Monday, 26 November 2018

Kasi ya Yanga Africans yazitisha Simba, Azam FC

Wachezaji wa Yanga, Mrisho Ngassa (kushoto), Kaseke na Ibrahim Ajibu wakifurahia moja ya mabao yao katika Ligi kuu Tanzania Bara.

Na Mwandishi Wetu, Bukoba
 KASI ya mabingwa wazamani wa soka Tanzania Bara, Yanga imezidi kuwatia hofu baada ya kuendeleza ushindi katika mechi za ugenini kwa kuifunga Kagera Sugar kwa mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa kaitaba mjini hapa.

Yanga wiki iliyopita ilianza mechi za ugenini kwa ushindi kama huo dhidi ya Mwadui ya Shinyanga katika mchezo mwingine wa ligi hiyo uliofanyika kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Wadau wengi wa soka zikiwemo Simba na Azam, walitegemea kuwa Yanga itakapoanza kucheza mechi za ugenini itapunguzwa kasi yake katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini timu hiyo imeonekana kutopoa na kuendeleza makali yake hata ugenini.

Huo ni ushindi wa pili wa Yanga ugenini na Kanda ya Ziwa baada ya wiki wili iliyopita kuibuka na ushindi kama huo dhidi ya Mwadui ya Shinyanga katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Kambarage.

Ushindi huo wa jana uliopatikana kupitia kwa wachezaji wake, Heritier Makambo na Raphael Daud yalitosha kabisha kuiwezesha Yanga kuibuka na ushindi huo na kuondoka na pointi zote tatu na kufikisha pointi 32, moja nyuma ya vinara Azam FC baada ya kucheza mechi 12 sawa na watani zao Simba waliopo nafasi ya tatu wakiwa na pointi 27.

Makambo aliandika bao la kwanza katika dakika ya 21 kwa kichwa akipokea pasi kutoka kwa Haji Mwinyi huku lile la kusawazisha la Kagera Sugar likiwekwa kimiani na Ramadhani Kapera.

Penalti hiyo ilitolewa na mwamuzi baada ya kipa wa Yanga kumchezea vibaya Jacob Ningo aliyekuwa akijaribu kufunga.

Yanga ilijihakikishia ushindi katika dakika ya 74 kwa bao la Daud, ambaye alijaza mpira kwa kichwa baada ya Pango Godfrey kupiga mpira uliomkuta mchezaji mmoja wa Yanga aliyepiga mpira kwa kichwa uliomkuta mfungaji aliyeujaza kimiani.

Yanga imehitimisha viporo vyake vizuri baada ya kushinda mchezo huo wa jana ugenini wakati ikielekea kukamilika duru la kwanza.

Msimamo
  
                                                 P        W       D        L        GF      GA      +/-    Pts    

 Azam                                     13       10      3        0       17       3        14       33     

Yanga                                     12       10      2        0       21       6        15       32     

 Simba                                     12       8        3        1         23      4        19       27     

 Mtibwa                                    14       7        2        5        17       11        6        23     

 Coastal                                    14       5        7        2        11        9        2        22     

 JKT Tanzania                          13       4        7        2        7        6        1         19      

 Mbeya City                              14       5        4        5        15       16       -1       19      

 Mbao                                         13       5        4        4        10      11        -1       19      

 Singida United                       14       5        3        6        12       14       -2      18      

 Kagera Sugar                         14       3        8        3        11        11        0       17      

 KMC                                             13       3        7        3        10      7        3        16      

 Ruvu Shooting                        14       4        4        6        13       21       -8      16      

 Stand United                             14       4        2        8        14       21       -7      14      

 Lipuli                                             14       2        7        5        7        10      -3      13      

 Mwadui                                       14       3        4        7        9        13       -4      13      

 Ndanda                                      14       3        4        7        9        20      -11      13      

 Alliance                                     14       3        4        7        8        19       -11      13      

 African Lyon                             13       2        5        6        9        13       -4      11       

 Tanzania                                    14       1         7        6        7        11        -4      10     

 Biashara United                     13       1         7        5        5        9        -4      10


Wachoraji wa Jengo la Abiria Uwanja wa Ndege Mwanza Watakiwa Kuharakishwa



Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe jana akipata maelezo ya ujenzi wa Jengo la mizigo la Kiwanja cha Ndege cha Mwanza kutoka kwa Mhandisi Mkazi wa Kampuni ya Unetec ya Dubai, Geofrey Asulumenye (aliyenyoosha mkono. Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri (MAB) ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mhandisi Prof. Ninatubu Lema.
Na Mwandishi Wetu, Mwanza
WACHORAJI wa jengo jipya la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Mwanza, wametakiwa kuharakisha ili serikali itangaze zabuni na ujenzi uanze mara moja.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe amesema jana mkoani hapa alipokuwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miundombinu ya kiwanja hicho ambayo ipo kwenye maboresho makubwa.

Baadhi ya vyumba katika jengo la mizigo la Kiwanja cha Ndege cha Mwanza ambalo linaendelea kujengwa, jana Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe alitembelea na kuridhika na maendeleo ya ujenzi.
Mhe. Kamwelwe amesema kukamilika kwa michoro hiyo ya jengo la kisasa kutasaidia serikali kupitia wasimamizi wa ujenzi huo Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kutangaza zabuni na kupatikana kwa mkandarasi atakayejenga jengo hilo.

“Kiwanja cha ndege kinashughuli nyingi na jengo la abiria ni kityu muhimu sana, hivyo ninaharakisha hao wachoraji wajitahidi kufanya haraka ili kukamilisha michoro hiyo,” amesisitiza Mhe. Waziri.

Hatahivyo, amesema ameridhishwa na mradi wa ujenzi wa jengo la mizigo ambalo lipo mita chache kutoka eneo la abiria, ambapo ndege za mizigo zimejengewa maegesho yake rasmi tofauti na awali zilikuwa zikishusha upande wa ndege za abiria.


1.        Mhandisi Simon Makoye (mwenye kofia ngumu),  akimuonesha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (katikati), mchoro wa eneo linapojengwa rada, jana alipotembelea na kukagua maendeleo ya miradi inayoendelea kwenye Kiwanja cha Ndege cha Mwanza.


Halikadhalika ametembelea jengo la kisasa la kuongozea ndege, ambalo nalo limekamilika kwa asilimia 90 na kuridhishwa na utendaji wa Mhandisi Mkazi, Godfrey Asulumenye wa Kampuni ya Unetec ya Dubai, pamoja na eneo linapojengwa rada.

“Nimeridhika kuna maendeleo kwa kiasi kikubwa tofauti na nilivyopita awali, sasa kuna tofauti maboresho yamekamilika kwa asilimia kubwa na imebaki sehemu za kumalizia tu, ninaimani kwa kiasi kikubwa mkandarasi huyu atakamilisha kwa wakati na kuboresha zaidi sehemu ambazo wanaona hazijakaa sawa kabla ya kukabidhi,” Mhe. Kamwelwe.

Mhandisi Asulumenye amesema maboresho hayo yamehusisha ujenzi wa jengo la mizigo, jengo la kuongozea ndege, Kituo cha umeme, urefushaji wa barabara ya kutua na kuruka kwa ndege kwa mita 700 na ikikamilika itakuwa na urefu wa kilometa nne.


1.        Mhandisi Mkazi wa Kampuni ya Unetec ya Dubai, Geofrey Asulumenye (kushoto) akimpa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe maelezo mbalimbali ya ujenzi wa Jengo la kuongozea ndege la Kiwanja cha Ndege cha Mwanza wakati alipofanya ziara jana.

Maboresho mengine kwa mujibu wa Mhandisi ni pamoja na uwekaji wat aa za kuomgozea ndege (AGL), mifereji mikubwa ya kupitisha maji ya mvua, maegesho ya ndege, mifumo ya maji taka na matenki ya maji safi.

Kiwanja cha Ndege cha Mwanza kwa sasa ni daraja la 4C kinauwezo wa kuhudumia ndege za abiria 300 na maboresho yakikamilika kitapanda na kuwa daraja la 4D. Takwimu zinaonesha kinahudumia abiria 500,000 kwa mwaka ila matarajio ni kufikia abiria milioni mbili baada ya maboresho kukamilika.

Neymar, Mbappe Kuiongezea Nguvu PSG Ikiivaa Liverpool


PARIS, Ufaransa
KOCHA wa timu ya Paris Saint-Germain (PSG), Thomas Tuchel amesema kuwa washambuliaji wake nyota wawili, Neymar na Kylian Mbappe watakuwa tayari kwa ajili ya kukabili Liverpool katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

Wawili hao waliumia wakati wakizichezea tiu zao za taifa na walikosa mchezo wa PSG, ambayo ilishinda bao 1-0 dhidi ya Toulouse lakini Tuchel alisema kuwa ana matumaini wachezaji hao wawili watakuwemo katika kikosi cha PSG kesho Jumatano.

"Wanaendelea vizuri siku hadi siku, tuna muda kabla ya Jumatano. Ni jambo zuri kwetu. Nafiiri wataweza kucheza, “alisema Mjerumani huyo katika mahojiano katika kipindi cha televisheni cha Telefoot.

PSG wana pointi tano baada ya raundi nne za mechi za Ligi ya Mabingwa wa Ulaya hatua ya makundi na ushindi wa mchezo huo wa katikati ya wiki kwa kocha Jurgen Klopp na ule wa Napoli iliyopo katika nafasi ya pili, utawaondoa mabingwa hao wa Ufaransa katika hatua ya makundi kwa mara ya kwanza tangu waliporejea katika mashindano makubwa Ulaya mwaka 2012.
--
Wakati huohuo, mabingwa wa England Manchester City leo Jumanne wanaifuata Lyon ya Ufaransa katika mchezo mwingine wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

Man City ilihitaji kuvunja benki na kutumia kiasi cha pauni milioni 80 kwa ajili ya kuwasajili John Stones na Nicolas Otamendi wakati nahodha wake Vincent Kompany akirejea katika ufiti baada ya kuwa majeruhi kwa muda.

Wakati akirejea kutoka Athletic Bilbao, Laporte alitumia muda kuzoea mazingira katika mechi tatu walizocheza nje ya uwanja wa nyumbani zikishia kwa vipigo wakati wakimaliza msimu.

Friday, 23 November 2018

Serikali yakifikiria kupanua Kiwanja cha Ndege Bukoba


1.   Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Isack Kamwelwe akipita eneo la ukaguzi wa abiria na mizigo la Kiwanja cha Ndege cha Bukoba, leo alipofanyua ziara ya kikazi. Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushari (MAB) ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mhandisi Prof. Ninatubu Lema.

 Na Mwandishi Wetu, Bukoba
SERIKALI inafikiria kufanya upanuzi na urefushaji wa barabara ya kutua na kuruka kwa ndege ya Kiwanja cha Ndege cha Bukoba licha ya changamoto zilizopo, ili kiruhusu kutua kwa ndege kubwa zaidi.

Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe katika ziara yake ya kikazi ya kukagua miundombinu ya taasisi zilizopo chini ya Wizara yake, ambapo kiwanja hicho kipo chini ya Mamlala ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).

Mhe. Kamwelwe alisema bado Kiwanja hicho kinakabiliwa na changamoto endapo kitaongezwa lazima baadhi ya nyumba za Ibada, hospitali na nyumba za kuishi watu zitalazimika kuondolewa ili kupisha upanuzi huo.

“Ukiangalia upande mmoja una makazi ya watu na upande mwingine ni Ziwa Viktoria na mwingine kuna Mlima, hivyo bado tunafanyia kazi hizi changamoto na endapo zitatatuliwa, basi miundombinu hii itaboreshwa zaidi kwa kuwa tayari lipo jengo zuri na lenye mfumo mzuri wa maji taka na mifumo mingine mbalimbali,” amesema Mhe. Kamwelwe.


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Isack Kamwelwe (kulia) leo akimsikiliza Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Bukoba, Bi. Doris Uhagile (katikati), akimpa maelezo mbalimbali wakati alipofanya ziara ya kikazi kwenye kiwanja hicho. Mwenye tai nyekundu ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela na kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Mhandisi Richard Ruyangu.

Hata hivyo, alisema Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) litaongeza safari zake mara mbili kwa siku wenye Kiwanja cha ndege cha Bukoba, kutokana na kuwa na abiria wengi kwa sasa.

Mhe. Kamwelwe alisema kwa sasa ndege hiyo aina ya Bombardier Q400 inakuja mara moja kwa siku kwa kila siku kuanzia Jumatatu hadi Jumapili.

“Kwa sasa abiria wameongezeka zaidi nimeelezwa kuwa kwa mwaka ilikuwa kiwanja kinaweza kuhudumia abiria 28,000 pekee, lakini sasa ni zaidi ya 45,000 kwa mwaka, hivyo inaonesha ni kiasi gani wanavyoongezeka na ndio maana ninasema kutakuwa na uwezekano wa kuongeza safari za ATCL na iwe mara mbili kwa siku balada ya sasa mara moja,” alisema Mhe. Kamwelwe.


1.   Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Bukoba, Bi. Doris Uhagile (katikati) leo akiwa eneo la ukaguzi wa tiketi za abiria ambapo alitoa maelezo ya namna mashirika ya ndege yavyohudumia abiria kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Isack Kamwelwe. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Richard Mayongela, akifuatiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri (MAB) ya TAA, Mhandisi Prof. Ninatubu Lema.

Alisema serikali tayari imenunua ndege mbili aina ya Airbus 220 zenye uwezo wa kubeba abiria 132 zitakazowasili nchini Desemba 18 na 23, 2018 tayari kwa safari za maeneo mbalimbali.

Ndege hizi zinaweza kutua kwenye viwanja vya ndege vya daraja la 4C, ambapo kwa sasa ni Songwe na Mwanza, na baada ya ukarabati kukamilika kwenye kiwanja cha Mtwara na kuboreshwa kwa Kigoma, pia itaweza kutua; hali kadhalika pia itatua kwenye viwanja vya Kimataifa vya Julius Nyerere (JNIA) na Kilimanjaro (KIA), ambavyo ni daraja la 4E.

Kiwanja cha Ndege cha Bukoba kinajengo la kisasa la abiria, ambalo lilizinduliwa Desemba 2017 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Mhe. John Pombe Magufuli, ambapo mbali na ATCL ndege nyingine zenye ratiba maalum zinazotua ni pamoja na Precision, wakati nyingine zinakuwa zimekodiwa bila kuwa na ratiba maalum kama Auric.


Thursday, 22 November 2018

BMT yaitaka RT kutumia vizuri mashindano ya wanawake

Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa, BMT, Alex Nkenyenge akizungumza na waandishi wa habari kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam kuhusu mashindano ya taifa ya riadha ya wanawake. Kulia ni Mwakilishi Mkuu wa Shirika la Misaada ya Kimaendeleo la Japan Tanzania, Jica, Toshio Nagase. Kushoto ni Katibu Msaidizi wa RT, Ombeni Zavalla.

Na Mwandishi Wetu
BARAZA la Michezo la Taifa (BMT), limelitaka Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) kutumia mashindano ya taifa ya riadha ya wanawake kuchagua timu ya wanariadha watakaoenda kushiriki mashindano ya kufuzu kwa Michezo ya Olimpiki 2020 itakayofanyika Tokyo, Japan.

Mashindano hayo ya pili ya taifa ya wanawake, ambayo yanajulikana kama JICA Ladies First, yatafanyika kwenye Uwanja Taifa Jijini Dar es Salaam kwa siku mbili kuanzia Jumamosi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Katibu wa BMT Alex Nkenyenge alisema, jumla ya wanariadha 155 wanatarajia kujitokeza kushiriki katika mashindano hayo.

Nkenyenge alisema kuwa mashindano hayo ni muhimu kwa sababu yatawasaidia RT kugundua vipaji vya riadha, ambavyo watavitumia katika mashindano mbalimbali ya kufuzu kwa michezo ya Olimpiki.

"Hii ni nafasi muhimu  kwa RT kuchagua wanariadha wenye viwango kwasababu mwakani kuna mashindano ya kufuzu kushiriki michezo ya Olimpiki," alisema Nkenyenge.

Alisema kutokana na hilo, Kamati ya RT iwe makini kwenye mashindano hayo ili kupata wanariadha watakaofanya vizuri na kufikia viwango, ambavyo vitawasaidia kwenda kushinda katika mashindano mbalimbali ya kufuzu kwa Olimpiki yanayotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Riadha (IAA).

Alisema mpaka sasa mikoa yote imethibitisha kushiriki katika mashindano hayo ambayo mwaka jana ilishirikisha wanariadha wanawake 123 kutoka mikoa 26 ya Bara na Visiwani.

Naye Mwakilishi Mkuu wa JICA, Toshio Nagase alisema mashindano haya ni muhimu kwa Tanzania hususani wanariadha wakike kwa sababu yanatoa nafasi ya wao kwenda Japan kushiriki mbio mbalimbali nchini humo.

Mbali na hilo alisema ushiriki wa mashindano hayo, unawasaidia  wanariadha kuinua vipaji vyao kutokana na kwenda nje ya nchi katika.mashindano ya kirafiki ambayo ni moja ya mazoezi ya kujiandaa na michuano mbalimbali ya kimataifa, yakiwemo yale ya kufuzu Olimpiki ya 2020.

"Nimefurahia kuona mwitikio wa mikoa ni mkubwa, tutaendelea kushirikiana ili kuinua vipaji vya wanariadha wa Tanzania," alisema Nagase.

Kwa upande wa Katibu msaidizi wa RT, Omben Zavalla alisema wanakila sababu ya kuwashukuru JICA kwa sababu wamefanya jambo kubwa kwa RT pamoja na maendeleo ya riadha kwa ujumla.

"Huu ni ushirikiano mzuri sana kwasababu unasaidia kuibua vipaji vya wanariadha mbalimbali kutoka mikoani," alisema Zavalla.

Alisema wanariadha waliochaguliwa kuwakilisha mikoa yao washindani kwa bidii ili kuonesha uwezo wao.

Mashindano hayo yanatarajia kuanza kesho huku wanariadha 155 wanatarajia kushiriki,ambapo kutakuwa na mbio za mita 100,200, 400, 800, 1,500 na meta 10,000 sambamba na kurusha mkuki.

Jica ndio wadhamini wa mashindano hayo, ambayo yaliadhishwa baada ya mwanariadha wa zamani kwa kushirikiana na RT kuiomba Jica idhamini ili Tanzania iwe na wanariadha wengi katika Olimpiki ya 2020.


Friday, 16 November 2018

Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi wajifunza mengi TB3




1.        Wajumbe wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar leo wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kutembelea jengo la Tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere kwa ajili ya kujifunza.

Na Mwandishi Wetu

WAJUMBE wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar imekiri kujifunza mambo makubwa katika ujenzi wa jengo la Tatu la Abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TB3), imeelezwa.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, ambayo ilikuwa na ziara kwenye jengo hilo na Mhe. Mohammed Said (Mwakilishi wa Mpendae), amesema ujenzi wa jengo hilo ni fundisho tosha kutokana na kwenda kwa kasi tangu ujenzi wake uanze Juni  2013, tofauti na ujenzi wa jengo la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Amani Abeid Karume umechukua takribani miaka 10 tangu mwaka 2009 lakini hadi sasa lina asilimia 39 pekee.

1.        Mhandisi Barton Komba wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), (aliyesimama mbele), leo akitoa maelezo ya maendeleo ya mradi wa jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere kwa Wajumbe wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar walipofanya ziara ya mafunzo.

Mhe. Said amesema TB3 ni jengo la kisasa kutokana na miundombinu yake ambayo mingi inaendeshwa kwa mifumo maalum, ikiwemo sehemu ya mizigo, ambayo inaendeshwa kupitia hatua tano.

“Katika ziara hii tumefarijika sana kwani tumejifunza mengi wenzetu walivyoweza kuufikisha mradi huu, kwa kweli tumechukua yote na tutakwenda kuishauri serikali namna bora ya kuendeleza ujenzi wa majengo na viwanja vya ndege kwa ujumla,” amesema Mhe. Said.

Hali kadhalika, Mhe Said amesema mbali na kutembelea jengo hilo, pia wamepata maelezo mazuri ya kiutendaji katika uendeshaji, ukusanyaji na mgawanyo wa mapato kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), na wataishauri serikali namna bora ya kudhibiti mapato.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Lawrence Thobias, ameishukuru kamati hiyo kwa kuichagua TAA kuwa sehemu yake ya mafunzo, kwa kuwa imezoeleka wengi wanaotaka kujifunza lazima waende nje ya nchi.

1.        Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Mohammed Said (aliyesimama katikati) pamoja na wajumbe wakimsikiliza Mhandisi Barton Komba wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) (aliyenyoosha mikono), akiwaelezea ujenzi wa jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere leo walipofanya ziara ya mafunzo. 

Bw. Thobias amesema TAA ikiwa ni moja ya taasisi za serikali chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, imekuwa ikijiendesha kwa kufuata sheria na taratibu za ukusanyaji wa mapato za serikali.

Akiwasilisha maendeleo ya mradi wa jengo la tatu la abiria, mmoja wa wasimamizi kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Burton Komba amesema hadi kufikia Oktoba 31, 2018 umefikia asilimia 85.53 na unatarajiwa kukamilika Mei 2019.

Mhandisi Komba amesema ujenzi wa jengo hilo ambalo litahudumia abiria milioni sita kwa mwaka, umehusisha eneo la maegesho ya ndege lenye mita za  mraba 227,000 lenye uwezo wa kuegesha ndege 19 za Daraja C kwa wakati mmoja zikiwa kwenye madaraja na eneo lisilokuwa na madaraja.

“Pia eneo hili linaweza kuegesha ndege za daraja E 11 mfano wa hii Dreamliner ya ATCL Boeing 787 na Boeing 777, ni eneo kubwa,” amesema.

Pia amesema kumejengwa maegesho ya magari mchanganyiko yasiyopungua 2075 kwa wakati mmoja; barabara za kuingia na kutoka eneo la jengo; uzio wa usalama, mifumo ya maji taka nay a mvua; ujenzi wa matanki ya kuhifadhia maji yenye ujazo wa lita milioni 2.26; kituo kikubwa cha umeme (33Kv); usimikaji wa jenereta saba zenye uwezo wa KvA 2000 kila moja; ujenzi wa mifumo ya kujaza mafuta kwenye ndege na kusimika mifumo ya mawasiliano na usalama.

Thursday, 15 November 2018

DStv yatangaza neema kwa wateja wake msimu huu wa sikukuu!


Meneja Masoko wa MultiChoice Tanzania Alpha Mria akizungumza jijini Dar es Salaam leo.
 
KATIKA msimu huu wa sikukuu ambapo watu wengi hujumuika na familia zao kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka, MultiChoice Tanzania imetangaza ofa kabambe kwa wateja wake na wale wanaojiunga na huduma za DStv kupitia kampeni yake maalum ijulikanayo kama ‘Ni Muda wa Kukiwasha na DStv’.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Meneja Masoko wa MultiChoice Tanzania Alpha Mria amesema wateja wa DStv sasa watapata burudani zaidi za kusisimua kupitia Soka, Filamu, Tamthilia, Katuni na vipindi mbali mbali vya watoto vitakavyoileta familia pamoja na kuimarisha upendo.
Msanii wa kujitegemea, Omary Mkali akitumbuiza wakati wa hafla ya Mult-choice leo.

Kwa mujibu wa Alpha, zaidi ya maudhui hayo yote yaliyotajwa hapo juu; Katika kunogesha sikukuu, maudhui mapya yatayoongezwa ndani ya DStv. 

Maudhui hayo ni pamoja na tamthilia ya Kapuni ambayo inaingia msimu wake wa pili katika chaneli ya Maisha Magic Bongo (MMB), Chaneli maalum (EA Movies) yenye mkusanyiko wa filamu bora za Afrika Mashariki, na pia sinema maalum za watoto katika chaneli ya Mnet inayojulikana kama Mnet ANIMANIA pamoja na vipindi mbalimbali vinavyohusiana na msimu huu wa sikukuu. 

Aidha, Alpha alisisitiza kuwa, Kipindi hiki cha sikukuu kupitia chaneli ya Maisha Magic Bongo (MMB) itawaletea wateja maudhui mapya na ya kusisimua zaidi, hivyo kuwasihi watanzania wakae tayari kupokea kitu kipya kutoka MMB tarehe 14 Disemba 2018.
Mkuu wa Mauzo wa kampuni hiyo Salum Salum akizungumza leo.
 Amesema DStv imekuwa mara kwa mara ikiwatunuku wateja wake waliopo na wapya zawadi na ofa kabambe huku wakiendelea kupata burudani ya uhakika muda wote. “Mwaka huu kama kawaida umekuwa mwaka wa neema kwa wateja kwani tumekuwa na mfululizo wa zawadi kwa wateja wetu”

Kwa wateja wapya wanaojiunga na DStv msimu huu watapata ofa maalum ya kuunganishwa kwa shilingi 79,000 pamoja na zawadi maalum ya kifurushi cha mwezi cha Bomba bila malipo ya ziada. Ofa hii itaendelea kwa muda wa miezi miwili kuanzia tarehe 15 Novemba 2018 na ni kwa nchi nzima.
Malkia wa Mipasho Afrika Mashariki, Khadija Omary Kopa.
 Akifafanua kuhusu ofa hiyo, Mkuu wa Mauzo wa kampuni hiyo Salum Salum, amesema kuwa ofa hii ni zawadi ya kufunga mwaka kwa wateja wapya wa DStv kwani katika kipindi cha miezi miwili wataweza kuunganishwa na DStv kwa gharama ya shilingi 79,000 tu na zaidi ya hapo kupewa kifurushi cha Bomba cha mwezi mmoja bila malipo ya ziada.

“Mbali na kuongezwa kwa chaneli na maudhui kedekede kwa wateja walipo wa DStv, pia kwa wale ambao bado hawajajiunga hatujawasahau, sasa tunawapa ofa hiii kabambe ya kujiunga kwa gharama nafuu na zaidi ya hapo wapate kifurushi cha mwezi mmoja bila malipo. Hii ni zawadi yetu ya sikukuu kwa wateja wetu” alisema Salum Salum.

Johnson Mshana na Shumbana wakati wa hafla hiyo leo.
Amesisitiza kuwa ofa hii ni kwa nchi nzima na tayari wameshajipanga na mawakala wote kuhakikisha kuwa ofa hii inapatikana nchi nzima. “Mtu yeyote asiwe na wasiwasi wa jinsi ya kuunganishwa kwa ofa hii. Tunao mawakala wetu wa usambazaji na ufundi nchi nzima, hivyo hata walio maeneo ya vijijini huduma hii watapata.

Wakati huohuo, DStv leo imewakabidhi waandishi wa habari zawadi za ving'amuzi na dishi na kuahidi kuwafungia vifaa hivyo baada ya kujibu maswali vizuri kuhusu 'Ni Muda wa Kukiwasha na DStv’.


Thursday, 1 November 2018

Baraza la Michezo Laipa Yanga Wiki Tatu


Na Mwandishi Wetu
BARAZA la Michezo la Taifa (BMT) limetoa wiki tatu kwa klabu ya Yanga kuhakikisha wanachama wake wanajisajili upya katika matawi yote nchini kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu, huku ikilipa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) mwezi mmoja  kutangaza tarehe ya Uchaguzi Mkuu wa klabu hiyo.

Hivi karibuni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dr Harrison Mwakyembe alikutana na viongozi wa Yanga pamoja na wazee wa klabu hiyo kusikiliza kero zao.

Kaimu Katibu Mkuu wa wa BMT, Alex Mkeyenge alisema jana kuwa wamefanya hivyo baada ya wanachama wa Yanga kuwasilisha malalamiko yao  kwa Waziri, na baada ya kuwahoji wakafikia muafaka na ndipo suala hilo likarejeshwa kwa BMT.

Mkyenge alisema Yanga ni timu ya wananchi na inahitaji kutoa burudani kwa wanachana na wapenzi wake pamoja na kutoa ajira kwa wachezaji iliowasajili, hivyo migogoro haina nafasi kwa sababu inaua soka nchini.

Na ndio maana BMT imeamua kutoa agizo kwa viongozi wa Yanga pamoja na TFF ili litekelezwe kwa wakati huo.

"Tunaomba wale kwenye kadi za Benki ya Posta na CRDB wote watumie muda waliopewa kwenda kwenye matawi yao kwa ajili ya kujisajili," alisema kiongozi huyo wa BMT.
Kikosi cha Yanga.
Alisema lengo ni kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa amani na haraka ili Yanga wapete viongozi wao halali, ambao wataingia madarakani kwa kupigiwa kura.

Akizungumzia  tarehe ya uchaguzi alisema wameiagiza TFF kupitia kamati yake ndani ya mwezi mmoja watangaze tarehe ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Yanga.

Alisema anaamini TFF itafanya kazi kwa weledi ili kuhakikisha wananusuru migogoro midogo, ambayo inarudisha nyuma hadhi ya klabu hiyo, ikiwemo kushusha ari za wachezaji wake.

"Tunataka kuona Yanga kama ilivyokuwa mwanzo,sio malumbano tena wanachama wameshatoa.madukuduku yao wakitaka uchaguzi ufanyike, “alisema Mkeyenge.

Kwa upande wa Makamu wa Rais wa TFF Athuman Nyamlani alisema Kamati ya TFF iko kamili kwa ajili ya kusimamia uchaguzi huo, huku ikisisitiza ndani ya muda huo tarehe ya uchaguzi itatangazwa.

"Kila kitu safari hii kitakwenda sawa kwa sababu kila mtu Yanga anataka uchaguzi na hili sio suala la mtu mmoja, “alisema Nyamlani.

Alisema muda waliopewa inatosha sana kufanya walichoagizwa kwa sababu uchaguzi huo umeahirishwa mara nyingi kutokana na wanachama mwenyewe kutoelewana.

Alifafanua zaidi ya kuwa, Yanga inahitaji kuwaburudisha wanachama na mashabiki wake, hivyo anapoendekeza migogoro,wanashindwa hata kusajili nakuwatunza vizuri wachezaji.

Mwakyembe amkabidhi bendera Miss Tanzania 2018


Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imemtaka mwakilishi wa miss Tanzania kwenda kuitendea haki lugha ya Kiswahili katika mashindano ya miss word yaliyopangwa kufanyika China Desemba nane mwaka huu.

Hayo yalisemwa na  Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe wakati akimkabidhi bendera ya taifa Miss Tanzania, Queen Elizabeth (pichani), anayetarajia kuondoka Novemba 8 kwenda Sanya, China, ambako shindano hilo litafanyika.

Akizungumza Waziri Mwakyembe alisema Serikali kupitia Wizara yake haikabidhi bendera hovyo hovyo isipokuwa unapokabidhiwa lazima ukalitendee haki taifa lako.

Alisema kutokana na hilo, Queen Elizabeth anapaswa kwenda kufanya vizuri katika shindano hilo kubwa, ambalo litasaidia kuitangaza Tanzania vizuri kama tu atakitumia vizuri kiswahili katika mashindano hayo.
Mratibu wa shindano la Miss Tanzania na Mkurugenzi wa The Look Company, Bi. Basila Mwanukuzi.


Alisema kiswahili ni moja ya lugha kubwa duniani, kwa hiyo anapaswa kuitangaza kwenye mashindano hayo.

Mbali na hilo aliipongeza kampuni ya The Look, ambao  ni waandaaji wa mashindano hayo kwa kurejesha heshima ya Miss Tanzania na kuahidi kuboresha zaidi huku akiwasisitizia kuwa warembo wote wanaoshiriki shindano hilo watapata nafasi ya kufanyakazi katika Shirika la Ndege Tanzania, ATCL, na mashirika mengine, ambayo yatakuwa yatakuwa tayari kuwasaidia.

Wao kama Serikali wanaamini katika shindano hilo mrembo huyo atafanya vizuri na kuipeperusha vema.bendera  ya nchi.

Naye Elizabeth alisema anakwenda China kushindana na si kushiriki kwa hiyo Watanzania wategemee mambo makubwa kutoka kwake.

Alisema amejiandaa vizuri na shindano hilo na anaimani katika mashindano hayo atafanya vizuri ili kuitangaza nchi yake.

Kwa upande wa muandaa wa shindano la Miss Tanzania,  Basila Mwanukuzi alisema Elizabeth amefanya maandalizi ya kutosha ambayo kamati yake imejirisha kuwa anakwenda kushindana na so kushiriki.

Alisema kurejea kwa Miss Tanzania ambayo inasaidiwa na wadau wengi, kumelifanya shindano hilo lirudishe heshima yake kama ilivyokuwa awali.

Alisema anawashukuru wadhamini waliojitikeza kufanikisha, huku akiendelea kuomba wadhamini wengine wajitokeze zaidi kuwapiga jeki.