Sunday, 15 September 2019

Wafanyakazi TAA Watakiwa Kufanya Kazi Kwa Bidii


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mhandisi Julius Ndyamukama (kushoto), akimkabidhi zawadi ya ngao, Theobald Benigius wa Idara ya Uhandisi na Huduma za Ufundi katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius  Nyerere (JNIA) katika sherehe ya kuwaaga Wastaafu baada ya kustaafu kwa mujibu wa sheria na taratibu za Utumishi wa Umma.

Na Mwandishi Wetu
WAFANYAKAZI wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) wametakiwa kuchapa kazi kwa bidii ili kurudisha hadhi ya taasisi hiyo.

Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Mhandisi Julius Ndyamukama wakati akiwaaga wastaafu watatu wa mamlaka hiyo.

Hafla hiyo ilikuwa mahsusi kwa ajili ya kuwaaga wastaafu kutoka Idara ya Uandisi na Huduma za Ufundi ya Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA), ambao ni Mhandisi Theobald Benigius, Ernest Kivela na Bertha Kipenda, ambao wamestaafu kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma.

Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Paul Rwegasha akimkabidhi mmoja wa wastaafu wa Idara ya Uhandisi na Huduma za Ufundi wa JNIA, Mhandisi Bertha Kipenda zawadi ya vifaa vya mazoezi katika hafla ya kuwaaga iliyofanyika hivi karibuni Jijini Dar es Salaam.


Alisema kuwa juhudi, maarifa na upendo ndio vigezo vitatu, ambavyo ni chachu ya kuipandisha na kuirejesha kileleni taasisi hiyo, ambayo ilianza kupoteza hadhi mbele ya uso wan chi na jamii, tofauti na huko nyuma, ambako ilikuwa ikifanya vizuri zaidi.

Alisema kwa sasa hadhi ya taasisi hiyo imeshuka mbele ya uso wa nchi na kusababisha baadhi ya kazi ilizokuwa ikizifanya zamani, sasa kufanya na taasisi nyingine.

“Nashauri tupendane na tuchape kazi kwa bidii, kwani sura yetu kama TAA hapo katikati ilidorora kwani tumepoteza kazi nyingi, hivyo tukitaka kurudisha hadhi yetu kama itatakiwa kusukumana, tutafanya hivyo kwa lengo hilo, ingawa najua wapo ambao hawataki hivyo,” alisema.

Hatahivyo, amewashukuru watumishi wenzake kwa kumpokea vizuri tangu kuteuliwa kwake kuongoza taasisi hiyo takribani miezi sita iliyopita, ambapo amewataka kushirikiana zaidi.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mhandisi Julius Ndyamukama, akiongea na watumishi walioudhuria hafla ya kuwaaga watumishi wa Idara ya Uhandisi na Huduma za Ufundi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), waliostaafu hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Pia ameweka angalizo kwa Watumishi wote kuwa muda wote atakaokuwepo hapo kama Mkurugenzi Mkuu, atalazimika kuwasumbua na kuwasukuma, ili sura ya TAA iliyopotea, kurejea katika hali yake yazamani.

 “Tukitaka kurudisha hadhi yetu kama ilivyokuwa zamani hivyo itahusu tusukumane na kusumbuana kidogo nitaomba mnivumilie, lakini lengo likiwa ni kutaka kurudisha TAA ya zamani, ingawa najua wapo wasiotaka,” alisema.

Aliwapongeza wastaafu hao na kuwataka kendelea kufanya kazi huko waliko ili kuendelea kuziimarisha afya zao.

Kwa upande wake
Kaimu Meneja wa Idara ya Uhandisi na Huduma za Ufundi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Mhandisi Diana Munubi (kushoto), akimkabidhi zawadi picha ya ua Ernest Kevela (wa kwanza kulia) katika hafla ya kuwaaga wastaafu wa Idara hiyo iliyofanyika hivi karibuni Jijini Dar es Salaam.


Mkurugenzi wa JNIA, Paul Rwegasha alisema watumishi hao walikuwa na nidhamu kubwa na kufanya kazi kwa bidii, pasipo kuchoka wala kuwa na malalamiko, ambapo amewataka wengine waliobaki kuiga mfano huo uliotukuka.

Lakini, pia amewataka Wastaafu hao kuendelea kufanya mazoezi kwani wamekuwa wakifanya kazi ngumu wawapo katika kituo chao cha kazi cha JNIA.

Watumishi kutoka Idara na vitengo mbalimbali vya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), wakiserebuka kwa kucheza muziki katika hafla ya kuwaaga watumishi wenzao wa Idara ya Uhandisi na Huduma za Ufundi waliostaafu hivi karibuni.


Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Uhandisi na Huduma za Ufundi, Mhandisi Alex Kalumbete amesema wastaafu hao walikuwa na uvumilivu mkubwa katika utumishi wa umma kutokana na kazi ngumu walizokuwa wakifanya za kiuhandisi.

Kaimu Meneja Uhandisi na Huduma ya Ufundi JNIA, Diana Munubi amesisitiza upendo uendelee kuwepo baina ya watumishi kama vile wastaafu hao walivyokuwa wakiuenzi wakati wa utumishi wao wote wa umma.

Mmoja wa wastaafu hao, Bw. Theobald Benigius kwa niaba ya wenzake ameishukuru TAA kwa kuwezesha kufanya kazi vizuri hadi utumishi wao kukoma kwa kustaafu, na amewaomba watumishi wenzake kuwa wavumilivu na tabia njema kwani wataweza kustaafu vizuri
.

No comments:

Post a Comment