mengi tangu uiongie madarakani miezi michache iliyopita mjini Dodoma.

Chaneta ilipoingia madarakani imeendesha kwa mafanikio mashindano ya Ligi Daraja la Kwanza yaliyofanyika kwenye viwanja vya Jakaya Kikwete jijini Dar es Salaam na timu saba kupanda daraja.


Mkutano Mkuu TOC kufanyika kesho Zanzibar

Na Mwandishi Wetu
MKUTANO Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) unafanyika kesho mjini hapa, imeelezwa.

Huo ni Mkutano Mkuu wa kawaida wa mwaka, lakini ni wa kwanza tangu kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu mjini Dodoma Desemba 18 mwaka jana.

Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi alisema leo Jumamosi mjini hapa kuwa, tayari maandalizi ya mkutano huo yameshakamilika na wajumbe walianza kuwasili tangu jana kwa ajili ya mkutano huo utakaofanyikia katika Kituo cha Amani Welezo.

Alitaja baadhi ya ajenda zitakazojadiliwa katika mkutano huo mkuu kuwa ni pamoja na mahudhurio, kuthibitisha ajenda, kuthibitisha na kupitisha Mkutano Mkuu wa Uchaguzi 2016, salamu za Rais, TOC.

Bayi alizitaja ajenda nyingine kuwa ni pamoja na taarifa ya shughuli za Kamati ya Utendaji ya TOC kwa mwaka huu na kupitia na kupitisha kalenda ya shughuli za TOC kwa mwaka 2018.


Nyingine ni taarifa ya Mhazini Mkuu kuhusu mahesabu yaliyokaguliwa 2016, kupokea na kupitisha rasimi ua bajeti ya TOC kwa mwaka 2018 na mengineyo kwa ruhusa ya mwenyekiti wa Mkutano Mkuu.

SuperSport kuonesha Ligi ya Mabingwa kupitia DSt


Na Mwandishi Wetu
MAGWIJI i wa kuonyesha michezo kote barani Afrika – SuperSport imethibitisha rasmi kupata idhini ya kuonEsha  moja ya michuano maarufu kabisa ya soka ulimwenguni -  Kambe la UEFA , ambapo sasa michuano hiyo itaonekana mubashara kupitia DStv na hivyo kuwawezesha mamilioni ya watazamaji kote barani Afrika kushuhudia michezo hiyo.

Hivi karibuni, SuperSport ilishiriki katika zabuni ya kupata idhini ya kuonyesha michuano hiyo na hatimaye kuthibitisha kupata idhini ya kuendelea kuonyesha michuano hiyo kwa miaka mitatu ijayo kuanzia msimu wa 2018/19.


“Hii ni siku ya Furaha na muhimu sana kwa SuperSport na wateja wetu wote wa DStv” amesema Mtendaji Mkuu wa SuperSport Gideon Khobane na kuongeza kuwa michuano ya UEFA ni moja ya mashindano makubwa na yanayoshirikisha timu maarufu na wachezaji nyota wengi sana hivyo itakuwa ni burudani ya aina yake kwa watazamaji wa DStv kote barani Afrika. Amesema kama kawaida, kupitia DStv, watazamaji wataona michuano hiyo mubashara tena kwa muonekano wa kiwango cha juu..

Friday, 8 December 2017

Guardiola Hafikirii kuvunja rekodi kwa sasa


MANCHESTER, England

KOCHA wa Manchester City Pep Guardiola anasema kuwa nafasi ya kueka historia haiku katika mawazo yake wakati anajiandaa kwa derby ya Jumapili dhidi ya wapinzani wao wakubwa Manchester United.

Endapo Man City atashinda mchezo huo utakuwa huo ni ushindi wao wa 14 mfululizo wa ligi, ukiwa ni rekodi kwa timu kushinda idadi hiyo ya mechi katika msimu mmoja wa Ligi Kuu.

Hatahivyo, Guardiola anasema kuwa kwa sasa anaangali jinsi atakavyopanga mipango yake kuhakikisha anakifunga kikosi cha kocha Jose Mourinho.

"Rekodi itaunjwa, lakini nachoangalia ni jinsi gani tutashida mchezo huo, alisema.

"Ikiwa unacheza mchezo mmoja alafu unafikiria kuhusu rekodi basi utasahau nini unachotakiwa kufanya.

NANI ATASHINDA MCHEZO?

Hii ni derby ya kwanza tangu Aprili mwaka 2013 ambako klabu hizo mbili zilipokutana wakati zikishikilia nafasi mbili za kwanza katika msimamo.

Endapo Man City itashinda kwenye Uwanja wa Old Trafford watakaa pointi 11 zaidi ya United ambao watapunguza hadi kubaki pointi tano, endapo watashinda mchezo huo.

Guardiola anaamini kuwa ni mapema mno kuamua nani atashinda ,chezo huo.

"Kushinda, kutoka sare au kushindwa Jumapili, hatuendi kushindwa au kushinda Ligi Kuu. Ni Desemba, alisema.


"Kuna pointi nyingi za kuzitafuta, zaidi ya 70, Kwa sasa tunaangalia mchezo huo.

Waziri Prof. Mbarawa awabana wadaiwa JNIA

Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (katikati mbele) akiwa katika chumba cha mikutano cha Kampuni ya ujenzi ya Kimataifa ya Uholanzi (BAM) linalojenga Jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBIII) alipofanya ziara. (Wa kwanza kushoto) ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela na (wa kulia) ni Balozi wa Uholanzi nchini, Jeroen Verheul.
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbarawa amewataka wadau wanaofanya shughuli mbalimbali zinazohusisha na kodi ya pango kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa Julius Nyerere (JNIA), kuhakikisha ifikapo Februari 1, 2018 wawe wameshalipa madeni yao.

Mkandarasi wa mradi wa jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Bw. Wolfgang Marschick (katikati kushoto) akitoa maelezo ya ujenzi huo leo. Wa pili kushoto ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbarawa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanza nia (TAA), Bw. Richard Mayongela.
Prof. Mbarawa alisema leo wakati alipoongea na wadau hao kwenye ukumbi wa watu Mashuhuri wa JNIA-TBII, wakati walipozungumza nao kujadili masuala mbalimbali.

Alisema baadhi ya wadau wameshalipa madeni yao kati ya bil 10 zilizokuwa zinadaiwa na sasa zimesalia bil. 3.7 ambapo amewataka baada ya kumalizika kwa sherehe za Krismas na Mwaka Mpya wahakikishe wanakamilisja madeni yao.

Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe.Prof. Makame Mbarawa (kushoto) akifurahia jambo na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela wakati walipokuwa wakitembelea ujenzi wa jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBIII). Nyuma ni Kaimu Mkurugenzi wa JNIA, Bw. Johannes Munanka.
“Hatutasita kumuondoa mtu yeyote atakayekuwa akiendelea kudaiwa kwani atakuwa hana sifa za kupangisha katika majengo haya ya viwanja vya ndege kwa kuanzia TBI na hapa TBII,” alisema Prof. Mbarawa.

Hatahivyo, aliyapongeza mashirika na ofisi ambazo zimekuwa zikilipa kwa wakati fedha za pango, ambapo uaminifu huo utawasaidia kupata nafasi katika jengo jipya la la tatu la abiria, ambalo litakuwa linauwezo wa kuhudumia abiria milioni sita (6) kwa mwaka.

Pia amewataka wale wasiowaaminifu wachague kulipa madeni ya pango au wanaodaiwa na serikali au kuondoka, ili kutoa nafasi kwa Watanzania wengine ambao wanania ya dhati ya kufanya biashara na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), wasimamizi wakuu wa viwanja vya serikali.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Richard Mayongela alisema tayari zabuni mbalimbali zimeshatangazwa na kuwataka wadau waliowaaminifu kujitokeza kuwania na kupata nafasi ya kufanya shughuli zao kwenye eneo la JNIA.

“Tumeshatangaza zabuni hizo na kama mhe. Waziri alivyosema zitakuwa za uwazi zikishirikisha wataalamu na tunauhakika watapatikana watu wenye mapenzi mema ya kufanya biashara na serikali” alisema Bw. Mayongela.
Katika hatua nyingine, Prof. Mbarawa alitembelea mradi wa ujenzi wa jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBIII) na kuridhishwa na kasi ya ujenzi, ambapo amewapongeza TAA, Tanroads na Kampuni ya ujenzi ya Kimataifa ya Uholanzi (BAM).


Naye Kaimu Mkurugenzi wa TAA, Bw. Mayongela, alisema kukamilika kwa jengo hilo kutatoa fursa nyingi za biashara zikiwemo uwekezaji katika hoteli, kumbi za mikutano, ofisi, migahawa, maduka makubwa ya bidhaa mbalimbali, huduma za kifedha (benki) na karakana za ndege.



Mkutano Mkuu wa Kawata wafunguliwa Zanzibar


Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
WACHEZAJI wametakiwa kuongeza jitihada katika mazoezi ili kupata nafasi ya ushiriki Michezo ya Olimpiki na kupata sifa ya kuwemo katika Kamisheni ya Wachezaji Tanzania (Kawata), imeelezwa.

Hayo yalielezwa jana mjini hapa na Makamu wa Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Henry Tandau wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Kawata katika ukumbi wa mikutano wa Amani, Welezo.

Makamu wa Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Henry Tandau na Katibu wa Kamisheni ya Michezo Tanzania (Kawata), Amina Ahmed.
Tandau ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) alisema kuwa, idadi ya wajumbe wa Kawata itapungua baada ya wajumbe wengi kukosa sifa, kwani wanaotakiwa ni wale tu walioshiriki Michezo ya Olimpiki.

Kawata ilikuwa inaundwa na wachezaji hai kutoka vyama au mashirikisho mbalimbali ya michezo nchini, bila kujali kama wameshiriki Olimpiki au la.
Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi akizungumza katika mkutano Mkuu wa Kawata Zanzibar leo.
Tandau alisema kuwa wamepokea walaka kutoka Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) unaoagiza kuwa kuanzia sasa wajumbe wa kamati za wachezaji ni wale tu watakaokuwa wameshiriki Olimpiki.

Alisema mjumbe atakuwa halali kwa vipindi itatu tangu alliposhiriki Olimpiki ya mwisho na baada ya hapo atastaafu kuwa mjumbe wa kamati hiyo.

“Hii ya mjumbe kuwa halali baada ya Olimpiki tatu tangu aliposhiriki ile ya mwisho ilikuwepo, lakini kipya ni lazima mjumbe wa Kawata awe ameshiriki Michezo ya Olimpiki, “alisema Tandau.

Alpoulizwa baada ya mkutano huo kutokana na walaka huo haoni kuwa wajumbe wa Kawata watapungua sana kwa kuwa vyama ingi vimeshindwa kupeleka wachezaji katika Olimpiki, Tandau alikiri hilo na kuwataka kufanya jitihada ili kushiriki michezo hiyo.

Wakati huohuo,  Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi alisema wamesikitishwa na kitendo cha baadhi ya vyama vya michezo kushindwa kuleta wajumbe katika mkutano huo wa Kawata licha ya kugharamia kila kitu.
Baadhi ya wajumbe wa Kawata katika mkutano mkuu leo Zanzibar.
Baadhi ya vyama hivyo ni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) na vingine.




Saturday, 2 December 2017

Uhamiaji, JKT Mbweni hapatoshi fainali netiboli Muungano

Na Cosmas Mlekani

MABINGWA watetezi wa taji la netiboli la Ligi Kuu ya Muungano, Uhamiaji kesho itacheza na mabinga wa Tanzania Bara JKT Mbweni katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Gymkhana mjini Zanzibar.

Uhamiaji walipata nafasi hiyo ya kucheza fainali baada ya kuifunga KVZ ya Zanzibar kwa mabao 55-41 katika mchezo ulijaa msisimko kwenye uwanja huo.

Katika mchezo huo Uhamiaji ilianza vizuri badaa ya kumaliza robo ya kwanza ikiwa mbele kwa mabao 14-7, na KVZ ikijitutumua na kulazimisha sare ya 12-12 na ile ya tatu, Uhamiaji ikarudi tena katika uongozi baada ya kumaliza ikiwa mbele kwa 15-11.

Nayo JKT Mbweni imetinga fainali kwa mbinde baada ya kuifunga kwa tabu Jeshi Stars pale ilipoibujka na ushindi kiduchu wa mabao 34-33 huku Jeshi Stars wakiongoza katika robo ya kwanza kwa mabao 9-6.

Hatahivyo, JKT Mbweni walkitumia uzoefu wao na kupata ushindi wa mabao 20-15 katika robo ya pili na kushida tena katika robo ya tatu kwa mabao 27-26 kabla ya robo ya nne JKT Mbweni kushinda 34-33.

MPAMBANO WA MARUDIO

Mpambano huo wa fainali kesho utakumbusha ule wa mwezi uliopita wa Ligi Daraja la Kwanza kwenye Uwanja wa Chuo cha Ushirika Moshi wakati Uhamiaji ilipotoka sare na JKT Mbweni kabla ya kufungwa na Jeshi Stars na kupoteza ubingwa wa Bara.

Kwa hiyo katika mchezo huo wa kesho, hakuna gtimu itakayokubali kufa kirahisi kwani kila moja itataka kudhihirisa kuwa bado wamo na haitakubali kufa kikondoo.

Kabla ya fainali kutakuwa na mchezo wa kusaka mshindi wa tatu wakati KVZ itakapochuana na Jeshi Stars katika mchezo utakaofanyika kuanzia saa 8:00 Mchana.


Mashindano hayo ya Ligi ya Muungano mbali na Uhamiaji, JKT Mbweni, Jeshi Stars na KVZ, timu zingine zilizoshiriki ni pamoja na Afya, JKU na Mundu za Zanzibar wakati zingine ni Polisi Moro na Polisi Arusha huku Madini Arusha ikishindwa kushiriki.